
UAMUZI unaosubiriwa wa kesi ya kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, umeibuka kuwa kipengele muhimu kinachoweza kuathiri mwelekeo wa siasa hasa kinyang’anyiro cha urais mwaka ujao wa 2027.
Uamuzi huo unaotarajiwa kutolewa Juni 8, kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, una uzito mkubwa kwa mustakabali wa Rais William Ruto kutetea kiti chake, pamoja na nafasi za viongozi wa upinzani akiwemo kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka, na mgombeaji wa urais wa Jubilee, Fred Matiang'i.
Bw Gachagua anatarajiwa kujua hatima yake wakati Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi kuhusu kesi zilizounganishwa za kupinga uhalali wa kuondolewa kwake madarakani Oktoba 2024 kupitia mchakato wa bunge.
Kesi hizo zinapinga uamuzi wa Bunge la Kitaifa na Seneti, walalamishi wakidai mchakato mzima ulikuwa kinyume cha Katiba na haukufuata taratibu zinazofaa.
Katika maombi yake, Bw Gachagua anataka mahakama iamue kuwa aliondolewa madarakani kinyume cha sheria na alipwe fidia ya mshahara na marupurupu ambayo angepata kama angekamilisha muhula wake wa miaka mitano aliochaguliwa mwaka 2022.
Mawakili wake wanasisitiza kuwa mchakato huo ulikiuka haki ya kusikilizwa kwa haki na ulifanywa kwa haraka kupita kiasi bila kufuata ipasavyo ushirikishaji wa umma.
Wachambuzi wa siasa wanasema hukumu hiyo inaweza kuzua mabadiliko mapya ya kisiasa yatakayovuka kesi binafsi ya Bw Gachagua na kugusa moja kwa moja kinyang’anyiro cha urais 2027.
Mchambuzi wa siasa Dismas Mokua, anasema Bw Gachagua tayari amegeuza changamoto yake ya kisiasa kuwa mtaji mkubwa wa ushawishi.
Kwa mujibu wake, Bw Gachagua amejijengea ushawishi mkubwa hasa katika eneo uchaguzi ujao.
“Amefanikiwa kubadilisha changamoto kuwa fursa na sasa ni mhusika muhimu katika siasa za 2027,” alisema Bw Mokua.
Anasema baadhi ya viongozi wa upinzani sasa wanamwona Bw Gachagua kama mtu muhimu wa kuwaunga mkono ili kuongeza nafasi zao dhidi ya Rais Ruto.
Hata hivyo, anaonya kuwa iwapo Bw Gachagua ataruhusiwa kugombea urais, hilo linaweza kumsaidia Rais Ruto kwa kugawanya kura za upinzani.
“Upinzani ukigawanyika na kuwa na wagombea wengi, utampa Ruto ushindi rahisi,” alisema.
Hali hiyo inamweka Bw Musyoka katika wakati mgumu, huku akishikilia azma yake ya kugombea urais baada ya muda mrefu wa kuunga mkono miungano ya upinzani.
Bw Mokua anasema kumtaka Bw Musyoka ajiondoe ili kumuunga mkono Bw Gachagua kunaweza kumgharimu kisiasa.
“Msingi wa Kalonzo utahitaji uongozi mpya ikiwa ataacha azma yake ya 2027,” alisema.
Vivyo hivyo kwa Dkt Matiang’i, ambaye pia ameibuka kama mgombea anayetarajia tiketi ya upinzani.
Wachambuzi wanasema kuna uwezekano mkubwa wa Dkt Matiang’i kusimama kivyake huku akijenga ajenda yake ya kisera kwa wapiga kura.
Wakati huo huo, mchambuzi Herman Manyora, anasema serikali na upinzani wote wanakabiliwa na changamoto kubwa kuelekea 2027.
Kwa upande wa Rais Ruto, Bws Manyora anasema ni lazima akubali changamoto za kiuchumi na kisiasa zinazoathiri wananchi.
“Lazima akubali kwamba mambo si mazuri kwa kila mtu,” alisema.
Aidha anaonya upinzani usitegemee kauli mbiu pekee kama “Wantam” kushinda uchaguzi bila mikakati madhubuti.
Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, ambaye pia anaongoza vuguvugu la Linda Mwananchi, amesema njia pekee ya kumshinda Dkt Ruto ni kuungana kwa upinzani chini ya mgombea mmoja.
“Tumeamua kama Linda Mwananchi kwamba hatutakubali kutumiwa kuruhusu Ruto kupata muhula wa pili. Tunaamini hakuna njia nyingine zaidi ya kuungana chini ya tiketi moja,” alisema Bw Sifuna.
Aliongeza kuwa upinzani lazima usameheane na kuweka tofauti pembeni ili kufanikisha lengo hilo.
Msemaji wa Muungano wa Upinzani, Dkt Mukhisa Kituyi, anasema uchaguzi ujao unapaswa kuwa wa hoja na si wa tamaa za binafsi, akisisitiza kuwa Kenya inahitaji mchakato wa uwazi unaozingatia uwezo na mipango ya kiuchumi kuliko maslahi ya mtu mmoja mmoja.
from Taifa Leo https://ift.tt/D4sUOSf
via IFTTT