Manusura wa ukatili wa polisi wadai wahanga wa utekaji wametengwa katika fidia

MANUSURA wa ukatili wa polisi wamelaumu serikali kwa kuwatenga waliotekwa nyara katika mpango wa fidia kwa waathiriwa wa ukiukaji wa haki za binadamu, wakitoa muda wa saa 24 kwa serikali kuchapisha majina ya Wakenya waliotambuliwa kufidiwa au waelekee mahakamani. Kupitia taarifa, Muungano wa Waathiriwa na Manusura wa Ukatili wa Polisi (CVSSV), walidai kuwa mwenyekiti wa kamati ya fidia ya ukiukaji wa haki za binadamu, Profesa Makau Mutua, ametekeleza kwa ubaguzi mapendekezo ya Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (KNCHR) licha ya kutokuwa na mamlaka ya kubadilisha, kupunguza au kusitisha sehemu yoyote ya ripoti hiyo. “Utekaji nyara ni miongoni mwa ukiukaji mbaya zaidi wa haki za binadamu uliofanywa na serikali katika historia ya Kenya. Hata hivyo, hakuna hata kesi moja kati ya visa 35 vya watu waliotekwa nyara na visa 135 vya mateso iliyojumuishwa katika awamu ya kwanza ya fidia,” alisema Jamil Longton. [caption id="attachment_189517" align="alignnone" width="2199"] Vijana wakishiriki maandamano Juni 25, 2026. Picha|Lucy Wanjiru[/caption] Muungano huo ulisema utekelezaji wa mapendekezo kwa ubaguzi umeharibu uaminifu wa mchakato huo na kudhoofisha juhudi za kutafuta haki kwa waathiriwa. Pia ulitaka serikali kuchapisha orodha kamili ya watu waliotambuliwa kufidiwa ili kuimarisha uwazi na kuondoa mashaka kuhusu mchakato huo. “Mapambano ya haki hayawezi kufanikiwa ikiwa serikali itaamua ni akina nani wanastahili kutambuliwa na akina nani wanapaswa kusahaulika. Tutaendelea kusimama na kila mwathiriwa kuhakikisha hakuna atakayesahaulika, kufutwa katika historia au kunyimwa haki,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo. Kundi hilo pia lilitilia shaka tangazo la serikali kuhusu fidia ya Sh348 milioni, likisema ni kampeni ya kujisafisha kisiasa kwa kuwa hakuna mnufaika yeyote aliyejitokeza hadharani kuthibitisha kupokea fedha hizo. Wakili wa waathiriwa hao, Abna Mango, alisema jopo la Profesa Mutua halina mamlaka ya kisheria kubadilisha mfumo uliopendekezwa na KNCHR na kwamba waathiriwa watawasilisha kesi mahakamani chini ya Kifungu cha 47 cha Katiba kuhusu haki ya kupata huduma za haki. “Kuondoa waathiriwa wa utekaji nyara ni kitendo kisicho na msingi kisheria. Kamati hii ilipaswa kuhakikisha waathiriwa wote wanapata fidia, badala ya kuchagua baadhi na kuwaacha wengine,” alisema Mango. Taarifa hiyo ilitolewa kabla ya maadhimisho ya miaka miwili tangu maandamano ya Gen Z ya Juni 25, 2024. Muungano huo ulisema ulikuwa umefahamisha rasmi idara za usalama kuhusu shughuli za kumbukumbu zilizopangwa Nairobi, Mombasa na miji mingine nchini. Jana, baadhi ya wanaharakati waliandamana hadi Bunge kuweka maua kwa heshima ya waliouawa wakati wa maandamano hayo, akiwemo Rex Masai na Eric Shieny. Pia walilaani kile walichokiita vitisho dhidi ya watetezi wa haki za binadamu, wakitaja kukamatwa kwa mwanaharakati Bob Njagi. Mwanaharakati Bernard Kavuli, ambaye alitekwa nyara mwaka 2024, alisema kuwa kuwakumbuka waathiriwa si uhalifu bali ni haki ya kikatiba.

from Taifa Leo https://ift.tt/k6wyEhD
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post