
RAIS William Ruto ameweka mkazo kwenye miradi ya nyumba za bei nafuu, utoshelevu wa chakula na miradi ya maendeleo ya jamii tofauti na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta, ambaye alijijengea urithi kupitia uwekezaji mkubwa katika barabara, reli, kawi na sekta ya afya.
Kufikia mwisho wa muhula wake wa kwanza mwaka ujao, serikali ya Rais Ruto inatarajiwa kuwa imetumia takriban Sh1.2 trilioni katika ujenzi wa barabara, mpango wa nyumba za bei nafuu, ruzuku ya mbegu na mbolea pamoja na miradi inayofadhiliwa kupitia Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF).
Fedha hizo ni karibu asilimia 47 ya Sh2.8 trilioni ambazo serikali yake itakuwa imewekeza katika miradi ya maendeleo tangu ilipoingia madarakani mwaka 2022. Hii inaonyesha kuwa karibu nusu ya fedha zote za maendeleo zimeelekezwa kwenye sekta hizo nne.
Ingawa serikali ya Ruto imeendelea kuwekeza katika barabara kama ilivyokuwa chini ya Uhuru, kiwango cha matumizi kimepungua. Serikali ya Uhuru ilitumia zaidi ya Sh862 bilioni kujenga, kukarabati na kutunza barabara kati ya mwaka 2017 na 2022, huku wastani wa matumizi ukiwa Sh172 bilioni kwa mwaka.
Kwa upande wa Rais Ruto, matumizi ya barabara yanatarajiwa kufikia Sh590 bilioni kufikia Juni 2027, kiasi ambacho ni takriban Sh271 bilioni chini ya alichotumia mtangulizi wake katika kipindi kama hicho.
Hata hivyo, tofauti kubwa imejitokeza katika sekta ya makazi. Serikali ya sasa imetilia mkazo mpango wa nyumba za bei nafuu na inatarajiwa kuwa imetumia karibu Sh220 bilioni kufikia mwisho wa muhula wa kwanza wa Rais Ruto.
Akizungumza baada ya kutia saini Mswada wa Fedha wa mwaka 2026, Rais alisema mpango huo unasalia kuwa nguzo muhimu ya mageuzi ya uchumi.
Alisema zaidi ya nyumba 274,000 zinaendelea kujengwa huku mpango huo ukiwa umechangia kuunda ajira zaidi ya 640,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Serikali pia imeongeza bajeti ya sekta ya makazi kutoka Sh64.2 bilioni katika miaka mitatu ya mwisho ya utawala wa Uhuru hadi zaidi ya Sh102 bilioni katika miaka mitatu ya kwanza ya utawala wa Ruto. Bajeti hiyo inatarajiwa kufikia Sh138 bilioni katika mwaka wa fedha unaoanza Julai 1.
Eneo jingine ambalo Rais Ruto ameweka msisitizo ni miradi ya maendeleo inayotekelezwa kupitia NG-CDF. Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa madarasa, maabara, vituo vya polisi, v vibanda vya waendesha bodaboda na miundombinu mingine ya kijamii.
Kufikia Juni mwaka ujao, zaidi ya Sh278 bilioni zitakuwa zimetumika katika miradi hiyo, na kuifanya kuwa sekta ya pili yenye matumizi makubwa baada ya barabara.
Katika sekta ya kilimo, serikali imeelekeza fedha nyingi kwenye ruzuku ya mbolea na mbegu kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chakula na kupunguza gharama kwa wakulima.
Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, zaidi ya tani milioni 1.1 za mbolea zimesambazwa kwa wakulima milioni 3.16 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Rais amesema serikali imetenga Sh20 bilioni kwa ruzuku ya mbegu na mbolea, ikilinganishwa na kutokuwepo kwa fedha hizo mwaka 2022. Zaidi ya wakulima milioni 6.5 sasa wananufaika na mpango huo.
Kwa ujumla, serikali ya Ruto inatarajiwa kuwa imetumia zaidi ya Sh103 bilioni katika mipango ya kuhakikisha taifa linajitosheleza kwa chakula kufikia mwisho wa muhula wake wa kwanza.
Kwa upande mwingine, urithi wa Rais Uhuru Kenyatta ulijengwa zaidi katika miradi mikubwa ya miundombinu. Mbali na kutumia fedha nyingi kujenga barabara, serikali yake iliwekeza Sh354 bilioni katika reli, ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kati ya Mombasa, Nairobi na Naivasha.
Aidha, serikali ya Uhuru ilitumia takriban Sh220 bilioni kupanua huduma za umeme kupitia mpango wa Last Mile Connectivity.
Huku muhula wa kwanza wa Rais Ruto ukielekea mwisho, inaonekana ameendelea na sera ya kuwekeza kwenye barabara, lakini amechagua kujenga urithi wake kupitia nyumba za bei nafuu, usalama wa chakula na miradi ya maendeleo ya jamii badala ya reli na kawi ambazo zilikuwa alama kuu za utawala wa Uhuru Kenyatta.
from Taifa Leo https://ift.tt/9ocW1pA
via IFTTT