
DODOMA, Tanzania:
JOTO kubwa la kisiasa linaendelea kutikisa Tanzania, maandamano ya Julai 7 yakikaribia huku viongozi wa serikali wakionya wanaoratibu tukio hilo kuwa watachukuliwa hatua kwa kueneza uchochezi.
Viongozi wa serikali wametoa onyo kwa wanaopanga kutumia maandamano hayo kuwashambulia maafisa wa usalama, kuchoma mali na kuahidi kutumia nguvu za kila aina kuhakikisha taifa hilo halisambaratishwi na uhalifu.
Wito wa kufanyika kwa maandamano hayo umeshamiri katika mitandao ya kijamii huku waratibu wakidai uwajibikaji kuhusu ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu, kuachiliwa huru kwa wafungwa wa kisiasa hasa kiongozi wa upinzani Tundu Lissu na kufanyika kwa mageuzi makubwa ya kisiasa na uongozi.
Uamuzi wa kuyafanya maandamano hayo Julai 7, inayojulikana kama Siku ya Saba Saba, una uzito mkubwa wa kihistoria.
Siku hiyo ya kitaifa huadhimishwa kutokana na kuanzishwa kwa TANU mnamo 1954. Chama hicho kiliongoza mchakato wa kuhakikisha Tanganyika inapata uhuru wake.
Akizungumza jijini Dodoma mnamo Juni 22, Waziri wa Masuala ya Ndani, Patrobas Katambi, alitoa onyo kali kwa wanaotumia majukwaa ya kisiasa kuchochea chuki na vurugu siku ya maandamano hayo.
"Kuna watu si mitandaoni tu bali pia kwenye majukwaa ya kisiasa na katika maeneo mbalimbali, ambao wanajigamba na kujitangaza, wakitoa kauli za uchochezi na ubaguzi dhidi ya Tanzania," akasema Katambi.
Aliwataka wananchi kupuuza watu wanaoeneza chuki, kuwachochea na kuwahamasisha kushiriki uhalifu huku akisema vitendo hivyo vitadhuru nchi kisiasa na kiuchumi.
Polisi nao walituma taarifa mnamo Juni 20, mkuu wa idara hiyo David Misime akisema wanaopanga maandamano hayo sasa wana nia ya kushiriki uhalifu na fujo.
"Miongoni mwa vitendo hivyo ni kuhamasisha watu kufunga barabara, kuchoma shule, kuwashambulia raia, kuwakata watu vichwa na kuwaua baadhi yao, pamoja na kuharibu mali za umma na za watu binafsi," akasema Misime.
Alisisitiza kuwa hakuna haki inayowapa raia ruhusa ya kuandamana iwapo wana nia ya kushiriki fujo, akisema polisi nao wako ange kukabiliana na hali yoyote itakayozuka.
Raia wengi wa Tanzania bado wanaonekana kutoridhishwa na jinsi uchaguzi wa Oktoba 2025 ulivyoendeshwa.
Rais Samia Suluhu alitangazwa mshindi kwa asilimia 98 ya kura lakini waangalizi na mashirika ya kimataifa yalisema uchaguzi huo haukuwa huru.
Ghasia zilizuka baada ya kura hiyo tata.
Tume ya Uchunguzi iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman ilitoa ripoti iliyosema vifo 518 vilishuhudiwa katika mikoa 11.
Ingawa hivyo, ripoti hiyo haikuweka wazi maafisa wa usalama na serikali ambao wanastahili kuwajibishwa kutokana na mauaji hayo.
from Taifa Leo https://ift.tt/tGEcgvb
via IFTTT