
BAADHI ya viongozi wa ODM jijini Nairobi wamekataa wazo la kugawana nyadhifa za kisiasa na UDA kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, wakisisitiza kuwa ODM ndiyo inafaa kutoa mgombeaji wa ugavana wa Nairobi.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa ODM Nairobi ambaye pia ni Mbunge wa Makadara, George Aladwa, viongozi hao walisema chama hicho kimekubaliana kumuunga mkono Rais William Ruto na Naibu wake Profesa Kithure Kindiki katika azma yao ya kutetea viti vyao mnamo 2027.
Kwa hivyo ODM inastahili kupewa nafasi ya kuwania ugavana wa Nairobi na iungwe mkono na wanasiasa wa vyama vingine tanzu ndani ya Kenya Kwanza.
“Kiti cha ugavana wa Nairobi lazima kibaki ODM na hakuna njia ya mkato kuhusu hilo. Tumesema tutamuunga mkono Rais Ruto na Naibu wake katika uchaguzi ujao. Hatutaki siasa za ugavi wa nyadhifa katika ngome za ODM,” alisema Bw Aladwa.
Mbunge huyo pia alitangaza rasmi nia yake ya kuwania ugavana wa Nairobi.
“Nimeijenga na kuihudumia ODM kwa miaka mingi pamoja na marehemu Raila Odinga. Wale wanaopanga kujiunga na chama wawe tayari kwa mchujo. Madiwani na wajumbe wengi wako nyuma yangu, na mchujo utakuwa wa haki na uwazi,” akaongeza.
Bw Aladwa pia alimtetea Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, akimtuhumu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kuwashambulia viongozi ambao anajua hawatajibu matamshi yake hadharani.
“Kanja alipitia taratibu zote za kuajiriwa na akathibitishwa kisheria. Gachagua aache kusambaza propaganda na amruhusu afanye kazi yake bila kuingiliwa,” alisema.
Viongozi hao walimtaka Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen kuchukua hatua dhidi ya Bw Gachagua wakidai matamshi yake yanayolenga jamii fulani yanaweza kuchochea mvutano wa kisiasa.
“Akihitaji kutofautiana na Rais afanye hivyo bila kuwahusisha wananchi wengine. Anapaswa kuheshimu Rais ambaye alichaguliwa na Wakenya,” akasema.
Aidha, walimtetea Waziri wa Afya Aden Duale, wakisema kauli tata anazodaiwa kutoa zilifasiriwa vibaya na baadhi ya viongozi kwa ajili ya maslahi ya kisiasa.
“Hakuna jamii iliyo bora kuliko nyingine nchini Kenya. Wanaomshambulia Duale wanapaswa kwanza kumkosoa Gachagua kwa matamshi yake,” akasema Bw Aladwa.
Bw Aladwa ndiye mgombeaji pekee wa ODM kutoka mrengo unaoongozwa na Dkt Oburu Oginga ambaye ametangaza analenga ugavana wa Nairobi.
Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino pia anataka ugavana ila kuna uwezekano finyu atatumia ODM kwa sababu anaegemea mrengo wa Linda Mwananchi.
from Taifa Leo https://ift.tt/0VjB7fX
via
IFTTT