Nani atatemwa? Rais kulazimika kufuta mawaziri kadhaa wa kiume ili kuteua wa kike

RAIS William Ruto anakabiliwa na kibarua kigumu cha kisiasa baada ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi kuwa Baraza lake la Mawaziri halikidhi matakwa ya Katiba kwa sababu halijatimiza sheria ya uwakilishi wa theluthi mbili ya kijinsia.

Uamuzi huo unaweza kumlazimu kuwaondoa mawaziri wawili wa kiume, hali ambayo inaweza kuwa na athari kubwa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Kwenye uamuzi wake, Mahakama Kuu iliagiza Rais Ruto aunde upya Baraza la Mawaziri ndani ya siku 120 ili liwe na uwakilishi wa theluthi mbili jinsi ilivyoamrishwa kwenye katiba.

Na sasa, Rais ana kibarua kusawazisha uaminifu kwa washirika wake wa kisiasa na wajibu wa kutii Katiba, maslahi ya muungano wa kisiasa na matarajio ya wananchi.

Wengi wanasubiri kuona mbinu atakayotumia kudumisha uthabiti wa kisiasa huku akitekeleza matakwa ya kisheria.

Baraza la Mawaziri la sasa lina Mawaziri 22, lakini wanawake ni sita pekee.

Itamlazimu Rais kuwaondoa mawaziri wawili wa kiume na kujaza nafasi zao kwa mawaziri wanawake ili kutimiza hitaji la theluthi mbili kisheria.

Iwapo uamuzi huo hautabatilishwa na Mahakama ya Rufaa, Rais Ruto hatakuwa na jingine ila kuyatekeleza mabadiliko hayo.

Ingawa hivyo, uamuzi huo umemwekea mtego wa kisiasa. Wachangunuzi wa kisiasa wanahoji kuwa kuwaondoa mawaziri wawili wa kiume ili kutoa nafasi kwa wa kike kutayumbisha Kenya Kwanza.

Vilevile, kuna mawaziri wanaohudumu ndani ya Serikali Jumuishi baada ya Rais Ruto kuingia kwenye ushirikiano wa kisiasa na ODM miaka miwili iliyopita.

Pia kumewa na suala tata kuhusu nani anapaswa kuchukuliwa kama mwanachama wa Baraza la Mawaziri.

Duru za Ikulu jana ziliarifu kuwa Rais huenda akakata rufaa kuhusu uamuzi huo na pia kusaka ufasiri zaidi wa kisheria
Afisa mmoja Ikulu alisema Baraza la Mawaziri halipaswi kutazamwa kuwa linajumuisha mawaziri wa kiume pekee.

Wanawake sita waliopo katika Baraza la Mawaziri ni Beatrice Askul Moe (Jumuiya ya Afrika Mashariki), Hanna Wendot Cheptumo (Jinsia), Deborah Mulongo Barasa (Mazingira,), Alice Wahome (Ardhi), Rebecca Miano (Utalii na Wanyamapori) na Roselinda Soipan Tuya (Ulinzi).

Mbali na mawaziri hao sita, afisa huyo alisema wanawake wengine wawili ni Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor na Katibu katika Baraza la Mawaziri Mercy Wanjau ambao hushiriki mara kwa mara katika vikao vya Baraza la Mawaziri.

"Hii inaongeza idadi ya wanawake hadi wanane, jambo linalotupa msingi wa kuamini kuwa Baraza la Mawaziri limeundwa kwa mujibu wa sheria," akasema afisa huyo.

"Uamuzi huo unaweza kupingwa katika Mahakama ya Rufaa. Huo ndio mtazamo wangu kwa sababu kuna wanawake wanane muhimu wanaoshiriki shughuli za Baraza la Mawaziri kila siku,

"Kwa kweli, Mwanasheria Mkuu ana jukumu muhimu sana katika Baraza la Mawaziri na yeye ni mwanamke. Kwa hivyo, huwezi kupuuza uanachama wake katika baraza hilo," akasema.

Hoja hiyo inaweza kuwa msingi wa rufaa iwapo serikali itaamua kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu badala ya kuunda upya Baraza la Mawaziri.

Katiba inaeleza kuwa Baraza la Mawaziri linajumuisha Rais, Naibu Rais, Mwanasheria Mkuu na Baraza la Mawaziri.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu si Waziri na hahesabiwi miongoni mwa nafasi 22 za mawaziri. Kwa upande mwingine, Katibu katika Baraza la Mawaziri huhudhuria vikao lakini si mwanachama wa baraza hilo kwa mujibu wa Katiba.

"Iwapo kutakuwa na rufaa, swali ni iwapo ofisi hizo zinaweza kuhesabiwa katika kutimiza kanuni ya theluthi mbili ya jinsia. Hili litakuwa mojawapo ya masuala muhimu ya kisheria yatakayoamua hatua inayofuata," akasema wakili Chris Omore.

Njia nyingine ni kuwabadilisha Mwanasheria Mkuu na Katibu wa Baraza la Mawaziri na mawaziri wawili wa kiume, bila kulazimika kumfuta kazi yeyote.

Njia ya tatu ni kuongeza Baraza la Mawaziri, lakini hilo limewekewa mipaka na Katiba.

Kifungu cha 152 cha Katiba kinaweka idadi ya Mawaziri wa Baraza la Mawaziri kati ya 14 na 22.

Hivyo, Rais hawezi kuongeza wizara mpya ili kuwapa nafasi wanawake zaidi bila kukiuka Katiba.

Hivyo basi, kinachobaki ni uamuzi mgumu wa kutangaza ni mawaziri gani wataondolewa.

Kwa mintaarafu hiyo, Rais atalazimika kuwaondoa baadhi ya mawaziri waliopo madarakani ili kutimiza matakwa ya Katiba wala si maslahi ya kisiasa.



from Taifa Leo https://ift.tt/p0bNhz1
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post