
MAWAZIRI wa mambo ya nje wa Urusi na Irani walijadili uwezekano wa kumaliza mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati kwa njia ya kidiplomasia. Wawili hao, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov na mwenzake wa Iran Abbas Araqchi, walifanya mazungumzo kuhusu namna ya kuhamisha mzozo huo kutoka uwanja wa kijeshi kwenda kwenye mazungumzo ya kisiasa na kidiplomasia. Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya nje ya Urusi, mawaziri hao walijadili kwa kina hali ya kisiasa na kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati, wakielezea kuwa mgogoro huo umetokana na kile walichokitaja kama uchokozi wa Amerika na Israeli dhidi ya Iran. Taarifa hiyo ilieleza kuwa wawili hao walibadilishana mawazo kuhusu uwezekano wa kufikia suluhisho la kudumu kwa kuzingatia sheria za kimataifa na maslahi ya nchi zote katika ukanda huo. Urusi ilieleza kuwa iliwasilisha misaada ya kibinadamu nchini Iran kama sehemu ya ushirikiano wao wa kimkakati unaojumuisha sekta za siasa, uchumi, kijeshi na nishati. Hata hivyo makubaliano hayo hayajumuishi ulinzi wa pamoja kati ya nchi hizo mbili. Wakati huo huo, leo (Jumapili) Pakistan itashirikisha Saudi, Uturuki na Misri kwenye mazungumzo kuhusu vita vya Iran, huku Islamabad ikijipanga kuwa mpatanishi kati ya Amerika na Iran kuhusu mgogoro huo. Kulingana na taarifa kutoka Wizaraya Mambo ya nje ya Pakistan,Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo nne watafanya majadiliano ya kina kuhusu masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na juhudi za kupunguza makali ya mivutano katika eneo hilo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, alisema mkutano huo utalenga kuanzisha utaratibu wa kupunguza mivutano. “Tutajadili mazungumzo na kuona yanaelekea wapi katika vita hivi na jinsi nchi hizi nne zinavyotathmini hali hiyo na nini kinaweza kufanyika,” alisema Fidan. Nchi hizo nne zimejaribu kupatanisha Washington na Tehran katika vita vilivyozuka Februari 28, na zote zinakabiliwa kwa kiasi kikubwa na hatari za usambazaji wa mafuta. Pakistan imewasilisha kwa Tehran pendekezo la Amerika la kumaliza vita huku maafisa wa Iran wakionyesha kuwa mazungumzo yatafanyika Pakistan au Uturuki. Rais wa Amerika Donald Trump anasema mazungumzo na Iran yanaendelea vizuri sana lakini Tehran imekanusha kufanya mazungumzo na Washington. Iran imekuwa ikiangalia vipengele 15 vya mapendekezo, ingawa afisa mmoja amelipinga akilielezea kuwa ni la upendeleo na lisilo la haki. Miongoni mwa masharti yake ni kuvunja mpango wa nyuklia wa Iran, kudhibiti maendeleo yake ya makombora na kwa kiasi fulani kukabidhi udhibiti wa Mkondo wa Hormuz. Katika mkutano uliofanyika mjini Istanbul, Fidan alisema mfumo mpya wa dunia wa nguvu nyingi unahitaji suluhisho la kulinda njia muhimu za nishati na biashara. Mnamo Machi 27, 2026, Trump kupitia ujumbe kwenye mtandao wa Truth Social,alisema mashambulizi yaliyokuwa yamepangwa dhidi ya miundombinu ya nishati ya Iran yamesitishwa hadi Aprili 6 akidai kuwa uamuzi huo ulifuatia ombi kutoka Iran. “Hata hivyo mazungumzo yanaendelea vizuri licha ya taarifa potofu,” alisema Trump. Iran imekanusha vikali madai ya kuwa katika mazungumzo ya moja kwa moja na Amerika huku viongozi wake wakisisitiza kuwa hawajakubali masharti yaliyowasilishwa kupitia mpango wa vipengele 15 uliopitishwa na Pakistan. Mashambulizi ya anga pia yameripotiwa kuendelea nchini Iran, huku watu sita wakithibitishwa kufariki katika eneo la Qom baada ya majengo kushambuliwa.
from Taifa Leo https://ift.tt/7RLyfWb
via
IFTTT