Genge la Chude Chude lahangaisha wakazi wa Ahero kwa uhuni na uporaji

WAKAZI wa Ahero eneobunge la Nyando, Kaunti ya Kisumu wamelalamikia utovu wa usalama ambao umewaacha wengi wao wakiwa na majeraha na pia kusababisha maafa.

Simulizi la wengi katika soko la Ahero limeeleza jinsi ambavyo usalama umedorora huku wahalifu wakishiriki kila aina ya uhuni na uporaji.

Clemant Otieno Onyango maarufu kama Karani ni kati ya wale ambao wameathirika, bado akiwa na majeraha baada ya kuvamiwa mjini Ahero.

Mnamo Aprili 3, 2026 Bw Onyango, mhudumu wa bodaboda alikuwa akimsindikiza mkewe kuabiri matatu kuelekea Sondu alipovamiwa nyakati za asubuhi.

Walipokuwa wakisubiri kuabiri gari kwenye mzunguko wa Ahero, vijana wawili walijitokeza na wakamvamia.

“Walitaka niwape simu na nilipokataa, mmoja wao alinikata kwa panga. Naamini nilinusurika kwa sababu mke wangu alipiga nduru na watu wakaja ndipo wahalifu hao wakatoroka,” akasema Bw Onyango.

Kutokana na juhudi za mkewewe alihamishwa hadi Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi ambako alitibiwa.

Imebainika kuwa uvamizi huo huendeshwa sana nyakati za asubuhi ambapo wengi wamesimulia walipokonywa simu na pia biashara zao kuvamiwa kabla ya asubuhi kufika na giza linapoingia.

Wakazi wanasema uvamizi huo unaendeshwa na magenge ya vijana ambao wapo kati ya umri wa miaka 15-26. Vijana hao hujihami kwa visu, panga na silaha nyingine butu.

Kuna kundi maarufu ambalo linafahamika kama ‘Chude Chude’ ambalo linawahangaisha wakazi.

Kundi hilo limehusishwa na kuwapiga na kuwajeruhi wakazi na abiria wanaotumia barabara ya Kisumu-Nairobi ambayo huwa na shughuli nyingi.

Katika kisa kimoja cha kushtusha, mwanachama wa genge hilo ambaye alikuwa ameokolewa na polisi na kupelekwa Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Nyangánde, Jumapili aliondolewa na wakazi wenye hasira na kupigwa hadi kufa nje ya hospitali hiyo.

Wafanyabiashara soko la Ahero pamoja na wahudumu wa bodaboda sasa wanashutumu polisi kwa kutochukua hatua kuwahakikishia usalama wao.

Wengi wanaeleza kuwa utovu wa usalama umechangia wao kuzifunga biashara zao mapema wakihofia kuporwa.

Pia sasa kuna uhasama mkuu kati ya wahudumu wa bodaboda na genge la Chude Chude huku pande zote zikilipiza kisasi kwa mauaji yanayotokea.

Jumapili iliyopita, mhudumu wa bodaboda aliuawa kwenye kisa ambacho kinaaminiwa kuwa ni cha kulipiza kisasi.

Pia kuna madai kuwa genge hilo linadhaminiwa na mtu mmoja ambaye ni mshirika wa mwanasiasa wa ngazi ya juu nchini.

Mnamo Jumanne Naibu Kamishina wa Nyando Elijah Maranga aliandaa mkutano wa kiusalama ambao pia ulihudhuriwa na Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Ahero Isaiah Mose na maafisa wengine.

“Tumekuwa tukiwakamata na kuwafikisha kortini lakini raia hawataki kutoa ushahidi kwa sababu wanasema watavamiwa. Pia tunaangalia kanda ya CCTV kwa sababu uvamizi mmoja uliotokea katika kituo cha mafuta cha Total,” akasema Bw Maranga.

Afisa huyo alisema kuwa pia wanachunguza kuhusishwa kwa genge hilo na wanasiasa.



from Taifa Leo https://ift.tt/1VkIoPH
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post