
KENYA inaanza mwaka mpya wa kifedha mwezi ujao ikiwa na pengo la zaidi ya Sh1.1 trilioni katika bajeti, hali inayoonyesha pengo kubwa kati ya mapato yanayokusanywa na serikali na kiwango cha matumizi yake.
Hali hiyo inaendelea kuibua wasiwasi kuhusu uwezo wa taifa hili kupunguza mzigo wa madeni na kufadhili miradi ya maendeleo bila kuendelea kukopa.
Kwa mujibu wa makadirio ya Wizara ya Fedha, serikali inapanga kutumia takriban Sh4.82 trilioni katika mwaka wa kifedha wa 2026/2027 huku ikitarajia kukusanya mapato ya Sh3.67 trilioni pekee.
Hii inaacha pengo la zaidi ya Sh1.1 trilioni ambalo litahitaji kufadhiliwa kupitia mikopo ya ndani na nje.
Pengo hilo limeendelea kushuhudiwa licha ya serikali kuahidi mara kwa mara kuimarisha nidhamu ya matumizi ya pesa na kupunguza kutegemea mikopo.
Gharama kubwa za kulipa madeni ya zamani, mishahara ya watumishi wa umma, matumizi ya kawaida ya serikali na utekelezaji wa miradi ya maendeleo zimeendelea kuongeza shinikizo kwa Wizara ya Fedha.
Changamoto nyingine kubwa ni kwamba ukusanyaji wa ushuru umekuwa ukikosa kufikia malengo yaliyowekwa kila mwaka.
Huku mapato yakipungua, matumizi ya serikali yameendelea kuwa makubwa na mara nyingi ni vigumu kuyapunguza kutokana na mahitaji ya huduma za umma na sababu za kisiasa.
Kutokana na hali hiyo, serikali sasa imeelekeza macho yake zaidi katika mikopo ya ndani baada ya mikopo ya nje kuwa ghali zaidi kutokana na ongezeko la viwango vya riba duniani na masharti magumu kutoka kwa wakopeshaji wa kimataifa.
Kwa mujibu wa nyaraka rasmi za bajeti, mwaka ujao wa kifedha utafadhiliwa kupitia mikopo ya nje ya Sh99.5 bilioni na mikopo ya ndani ya zaidi ya Sh1 trilioni.
Hii ni tofauti na miaka iliyopita ambapo serikali ilitegemea zaidi Eurobond, Benki ya Dunia na taasisi nyingine za kimataifa kufadhili matumizi yake.
Wataalamu wa uchumi wanaonya kuwa kukopa fedha nyingi kutoka kwa benki za ndani kunaweza kuathiri sekta ya kibinafsi.
Benki nyingi hupendelea kukopesha serikali kwa kuwa ni mkopaji mwenye hatari ndogo, jambo linalopunguza nafasi ya wafanyabiashara na wawekezaji kupata mikopo kwa ajili ya kuendesha na kupanua biashara zao.
Baada ya maandamano makubwa yaliyoshuhudiwa mwaka wa 2024 kupinga ongezeko la ushuru, Wizara ya Fedha imeamua kutopendekeza kodi mpya nzito katika Mswada wa Fedha wa 2026.
Badala yake, Waziri wa Fedha, John Mbadi amesema serikali italenga kuboresha ukusanyaji wa ushuru na kuongeza idadi ya walipakodi.
Miongoni mwa hatua zinazopendekezwa ni kuimarisha matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa KRA (eTIMS), kuunganisha mifumo ya KRA na jukwaa la eCitizen pamoja na kuongeza ukaguzi katika sekta isiyo rasmi ili kuwatambua walipakodi wapya.
Kwa mujibu wa Mbadi, hatua hizo zinalenga kuongeza mapato ya takriban Sh120 bilioni bila kuongeza mzigo kwa wananchi ambao tayari wamekuwa wakilalamikia gharama kubwa za maisha na viwango vya juu vya ushuru.
Mbali na ushuru, serikali imeanza kutafuta mbinu nyingine za kufadhili miradi ya maendeleo.
Bajeti ya mwaka ujao inalenga kukusanya Sh80 bilioni kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na ya kibinafsi (PPP), hasa katika miradi ya barabara, unyunyizaji na usafiri wa magari ya umeme.
Aidha, serikali inatarajia kuongeza fedha kupitia uuzaji wa sehemu ya hisa zake katika kampuni ya Safaricom na kuelekeza mapato hayo kwenye Hazina ya Miundomsingi iliyoundwa kuvutia uwekezaji wa sekta ya kibinafsi katika miradi mikubwa ya maendeleo.
Wachambuzi wa uchumi wanaamini kuwa mwelekeo huo unaonyesha mabadiliko makubwa katika sera za ufadhili wa maendeleo nchini.
Hata hivyo, wanaonya kuwa mafanikio yake yatategemea uwezo wa serikali kuongeza mapato bila kulemea wananchi, kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima na kuhakikisha mikopo inayochukuliwa inatumika kwa miradi yenye manufaa ya moja kwa moja kwa uchumi na maisha ya Wakenya.
from Taifa Leo https://ift.tt/HGoBPED
via IFTTT