Mwanasayansi Mkenya apewa Sh187 milioni kutafiti AI

MWANASAYANSI wa Kenya Dkt Samuel Oyola amepokea ruzuku ya Sh187 milioni ili kuunda mfumo wa afya ya umma unaotumia akili unde (AI) wenye uwezo wa kutabiri mkurupuko wa magonjwa na kufuatilia vimelea vinavyostahimili dawa.

Vimelea ni viumbe kama virusi, bakteria na fangasi vinavyoweza kusababisha maambukizi mwilini.

Dkt Oyola, ambaye ni Mkuu wa Sayansi ya Jenomu katika Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI), alipokea ruzuku hiyo ya dola za Marekani milioni 1.45 (Sh187 milioni) kutoka Wakfu wa Gates.

Atafanya kazi kwa kushirikiana na wanafunzi wawili wa shahada ya uzamifu (PhD), ambao watatumia teknolojia ya akili unde kuchanganua taarifa zitakazokusanywa.

Watafiti hao watakusanya sampuli za maji taka kutoka maeneo 30, yakiwemo 18 jijini Kisumu na 12 jijini Mombasa, ikiwa ni sehemu ya utafiti ulioanza wakati wa janga la corona.

Miji hiyo miwili ilichaguliwa kwa sababu Nairobi tayari ilikuwa na mradi kama huo wa ufuatiliaji wa maji taka, huku Kisumu na Mombasa zikiwa na mifumo mingine mikubwa ya majitaka iliyoimarishwa nchini.

Dkt Oyola alisema jana kuwa wakati wa janga la corona waligundua kuwa inawezekana kubaini baadhi ya vimelea kupitia maji taka.



from Taifa Leo https://ift.tt/awqgReF
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post