Ruto amwaga miradi ya mamilioni Magharibi, Oparanya akipigiwa debe 2027

RAIS William Ruto jana alisema serikali yake itaendelea kutekeleza miradi ya mabilioni ya pesa Magharibi mwa nchi huku wabunge wanaounga serikali yake wakiahidi kuwa eneo hilo litaendelea kuunga serikali katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Kiongozi wa nchi jana alikuwa katika Kaunti ya Busia ambapo alipigia debe miradi ambayo serikali yake imetekeleza na inaendelea kutekeleza kuinua eneo hilo kimaendeleo.
Kwa upande mwingine, Kiongozi wa Wachache katika Bunge, Junet Mohamed, Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya na wabunge wa ODM na UDA nao walishiriki mchango eneobunge la Malava ambapo walipuuza umaarufu wa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.
Huku Rais akiwa Busia, kundi la wabunge wa chama cha ODM likiwa Magharibi nalo lilisema kuwa Bw Oparanya ndiye atakuwa mgombeaji mwenza wa Rais 2027.
“Watu wakuje polepole na wajue huwezi kuruka laini na wajue kuna watu walikaa na Raila miaka na mikaka. Oparanya ndiye anatosha kutuongoza hapa Magharibi kama kiongozi wa ODM baada ya Oburu Oginga. UDA wakipata rais, sisi ODM lazima tupate naibu rais na huyo ni Oparanya,” akasema Bw Mohamed.
“Hii pesa yote ambayo inataka kugawanya ODM ni pesa ya Uhuru Kenyatta na ndiyo anatumia kugawa chama chetu lakini hatafaulu. Kama Uhuru alishindwa kufanya baba kuwa rais 2022 sasa ndiye atasaidia mtu yeyote, sisi hatuwezi kuelekea barabara hiyo,” akaongeza mbunge huyo wa Suna Mashariki.
Mbunge huyo alisisitiza kuwa ODM haitarejelea siasa za maasi na nguvu zao zote sasa ni kuhakikisha kuwa chama kitaendelea kuwa imara. Bw Oparanya alisema amekuwa na uzoefu wa siasa na hatikiswi na wimbi la Bw Sifuna huku akisema kuwa hawezi kusaliti ndoto ya marehemu Raila Odinga.
“Mimi mpaka watu wamekuja kuniambia nitengeneze chama kipya lakini nikakataa. Hakuna kiongozi ambaye alikuwa na ufuasi kuliko Raila na wakati huu kama Magharibi tunaingia moja kwa moja kwa serikali ya Rais Ruto,” akasema Bw Oparanya.
Rais Ruto alisema eneo la Magharibi ni sehemu ya nchi wala haliwezi kuachwa nyuma huku maeneo mengine yakiendelea kupiga hatua kimaendeleo. Alitaja baadhi ya miradi ambayo serikali yake imetekeleza huku akijizuia kuzungumzia suala la umaarufu wa Sifuna.
“Tulianzisha barabara ya Mundere kule Seo Port, Matayos na Funyula. Mliniuliza barabara kutoka Butula-Nambale-Amukura-Kocholia, na mwezi ujao nitakuja hapa kuanzisha barabara hiyo ya kilomita 58 kwa sababu nimepata mwanakandarasi,” akasema Rais. Alikuwa akihutubu wakati wa kutawazwa kwa Askofu wa nne wa Kanisa la ACK Vitalis Job Ekuru, hafla ambayo pia ilihudhuriwa na Makamu wa Rais wa Uganda Jesca Alupe.
 “Tuna reli kutoka Narok na tumesema itakuja ifike hapa Malaba ili kurahisisha usafiri. Mimi na Rais wa Uganda Yoweri Museveni tulikubaliana huu ni mradi ambao tufanya pamoja kurahisisha usafiri na kusaidia nchi zetu kuimarisha uchumi,” akaongeza Rais Ruto
“Kuna barabara itakayofika hapa Malaba kutoka Mau Summit. Nitakuja kuzindua barabara ya Malava-Kimaeti-Bungoma. Barabara nyingine ambazo ziko hapa Busia ambazo ni kilomita 225 zimetengewa Sh5 bilioni na serikali,” akasema Rais Ruto. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Gavana Paul Otuoma, mwenzake wa Kakamega Fernandes Barasa na Kenneth Lusaka wa Bungoma miongoni mwa wabunge wengine kutoka Magharibi mwa Nchi.
“Tumeweka Sh1.2 bilioni za kuongezea miradi ya stima hapa Busia. Nilikuja kuzindua soko Amagoro na tunaendelea kuwajengea masoko mengine 19 mapya kwa sababu tunataka wafanyabiashara wetu waendelee kufanya biashara mahali safi na kuna umeme,” akasema
“Tumetoa Sh3.6 bilioni kuwajenga wanafunzi nyumba kupitia mradi wa nyumba ili wasome mahali ambao kuna usafi na panatoshana,”
“Nimeona wengine wananiambia eti niondoke kwa serikali niunge mtu mwengine mkono (Sifuna) eti ataunda serikali nisiyoijua. Hao viongozi hawajui wanaenda wapi na wao watuheshimu badala ya kututusi ndipo tuwaunge mkono kwa lazima,” akaongeza Bw Oparanya.


from Taifa Leo https://ift.tt/Jn12IpZ
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post