Oburu akejeli Orengo kushiriki maandamano akipuuza kaunti

KIONGOZI wa ODM Dkt Oburu Odinga amemkosoa vikali Gavana wa Siaya James Orengo kwa madai ya kupuuza utoaji wa huduma kwa wananchi huku akijikita zaidi katika siasa za kitaifa na maandamano dhidi ya serikali. Akizungumza akiwa Siaya, Dkt Oburu alisema Orengo anapaswa kuelekeza nguvu zake katika kutatua changamoto zinazowakabili wakazi wa kaunti hiyo badala ya kutumia muda mwingi katika kampeni za kisiasa. Kwa mujibu wa seneta huyo wa Siaya, wananchi wanakabiliwa na barabara mbovu, ukosefu wa maji, huduma duni za afya na kucheleweshwa kwa mishahara ya wafanyakazi wa kaunti, hali ambayo imesababisha migomo ya mara kwa mara. 'Ningependa kumsihi gavana wangu Bw Orengo aache kupiga kelele bila matokeo huku wananchi wakiteseka bila barabara nzuri, maji safi, huduma bora za afya na hata mishahara kwa wauguzi na wafanyakazi wengine,' alisema Dkt Oburu. Alimtaka gavana huyo kushirikiana kwa karibu na serikali ya kitaifa akisema Katiba inahimiza ushirikiano kati ya serikali kuu na zile za kaunti ili kuharakisha maendeleo. 'Keti ofisini ufanye kazi kwa ajili ya wananchi. Dumisha uhusiano mzuri na serikali ya kitaifa ili upate miradi na rasilimali zaidi kwa manufaa ya watu wa Siaya,' aliongeza. Kauli za Dkt Oburu zinajiri wakati Orengo amejitokeza kuwa mmoja wa viongozi wakuu wa vuguvugu la Linda Mwananchi. Katika miezi ya hivi karibuni ameshiriki maandamano dhidi ya serikali, kuwatetea waandamanaji mahakamani na kusisitiza uwajibikaji serikalini. Mnamo Ijumaa alikuwa miongoni mwa mawakili waliofanikisha kuachiliwa kwa zaidi ya vijana 200 waliokamatwa wakati wa maandamano ya kumbukumbu ya Juni 26 yaliyoandaliwa na wanaharakati wa Gen Z na mashirika ya kijamii. Dkt Oburu pia alipuuza madai kwamba hajawahi kushiriki katika mapambano ya demokrasia nchini, akisema amekumbana na mateso ya kisiasa na hata kuonja gesi ya kutoa machozi mara nyingi. 'Msiseme sijawahi kuteseka. Nimevuta gesi ya kutoa machozi mara nyingi tangu nilipoingia siasani,' alisema. Aidha, aliwapongeza wanachama wa ODM kwa kutoshiriki maandamano ya Gen Z ya Alhamisi, akisema walionyesha nidhamu na kutii chama. Kuhusu uchaguzi mkuu wa 2027, Dkt Oburu alisema ODM haina haraka ya kuingia katika mazungumzo ya miungano ya kisiasa kwani bado kuna muda wa kutosha kabla ya muda wa kisheria kuisha. Aliongeza kuwa chama kinaandaa mikakati yake kwa utulivu na kina imani kuwa kitakamilisha mazungumzo ya miungano kabla ya mwisho wa mwaka huku akitabiri kuwa kutakuwa na mabadiliko makubwa ya kisiasa kabla ya uchaguzi ujao.

from Taifa Leo https://ift.tt/xTrNkg0
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post