Ushuru mpya hautafinya pato la wakulima, Waziri Kagwe asisitiza

WAZIRI wa Kilimo Mutahi Kagwe amehakikishia wakulima wa majanichai kuwa ushuru mpya wa mauzo ya bidhaa hiyo nje ya nchi hautapunguza mapato yao.

Bw Kagwe alisema ushuru huo unanuia kuimarisha ushindani wa chai ya Kenya katika soko la kimataifa.

Katika maelezo kuhusu ushuru mpya wa asilimia 0.8 uliowekwa na Bodi ya Majanichai Kenya (TBK) kwa chai inayouzwa nje, Bw Kagwe alisema matozo hayo hayataathiri fedha ambazo wakulima hupata kwa kila kilo ya majanichai mabichi.

Alieleza kwamba ushuru huo utalipwa na wauzaji wa majanichai nje ya nchi wala si wakulima.

“Bei ya majanichai mabichi kwa wakulima huamuliwa na mapato ya viwanda. Asilimia 50 ya fedha zitakazokusanywa hupitia hazina ya mauzo ya majanichai na zitatumika moja kwa moja kulinda na kuboresha mapato ya wakulima,” akasema.

Kwa mujibu wa waziri wauzaji hao watalipa ushuru wa asilimia 0.8 ya thamani ya majanichai inayouzwa kupitia mnada au moja kwa moja.

Nao watakaoagizaji majanichai kutoka nje ya nchi watalipia ushuru wa asilimia 100 ya thamani ya kila mzigo wa majanichai iliyosindikwa.

“Asilimia 100 inayotozwa waagizaji imewekwa ili kuwalinda wakulima wetu wa majanichai,” alieleza.

Wakulima wadogo, vyama vya ushirika, viwanda vya majanichai, wauzaji wa rejareja wa ndani, wauzaji wa jumla na watumiaji wa ndani hawatalipa ushuru huo kwani unatozwa tu katika hatua ya kuuza majanichai nje au kuiagiza kutoka nje.

Ushuru huo unatarajiwa kuzoa Sh1.38 bilioni kwa mwaka kutokana na mauzo ya nje na Sh40 milioni kwa chai itakayoingizwa nchini. Kwa mwaka hela hizo zitakuwa Sh1.42 bilioni.

Bw Kagwe alitetea ushuru huo wa asilimia 0.8 akisema ni mdogo kwa kuwa unawakilisha sehemu ndogo sana ya thamani ya mauzo ya majanichai nje ya nchi.

Alifichua kuwa nchi kama Sri Lanka hutoza kiwango cha juu zaidi lakini bado hupata mapato karibu mara mbili zaidi kutokana na mauzo ya majanichai.



from Taifa Leo https://ift.tt/msYXLQJ
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post