Kanja aelezea jinsi walivyozima njama za wahuni maandamano ya Juni 25

INSPEKTA Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, amesema kuwa idara za usalama zilikuwa zimepokea taarifa za kijasusi kuhusu mipango ya kusababisha vurugu katika maeneo mbalimbali nchini, hasa katikati mwa jiji la Nairobi (CBD), kabla ya maadhimisho ya mwaka wa pili tangu maandamano ya Gen Z ya Juni 2024. Akizungumza Alhamisi mjini Kitengela akiwa ameandamana na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli pamoja na makamanda wengine wakuu wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), Bw Kanja alisema hatua ya kuweka vizuizi katika barabara kuu zinazoelekea Nairobi, ilichukuliwa baada ya kupata taarifa kwamba makundi ya wahuni yalikuwa yakipanga kupenyeza maandamano ya amani na kuyageuza kuwa vurugu. Alisema maafisa wa usalama walichukua hatua za haraka ili kuzuia hali ambayo ingeweza kuhatarisha maisha ya wananchi na kusababisha uharibifu wa mali. “Idara za usalama zilichukua hatua mapema kwa kuweka vizuizi katika barabara kuu zinazoingia jijini Nairobi ili kuzuia vurugu zilizokuwa zimepangwa. Lengo letu lilikuwa kuhakikisha usalama wa wananchi na kulinda mali,” alisema Bw Kanja. Kwa mujibu wake, maeneo mengi yaliyoshuhudia vurugu katika maandamano ya awali yalibaki tulivu kutokana na hatua zilizowekwa. “Kitengela imekuwa tulivu kama maeneo mengine mengi nchini ambayo hapo awali yalishuhudia vurugu. Hii inaonyesha kuwa wananchi wengi walichagua kudumisha amani,” alisema. Bw Kanja alisisitiza kuwa polisi hawapingi maandamano ya amani yanayoruhusiwa chini ya Katiba, lakini hawatakubali maandamano yanayogeuka fujo, uporaji au uharibifu wa mali. “Wakenya wana haki ya kufanya maandamano ya amani na kuwasilisha malalamishi yao kwa mujibu wa Katiba. Hata hivyo, hatutakubali maandamano ya fujo yanayoweka maisha ya watu na mali zao hatarini. Usalama ni jukumu la kila mmoja wetu,” alisema. Kuhusu watu waliokamatwa kabla ya maandamano hayo, Kanja alisema sheria itafuatwa kikamilifu na kwamba hakuna mtu atakayeadhibiwa bila ushahidi wa kutosha. “Uchunguzi unaendelea na wale waliokamatwa watapewa haki zao zote kisheria. Hakuna mtu atakayelengwa kwa njia isiyo halali, lakini yeyote atakayepatikana na hatia ya kuvunja sheria atafikishwa mahakamani,” alisema. Kutokana na hofu ya vurugu, biashara nyingi mjini Kitengela zilisalia kufungwa kwa muda mrefu jana huku shughuli za kiuchumi zikidorora. Maduka makubwa yalifungwa, magari machache yalionekana kwenye Barabara ya Namanga na shughuli katika vichinjio vya Kitengela zilipungua kwa kiasi kikubwa. Wakazi wengi walisema walichagua kubaki majumbani kutokana na uwepo mkubwa wa polisi na hofu ya machafuko ambayo yaliwahi kushuhudiwa katika maandamano ya awali. Hata hivyo, kufikia alasiri, hali ilikuwa tulivu huku maafisa wa usalama wakendelea kufanya doria katika maeneo mbalimbali ya Kajiado na viunga vya Nairobi.

from Taifa Leo https://ift.tt/u8nfUVt
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post