
HUKU viongozi wa upinzani wakiharakisha juhudi za kuunda muungano kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Agosti 10, 2027, changamoto kubwa si tena iwapo wataungana kumpinga Rais William Ruto, bali ni nani atakayepeperusha bendera ya urais.
Mazungumzo yanayoendelea nyuma ya pazia yamegeuka kuwa mvutano wa kisiasa unaohusisha ushawishi wa vyama, nguvu za kikanda, uwezo wa kifedha na matamanio ya kila kiongozi, huku kila mmoja akiamini ana uzito wa kisiasa unaostahili kumfanya awe mgombea mkuu.
Licha ya viongozi wote kukubaliana kuwa tiketi moja ndiyo njia bora ya kumshinda Rais Ruto, wengi hawako tayari kuacha azma ya urais bila kupata hakikisho la nafasi muhimu katika serikali au ndani ya muungano.
Muungano huo, unaojitambulisha kama Muungano wa Serikali Mbadala, unaleta pamoja aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa People's Liberation Party Martha Karua, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i, kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, Justin Muturi, Peter Munya na viongozi wengine.
Hata hivyo, maswali yanayozua mvutano ni mengi.
Nani anafaa kuwa mgombea wa urais? Atachaguliwaje? Je, muungano una uwezo wa kifedha kupambana na rais aliye madarakani?
Na viongozi walio na ndoto za urais wako tayari kuweka kando maslahi yao binafsi kwa manufaa ya umoja?
Baada ya maandamano ya Gen Z ya Juni 25, 2024 na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kuanza kushirikiana kisiasa na Rais Ruto, upinzani ulibadilika na kuzaliwa kwa muungano mpya unaojumuisha hata baadhi ya waliokuwa washirika wa Kenya Kwanza wakiongozwa na Bw Gachagua.
Swali la mgombea wa urais ndilo linalopewa uzito mkubwa.
Kalonzo anaona 2027 kama nafasi yake bora zaidi ya kuwania urais, huku Matiang'i akitajwa kuwa chaguo la wanaotaka kiongozi mwenye rekodi ya mchapa kazi serikalini.
Martha Karua anaendelea kujijenga kama sauti ya mageuzi, huku Gachagua akiwa na ushawishi mkubwa Mlima Kenya.
Wamalwa na Munya nao wanaendelea kutegemewa katika maeneo yao.
Hata hivyo, Karua na Matiang'i wanasisitiza kuwa mgombeaji hafai kuchaguliwa kupitia makubaliano ya viongozi wachache bali kwa mfumo wa wazi unaotegemea utafiti wa kisayansi na ukubwa wa uungwaji mkono.
"Hatupaswi kumchagua mgombea kupitia mazungumzo ya vyumbani. Lazima achaguliwe kwa mchakato wa kisayansi, wazi na unaokubalika na Wakenya wote," amesema Karua.
Matiang'i pia amesema haki na uwazi vinapaswa kutangulia maslahi ya watu binafsi ili mshindi akubalike na washirika wote wa muungano.
Viongozi hao wanaeleza kuwa historia ya siasa za Kenya imeonyesha kuwa migogoro ya uteuzi ndiyo imekuwa ikivunja upinzani.
Mnamo 2002, Simeon Nyachae alikataa kujiunga na Muungano wa NARC uliomwunga mkono Mwai Kibaki. Mnamo 2007, Kalonzo Musyoka alijiondoa ODM kutokana na mzozo wa uongozi na kuwania urais kivyake.
Hata Azimio ilikumbwa na mvutano kuhusu uteuzi wa mgombea mwenza wa Raila Odinga mnamo 2022.
Mchambuzi wa siasa Dismas Mokua asema uhalali wa mchakato wa uteuzi ni muhimu zaidi kuliko jina la mgombeaji.
"Mchakato ndio unaofanya wafuasi wakubali matokeo. Bila uhalali, umoja hauwezi kudumu," anasema.
Wakati huo huo, uamuzi wa Mahakama Kuu uliothibitisha kuondolewa kwa Gachagua madarakani umebadili hesabu za kisiasa.
Awali alikuwa akijichukulia kama msemaji mkuu wa Mlima Kenya kupitia chama chake cha Democracy for the Citizens Party (DCP), lakini sasa wachambuzi wanasema anaweza kujikuta akitengeneza wafalme wa kisiasa badala ya kuwa mgombeaji.
Changamoto nyingine ni iwapo Mlima Kenya utakubali kumuunga mkono mgombea ambaye hatatoka eneo hilo au kusiwe na mgombea mwenza kutoka ukanda huo.
Wachambuzi wanasema hali hiyo inaweza kumfaidi Rais Ruto kisiasa ikiwa atamdumisha Profesa Kithure Kindiki kama mgombea mwenza.
Aidha, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna ameibuka kama sura mpya ya vuguvugu la Linda Mwananchi pamoja na Gavana wa Siaya James Orengo na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino.
Ingawa viongozi wanakanusha kuwepo kwa ushindani kati ya makundi hayo mawili, mawasiliano yanaendelea kuhusu ushirikiano.
Seneta wa Kitui Enoch Wambua amesema makundi yote yana lengo moja la kuhakikisha Rais Ruto anahudumu kwa muhula mmoja pekee.
Mbali na uteuzi wa mgombea urais, fedha za kampeni zimeibuka kama changamoto nyingine kubwa.
Muungano unapanga kutumia michango ya wananchi, teknolojia na uhamasishaji wa kujitolea badala ya kutegemea wafadhili wakubwa.
Karua amesema uchaguzi haupaswi kuamuliwa na wingi wa fedha bali uadilifu na uwezo wa viongozi.
"Uongozi si suala la kuwa na fedha nyingi. Wakenya wanapaswa kuwachagua viongozi kwa uadilifu, uwezo na kujitolea kwao kuhudumia wananchi," amesema.
Matiang'i naye ameonya dhidi ya matumizi ya rasilimali za serikali katika kampeni, akisema yanaharibu ushindani wa kidemokrasia.
Kwa mujibu wa wachambuzi, hata kama muungano huo utafanikiwa kukubaliana kuhusu mgombea na fedha za kampeni, bado utahitaji sera mbadala zinazowapa Wakenya matumaini kuhusu ajira, uchumi, kodi na utawala bora.
Wanasema historia imeonyesha kuwa miungano mingi ya upinzani imevunjika kutokana na tamaa za uongozi.
Safari hii, viongozi wa muungano wanalazimika kwanza kutatua mivutano ya ndani kuhusu uongozi, usawa wa kikanda, fedha na sera kabla ya kuwaomba Wakenya wawape mamlaka ya kuongoza nchi mnamo 2027.
from Taifa Leo https://ift.tt/kUwi80j
via IFTTT