
KARIBU muongo mmoja uliopita, safari ya kuelekea Lamu ilikuwa sawa na kuingia eneo la vita kutokana na mashambulizi ya kigaidi.
Mashambulizi hayo yalitikisa maeneo ya Mpeketoni, Kibaoni, Witu, Hindi, Msitu wa Boni pamoja na miji ya mpakani ya Kiunga na Ishakani kati ya mwaka 2014 na 2022.
Hadi sasa, mataifa ya Magharibi bado hayajaondoa tahadhari za usafiri kwa maeneo hayo, huku Serikali pia ikiendelea kutekeleza amri ya kutotoka nje usiku katika baadhi ya maeneo, huku kukiwa na marufuku ya kusafiri usiku.
Katika mwaka wa 2015, serikali ilianzisha Operesheni Linda Boni, ambayo sasa inajulikana kama Operesheni Amani Boni (OAB), oparesheni ya pamoja ya vyombo vya usalama inayolenga kurejesha utulivu Lamu pamoja na maeneo ya Tana River, Garissa na Kilifi yanayopakana na Msitu wa Boni.
Juhudi hizo, pamoja na uhamasishaji wa jamii dhidi ya itikadi kali na uchochezi, zimeifanya Lamu kubadilika kutoka kitovu cha ugaidi hadi kuwa mfano wa amani unaotambuliwa kimataifa.
Wiki iliyopita, Lamu iliweka historia kwa kuwa mamlaka ya kwanza ya serikali za mitaa barani Afrika kutunukiwa Tuzo ya Amani ya United Cities and Local Governments (UCLG) katika kongamano lililofanyika Tangier, Morocco.
Kaunti hiyo iliibuka mshindi kati ya washiriki zaidi ya 100 duniani, huku ikiwa ni tano pekee zilizofika hatua ya mwisho.
Awali Machi mwaka huu, pia ilitunukiwa tuzo ya ‘Best Community Impact Award’ nchini India kupitia mradi wa Kiunga Solar Desalination, unaosafisha maji ya chumvi kutumika nyumbani.
Mkurugenzi wa Kudumisha Amani Lamu, Bw Shee Kupi, alisema mafanikio hayo hayakutokana na operesheni moja ya usalama bali kuifanya amani kuwa sehemu ya mfumo wa utawala wa kaunti kupitia sera, sheria na mipango ya maendeleo.
“Mbinu za kutoa tahadhari mapema na kushughulikia migogoro kabla haijazidi zilianzishwa. Pia tuliunganisha ujenzi wa amani katika sera, sheria, mipango na bajeti za kaunti ili kuhakikisha unaendelea hata baada ya mabadiliko ya kisiasa," alisema Bw Kupi.
Aliongeza kuwa uwekezaji katika maji, mbinu za riziki, huduma za kijamii na maandalizi ya kukabiliana na majanga ni uwekezaji katika amani kwa sababu hushughulikia chanzo cha migogoro.
Wakazi wamekiri kuwa tuzo hizo ni za haki, kwani hali ya usalama imeimarika kwa kiasi kikubwa.
Mkazi wa Bakanja, Bw Kamau Mbuthia, alisema zamani walilala vichakani kwa hofu ya mashambulizi.
“Leo tunaweza kulala majumbani bila hofu yoyote ya kushambuliwa. Tunashukuru serikali kwa juhudi zake za kuboresha usalama,” alisema.
Mkazi wa Kiunga, Bi Khadija Athman, alisema shule hazifungwi tena kutokana na hofu ya mashambulizi ya Al-Shabaab.
Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Stephen Sangolo, alisema mashambulizi ya kigaidi yamepungua kwa kiwango kikubwa, ingawa alionya kuwa vitisho vya ugaidi, uhalifu wa mipakani na athari za mabadiliko ya tabianchi bado vipo.
Kuimarika kwa usalama pia kumechochea ukuaji wa sekta ya utalii.
Kulingana na Waziri wa Utalii katika Kaunti hiyo, Bi Aisha Miraj, wageni wanaolala hotelini sasa hufikia wastani wa asilimia 55 wakati wa msimu wa chini na huzidi asilimia 90 wakati wa msimu wa juu wa utalii.
Akipokea tuzo hiyo, Gavana Issa Timamy alisema ni ushindi wa wananchi wa Lamu na washirika wote walioshiriki kujenga amani.
from Taifa Leo https://ift.tt/2gOyf3C
via IFTTT