
JARIBIO la kukabidhi umiliki wa Shule ya Msingi ya Jamii ya Gatoto iliyoko Mukuru kwa Reuben kwa wamiliki wake wa kibinafsi lilikwama Alhamisi baada ya umati wenye hasira kuwafurusha maafisa na mawakili waliokuwa wamefika kusimamia zoezi hilo.
Miongoni mwa waliolazimika kutoroka kwa magari yao ni kiongozi wa chama cha People's Liberation Party (PLP) Martha Karua na Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) Charles Kanjama.
Bi Karua alikuwa katika eneo hilo kwa takriban dakika mbili pekee kabla ya umati kuanza kumsongea, hali iliyowalazimu maafisa wa polisi waliokuwa wakilinda zoezi hilo kuingilia kati na kumwezesha kuondoka salama.
Waandamanaji walifunga lango la shule wakipaza sauti: "Shule hii ni ya umma na tuna hati miliki."
Aliyekuwa mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya shule hiyo, Felix Mwangangi, alisema walifika mapema asubuhi kwa lengo la kukamilisha zoezi ilivyoagiza mahakama, lakini mazingira yakawa ya uhasama.
"Baadhi ya watu waliokuwa hapo si wazazi. Walisema walilipwa kuhakikisha zoezi hilo halifanikiwi," alisema.
Wamiliki wa shule walilaumu polisi kwa kutowachukulia hatua waliozuia utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama Kuu.
Walisisitiza kuwa wataendelea kupigania warejeshewe usimamizi wa shule hiyo wakisema kuigeuza kuwa ya umma kutadhuru elimu ya watoto wengi kutoka makazi duni.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Makadara (OCPD) Judy Nyongesa alikanusha madai hayo akisema polisi walitekeleza maagizo ya mahakama huku wakiepuka kuzua taharuki mbele ya wanafunzi waliokuwa shuleni.
Alisema shule hiyo ilizinduliwa na Rais William Ruto kama shule ya umma chini ya Wizara ya Elimu na wakazi wengi wanataka iendelee kuwa ya umma.
Mnamo Juni 25, Mahakama Kuu iliamuru shule hiyo isajiliwe tena kama shule ya kibinafsi isiyo ya kutengeneza faida chini ya Sheria ya Elimu ya Msingi na irejeshwe kwa waombaji ifikapo Julai 2.
Jaji Gregory Mutai pia aliamuru OCPD wa Makadara ahakikishe kuna angalau maafisa watatu wa polisi wakati wa shughuli hiyo, huku gharama ya ulinzi ikilipwa na walalamishi.
Wakati huo huo, baadhi ya wazazi wamewasilisha notisi ya kukata rufaa wakisema familia nyingi za Mukuru kwa Reuben haziwezi kumudu karo inayotozwa na shule za kibinafsi, hivyo shule hiyo inapaswa kubaki ya umma.
from Taifa Leo https://ift.tt/wvFzX4y
via IFTTT