
Waziri wa Ardhi Kaunti ya Kajiado, Hamilton Parseina, pamoja na afisa wa cheo cha chini katika idara hiyo wanakabili na hatari ya kifungo cha miezi sita jela au faini ya Sh200,000 kila mmoja kwa madai ya kukaidi amri ya mahakama kuhusu jaribio tata la kugawa kituo cha biashara cha Oloyiakalani katika Kaunti Ndogo ya Kajiado Magharibi.
Mzozo huo umeibua vita vikali vya kisheria kati ya wakazi na Serikali ya Kaunti ya Kajiado, huku wakazi wakidai maafisa wa kaunti walilenga kinyume cha sheria eneo hilo la ekari 68 bila kufuata utaratibu unaotakiwa.
Kaunti hiyo ilianza kwa kuwasilisha wazo hilo kupitia zoezi la ushirikishaji wa umma, ambalo lilipingwa na wakazi, hali iliyowasukuma kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Hakimu Kajiado kupitia kesi nambari MCCCMISC/E032/2026 kwa Notisi ya Hoja ya Machi 30, 2026 mbele ya Hakimu Mkuu Roseline Oganyo.
Kupitia kwa wakili Enock Nyongesa, walalamishi Ronald Kiranti, Solomon Kikanae na Obadiah Likam, kwa niaba yao na wakazi wengine, waliomba mahakama izuie washtakiwa, wakiwemo Waziri wa Ardhi wa Kaunti Ardhi Hamilton Parseina, Afisa Mkuu katika Idara ya Ardhi, Idara ya Mipango na Maendeleo ya Miji, Serikali ya Kaunti ya Kajiado pamoja na Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC), kuendelea na zoezi hilo hadi kesi itakaposikizwa na kuamuliwa.
Walalamishi walieleza mahakama kuwa tarehe zilizotajwa katika notisi zilikuwa tayari zimepita kwani zoezi hilo lilikuwa limepangwa kufanyika Jumanne, Machi 17, 2026.
Walidai kuwa Serikali ya Kaunti au mamlaka husika ilipaswa kuandaa notisi mpya inayotoa muda wa kisheria wa siku 21 kabla ya kuanza kwa zoezi hilo.
Aidha, waliambia mahakama kuwa notisi iliyotolewa haikukidhi masharti ya kikatiba kuhusu ushirikishaji wa umma, ambayo yanataka matangazo hayo kuchapishwa katika magazeti yenye usambazaji mkubwa.
Waliongeza kuwa ardhi inayozungumziwa ni ardhi ya umma inayosimamiwa na Tume ya Kitaifa ya Ardhi na haijawahi kutengwa wala kupangwa na iliyokuwa Halmashauri ya Kaunti ya Olkejuado.
Kwa hivyo, walisema jukumu la kusimamia ardhi ya umma kwa niaba ya serikali za kaunti na kitaifa ni la Tume ya Kitaifa ya Ardhi wala si Ofisi ya Afisa Mkuu.
Kupitia kwa hati ya kiapo, walalamishi pia walidai kuwa jamii haikuwahi kuomba upangaji wa mji huo kupitia mkutano wa umma wala ombi la maandishi.
Waliitaka Serikali ya Kaunti kuahirisha zoezi hilo ili jamii ipate muda wa kutosha kujadili huduma za umma zinazopaswa kuhifadhiwa kwenye ardhi hiyo.
Wakazi hao pia walidai kuwa ardhi hiyo inapakana na mashamba binafsi na kwamba migogoro ya mipaka inapaswa kwanza kushughulikiwa na Msajili wa Ardhi kabla ya mchakato wowote wa upangaji kuanza ili kuepuka matatizo ya kisheria na uvamizi wa mashamba ya watu binafsi.
Aidha, walieleza kuwa maeneo hayo kwa sasa hayana maendeleo yoyote yanayohitaji upangaji wa haraka na kwamba mchakato wowote unapaswa kufanywa kwa utaratibu unaofaa na kwa mashauriano na Tume ya Kitaifa ya Ardhi pamoja na jamii ya eneo hilo.
Mnamo Machi 30, 2026, mahakama ilitoa amri ya muda kuwazuia washtakiwa, maajenti wao au wawakilishi wao kuendesha au kuendelea na zoezi lolote la ushirikishaji wa umma, upangaji, ugawaji au utoaji wa ardhi katika Kituo cha Biashara cha Oloyiakalani hadi kesi hiyo isikizwe na kuamuliwa.
Kesi hiyo itatajwa tena Mei 26, 2026 mbele ya Hakimu Mkuu Roseline Oganyo.
“Fahamuni kwamba kutotii au kutofuata amri hii ya mahakama kutasababisha hatua za kisheria dhidi yenu na mtu mwingine yeyote atakayekaidi amri hiyo,” ilisema sehemu ya amri ya mahakama.
Hata hivyo, wakili wa walalamishi alidai kuwa maahenti wa washtakiwa walionekana mapema wiki hii mjini humo wakijaribu kuendeleza zoezi hilo lililozuiwa, hatua aliyosema ilisababisha taharuki miongoni mwa wakazi na ni dharau kwa mahakama inayoweza kufanya waadhibiwe kisheria.
Mtu anayepatikana na hatia ya kuidharau mahakama anaweza kutozwa faini isiyozidi Sh200,000, kufungwa jela kwa muda usiozidi miezi sita au kupewa adhabu zote mbili.
from Taifa Leo https://ift.tt/g3hO6YU
via IFTTT