
VITA vikali vya kisiasa vya kudhibiti kura za eneo la Mlima Kenya Mashariki vimeibuka huku makundi matano ya kisiasa yakijipanga kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Makundi hayo yanawaunganisha Naibu Rais Kithure Kindiki, kinara wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua, mwanasiasa Fred Matiang’i wa Jubilee, Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru na aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza.
Mlima Kenya Mashariki unajumuisha kaunti ya Meru iliyo na wapiga kura 772,000, Tharaka Nithi 232,000 na Embu 334,000.
Washirika wa Profesa Kindiki sasa wanataka pia Kirinyaga yenye wapiga kura 376,000 ijiunge na muungano huo.
Kwa mujibu wa takwimu za IEBC za 2022, eneo hilo lina takriban wapiga kura milioni 1.7, idadi inayotarajiwa kuongezeka hadi milioni 2.5 kufikia 2027.
Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, amesema mpango huo unalenga kupambana na kutengwa kisiasa kwa eneo hilo na pia kuwapa wakazi wa Mashariki nguvu ya kujadiliana kisiasa bila kutegemea Mlima Kenya Magharibi.
“Kama Gachagua ataonekana kuwa na nguvu zaidi kisiasa, sisi wa Mashariki hatutamfuata. Tutabaki Mashariki chini ya uongozi wa Kindiki,” alisema Ruku.
Mpango huo unaungwa mkono na Gavana wa Embu Cecily Mbarire ambaye pia ni mwenyekiti wa chama tawala cha UDA.
Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wanaonya kuwa mkakati huo unaweza kumdhoofisha Profesa Kindiki kitaifa kwa kumfanya aonekane kama kiongozi wa eneo dogo badala ya mwanasiasa wa kitaifa.
Changamoto kubwa kwa Kindiki ni kwamba viongozi wengine ndani ya serikali jumuishi kutoka Pwani, Magharibi na Nyanza pia wanapigania kuwa mgombea mwenza wa Rais William Ruto mwaka 2027.
Kwa upande mwingine, Gachagua anaonekana kuwa na ushawishi mkubwa katika eneo pana la Mlima Kenya linalojumuisha Kiambu, Murang’a, Nyandarua, Nyeri na Laikipia, maeneo yenye zaidi ya wapiga kura milioni tatu.
Katika Mlima Kenya Mashariki, kundi la Gachagua linategemea Mithika Linturi Meru, Kamau Murango Kirinyaga na Mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji Embu.
Kawira Mwangaza pia ameibuka tena kisiasa baada ya kuondolewa mamlakani mwaka 2024, kupitia chama chake cha Umoja na Maendeleo Party.
Ameungana na kundi la Linda Mwananchi ndani ya ODM linalohusisha Seneta Edwin Sifuna na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino.
Kwa upande wake, Fred Matiang’i amejiunga na aliyekuwa Gavana wa Meru Peter Munya katika kuimarisha ushawishi wake eneo hilo.
Anne Waiguru naye ameonekana kupigana kivyake huku akionyesha nia ya kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto mwaka 2027.
Gachagua amesema mipango hiyo yote inalenga kugawa kura za Mlima Kenya ili eneo hilo lisipige kura kwa pamoja dhidi ya Rais Ruto.
“Hii si vita kati ya Mashariki na Magharibi. Serikali ndiyo inafadhili mgawanyiko huu. Lazima nguvu zote zinazompinga Ruto ziungane nyuma ya mgombea mmoja wa upinzani,” alisema Gachagua akiwa Kajiado wiki iliyopita.
Mchanganuzi wa siasa John Okumu anasema kati ya makundi hayo matano, mawili pekee yanaunga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto.
Anasema viongozi wanaoonekana kuwa na nguvu kubwa zaidi kwa sasa ni Kindiki, Gachagua na Kawira Mwangaza.
“Kindiki ana nafasi kubwa kwa kuwa Naibu Rais lakini anaonekana kuogopa kuunganisha Mlima Kenya kama ngome moja. Gachagua anaonekana kuwa mbele kisiasa huku Mwangaza akijaribu kupanua ushawishi wake nje ya Mashariki,” alisema Okumu.
Mchanganuzi mwingine, Malila Munywoki, amesema vita vya Mlima Kenya Mashariki vinaweza kuwa hatari zaidi kwa Rais Ruto kwa sababu wengi wa viongozi huko wanapinga kuchaguliwa kwake tena.
“Ukichunguza Gachagua, Matiang’i na Mwangaza, wote wanampinga Ruto. Hilo linaonyesha kuwa Rais anaweza kupata wakati mgumu sana 2027, na Kindiki ndiye atakayepata pigo la kwanza,” alisema Munywoki.
from Taifa Leo https://ift.tt/EhXkZmd
via
IFTTT