Wawili wauawa kwa risasi polisi wakitibua maandamano ya kupinga uchimbaji dhahabu Siaya

WATU wawili Jumatatu, Aprili 6, 2026 walipigwa risasi na kufa Gem-Ramula, Kaunti ya Siaya, wanakijiji walipoandamana kupinga mipango inayonukia ya kuwafurusha kwenye ardhi yao wakipinga shughuli za kampuni ya uchimbaji wa dhahabu ya Shanta.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Polisi wa eneo hilo, Charles Wafula, waliouawa walikuwa kati ya watu ambao walikuwa wamevamia kituo cha polisi baada ya maafisa kuwatawanya wakati wa maandamano hayo.

Bw Wafula alisema waandamanaji hao walikasirika kutokana na kile walichodai walitaka kuhamishwa kiharamu na kampuni hiyo.

Walivamia kituo hicho cha polisi wakati wa maandamano hayo na kulazimisha polisi hao waingilie kati.

“Walikuwa wamepanga maandamano lakini hawakuambia polisi na maafisa wetu walipoingilia kati kutuliza hali walivamiwa pamoja na kituo. Magari na vifaa vingine viliharibiwa,” akasema Bw Wafula.

Waliouawa walithibitishwa kuwa ni Henry Otieno na Jack Omenda ambao walikuwa wakiandamana kupinga kuondolewa kwenye ardhi waliyosema wameishi tangu enzi za mababu wao.

“Wanajamii walikuwa wamekusanyika na kuandaa maandamano dhidi ya Kampuni ya Shanta Gold ambayo inataka kuwahamisha bila idhini yao,” akasema Mkurugenzi Mkuu Chris Owalla wa Vuguvugu la kutetea haki la CIAGK.

Bw Owalla alisema polisi waliwamiminia wakazi risasi bila onyo baada ya mtafaruku kwenye soko la Ramula.

“Wakazi wanasema kulikuwa na majibizano kati ya polisi na wakazi ambapo polisi walimua kuwaua Henry na Jack papo hapo,” akasema Bw Owalla.

Aidha aliwakashifu wakuu wa polisi akiwemo Bw Wafula na Charles Emodo kutoka Idara ya Upelelezi eneo hilo.



from Taifa Leo https://ift.tt/cehJHYO
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post