Ushahidi wakosa kuonyesha kilichomuua mtoto ndani ya gari kanisani

MAHAKAMA ya Mombasa imehitimisha kuwa hakuna ushahidi wa kutosha katika kesi ya kifo cha Emmanuel Wasike, mtoto wa miaka sita ambaye mwili wake ulipatikana ndani ya gari katika Kanisa la Ushindi Baptist, Likoni, Kaunti ya Mombasa mwaka wa 2018.

Mahakama iliamua kuwa, Emmanuel huenda aliingia mwenyewe ndani ya gari hilo lakini akashindwa kutoka, hali iliyosababisha kifo chake kutokana na joto kali lililomwathiri.

“Mahakama hii imebaini kuwa kifo hiki kilitokana na ajali ya kusikitisha na ya bahati mbaya. Hakuna ushahidi unaoweza kumhusisha mtu yeyote na kosa la uhalifu,” mahakama ilisema katika uamuzi wake.

Ingawa uamuzi huo umehitimisha mchakato wa uchunguzi wa kisheria, umeiacha familia ya marehemu bila majibu ya uhakika kuhusu maswali mengi yanayohusu dakika za mwisho za Emmanuel, ikiwemo jinsi alivyoingia kwenye gari hilo ambalo milango yake haikuwa rahisi kufunguliwa.

“Mahakama inatoa rambirambi kwa familia ya marehemu na ina matumaini kuwa uamuzi huu utawapa angalau faraja na kufunga ukurasa wa tukio hili,” mahakama ilihitimisha.

Mwili wa Emmanuel ulipatikana ndani ya gari aina ya Toyota saloon linalomilikiwa na askofu wa kanisa hilo mnamo Februari 26, 2018.

Gari hilo lilikuwa limeegeshwa ndani ya eneo la Kanisa la Ushindi Baptist katika eneo la Majengo Mapya, Likoni.

Uchunguzi wa mahakama haukuanza hadi Septemba 16, 2019, zaidi ya mwaka mmoja na miezi sita baada ya tukio hilo.

Baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa, mahakama ilisema mashahidi wote walikuwa na maelezo yanayolingana kuhusu matukio muhimu, kwamba mwili wa marehemu ulipatikana kwenye kiti cha nyuma cha gari lililokuwa limeegeshwa ndani ya kanisa na haukuwa na majeraha yoyote ya nje.

“Ushahidi wa kitabibu unaonyesha kuwa kifo kilisababishwa na mazingira ya joto kali yaliyosababisha viungo mbalimbali vya mwili kushindwa kufanya kazi,” mahakama ilieleza.

Mahakama ilisema kuwa ushahidi wote unaunga mkono hitimisho kwamba Emmanuel aliingia mwenyewe ndani ya gari lakini akashindwa kutoka, na hatimaye akafariki kutokana na joto kali lililokuwa ndani ya gari.

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, mama wa marehemu, Bi Joyce Wasike, alieleza kuwa mnamo Februari 25, 2018, majira ya saa nane mchana baada ya ibada kumalizika, aligundua kuwa mwanawe alikuwa ametoweka.

“Baada ya juhudi za kumtafuta kugonga mwamba, nilitoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Likoni na vituo vingine vya karibu. Siku iliyofuata, polisi walinijulisha kuwa mtoto alikuwa amepatikana ndani ya gari la askofu,” aliiambia mahakama.

Alisema alimkuta Emmanuel akiwa amelala kwenye kiti cha nyuma cha gari hilo, ambalo lilikuwa limeegeshwa ndani ya eneo la kanisa huku milango ikiwa imefungwa na madirisha yakiwa yamepandishwa.

“Marehemu hakuwa na majeraha yoyote yanayoonekana. Niliamini alifariki kutokana na kukosa hewa,” alisema mbele ya mahakama mnamo Desemba 6, 2022.

Afisa wa upelelezi, Lenny Nyamai, aliiambia mahakama kuwa taarifa ya mtoto kupotea ilitolewa Februari 25, 2018.

Siku chache baadaye mwili wa Emmanuel ulipatikana ndani ya gari lililokuwa limeegeshwa katika eneo la kanisa.

Alisema pia hakukuwa na majeraha yoyote ya nje kwenye mwili wa mtoto.

Ingawa milango ya gari ilikuwa imefungwa, haikuwa imefungwa kwa ufunguo.

Madirisha yalikuwa na vioo vya giza (tinted), huku mfumo wa CCTV ukiwa haukuwa ukifanya kazi.

Afisa huyo pia aliiambia mahakama kuwa gari hilo liliripotiwa kuwa na hitilafu kwenye mfumo wa kufunga milango na halikuwa likitumika mara kwa mara.

Hata hivyo, kulingana na uchunguzi wake, licha ya hitilafu hiyo, haikuwa rahisi kuingia ndani ya gari hilo kwani hata maafisa wa polisi walipata ugumu kufungua milango yake.

Hali hiyo ilizua maswali kuhusu namna mtoto huyo aliweza kuingia ndani ya gari, jambo ambalo afisa huyo hakuweza kulieleza katika matokeo ya uchunguzi wake.

Askofu Joseph Kitusa Timora alitoa ushahidi mnamo Oktoba 15, 2025, akisema alikuwa Nairobi alipopokea taarifa za tukio hilo.

Alithibitisha kuwa gari hilo lilikuwa lake na lilikuwa limeegeshwa ndani ya eneo la kanisa.

Pia alisema mfumo wa kamera za CCTV wa kanisa haukuwa ukifanya kazi wakati huo.

Daktari Aisha Ali wa Hospitali ya Rufaa ya Coast General alisema ripoti ya uchunguzi wa maiti ilibainisha Emmanuel alifariki kutokana na athari za joto kali kwa viungo vya mwili wake.



from Taifa Leo https://ift.tt/H1hzQGE
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post