
Miaka 20 baada ya kuzua gumzo nchini Kenya kwa kuhusishwa na uvamizi wa kampuni ya habari ya Standard Group mwaka 2006, mmoja wa mamluki waliokuwa wakijulikana kama “Artur Brothers” sasa anawania uongozi wa juu nchini Armenia.
Artak Sargasyan, ambaye hapo awali alitumia jina la Artur Sargsyan nchini Kenya, ni miongoni mwa wanaowania wadhifa wa Waziri Mkuu kufuatia uchaguzi wa bunge unaotarajiwa kufanyika leo nchini Armenia.
Sargasyan amejipata tena katika vichwa vya habari baada ya kufanya mahojiano kwa vyombo vya habari vya Armenia akisimulia kwa mara ya kwanza jinsi alivyoingia Kenya na kupata ushawishi mkubwa wakati wa utawala wa Rais Mwai Kibaki.
Alikiri kuwa majina ya “Artur Margaryan” na “Artur Sargasyan” yalikuwa bandia yaliyotumiwa kuficha wasitambuliwe walipokuwa nchini Kenya.
Ndugu hao walizua utata mkubwa mwaka 2006 walipohusishwa na uvamizi wa Standard Group, ambapo maafisa wenye silaha walivamia ofisi na mashine za uchapishaji za kampuni hiyo. Wanasiasa wa upinzani wakiongozwa na Raila Odinga waliwataja kama mamluki waliokuwa na uhusiano wa karibu na maafisa wa serikali.
Katika mahojiano hayo, Sargasyan alidai kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Winnie Wangui, ambaye wakati huo alihusishwa na familia ya Rais Kibaki. Alisema walikutana nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kabla ya kuhamia Kenya kwa shughuli za biashara.
Pia alidai kuwa alipata cheo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi baada ya kushiriki katika operesheni za usalama zilizolenga kumlinda Rais Kibaki, madai ambayo hayajawahi kuthibitishwa rasmi.
Ripoti za bunge la Kenya zilizochapishwa mwaka 2007 zilihitimisha kuwa ndugu hao walikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na watu wenye ushawishi mkubwa serikalini na walifurahia ulinzi wa ngazi za juu za mamlaka.
Baada ya kufukuzwa Kenya mwaka 2006, ndugu hao walitoweka kwenye macho ya umma kwa miaka mingi kabla ya kurejea Armenia na kuingia katika siasa.
Sasa Sargasyan anajitambulisha kama mwanasiasa mwenye uzoefu wa kimataifa na anaahidi kuigeuza Armenia kuwa “Singapore ya eneo la Caucasus”. Hata hivyo, kivuli cha sakata la Artur Brothers nchini Kenya kinaendelea kumfuata huku akisaka wadhifa wa juu kisiasa nchini humo.
from Taifa Leo https://ift.tt/XrNAWLJ
via
IFTTT