Je, inawezekana Ndindi Nyoro anasubiri matokeo Ol Kalou kuamua ni Wantam au Tutam?

HUKU uchaguzi mkuu wa 2027 ukizidi kukaribia, Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro anakabiliwa na uamuzi mgumu wa kisiasa ambao unaweza kuimarisha hadhi yake kama mwanasiasa wa kitaifa au kudhoofisha uungwaji mkono wake katika eneo la Mlima Kenya na sehemu nyingine za nchi. Nyoro amejikuta katikati ya mgawanyiko mkubwa wa kisiasa unaoshuhudia baadhi ya viongozi wakimuunga mkono Rais William Ruto kuwania muhula wa pili kupitia kauli mbiu ya 'Tutam', huku wengine wakisukuma vuguvugu la 'Wantam' linalosisitiza kuwa Rais anafaa kuhudumu kwa muhula mmoja pekee. Tofauti na viongozi wengi wa kizazi chake, Nyoro hajajitokeza wazi kuunga mkono upande wowote. Badala yake, amechagua kubaki katikati, msimamo ambao sasa unaonekana kuzidi kuwa mgumu huku shinikizo zikiongezeka kutoka kwa marafiki na wapinzani wake wakimtaka atangaze msimamo wake. Wakati huohuo, wapinzani wake wa kisiasa wameanza kujipanga. Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Kenya (CA) Charles Karondo na aliyekuwa mgombea wa ubunge Karanja Wamatangi ni miongoni mwa wanaotajwa kutaka kumng'oa katika uchaguzi ujao. Aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria pia alimkejeli akisema alikuwa amemwonya kuhusu siasa za Mlima Kenya lakini hakusikia. Nyoro pia amekosolewa kutokana na jinsi alivyoshughulikia Mswada wa Fedha wa 2026. Ingawa aliukosoa hadharani, hakupiga kura kuunga mkono wala kuupinga bungeni, hatua iliyowakasirisha wafuasi wa serikali na upinzani kwa pamoja. Wakosoaji wake walimtaja kama mwanasiasa asiyeaminika huku washirika wa serikali wakidai hana msimamo thabiti. Wiki iliyopita, Nyoro aliitisha mkutano na wanahabari uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu. Badala ya kutangaza mwelekeo wake wa kisiasa, aliomba apewe siku 21 hadi 28 zaidi ili afanye mashauriano kabla ya kutoa uamuzi. "Nafahamu matarajio ya wengi na ninajua ninachopaswa kusema ili nipate sifa za haraka. Lakini baada ya kushiriki kwa kiasi kikubwa kuunda serikali hii mwaka 2022, nimepata busara zaidi na sitafanya maamuzi kwa kufuata hisia za wakati," alisema. Aliahidi kuwa baada ya kipindi hicho atatangaza msimamo wake wa kisiasa na kueleza muungano anahisi unafaa kuongoza nchi. Mchambuzi wa siasa John Okumu anasema Nyoro anakabiliwa na shinikizo kubwa zinazozidi uwezo wa mwanasiasa mmoja kufanya uamuzi wa binafsi. Kwa mujibu wake, viongozi wa Mlima Kenya sasa wanapimwa kwa kuonekana waaminifu kwa eneo hilo au wasaliti, hasa kutokana na kuongezeka kwa upinzani dhidi ya utawala wa Rais Ruto. Kwa upande wake, mchambuzi Festus Wangwe anaamini Nyoro huenda anasubiri matokeo ya uchaguzi mdogo wa Ol Kalou wa Julai 16 na mwelekeo wa mazungumzo ya kisiasa yanayoendelea nyumbani kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua huko Wamunyoro, Nyeri, kabla ya kufanya uamuzi wake. Anasema huenda Nyoro pia anatamani kuwa mmoja wa viongozi wakuu wa kisiasa wa Mlima Kenya, lakini shinikizo kutoka kwa umma zinamnyima nafasi ya kuendelea kusubiri kwa muda mrefu. Tangu achaguliwe kuwa Mbunge wa Kiharu mwaka 2017 na kuchaguliwa tena mwaka 2022, Nyoro amejijengea sifa kama mmoja wa wanasiasa vijana wenye ushawishi mkubwa nchini. Ukaribu wake na Rais Ruto uliwahi kuzua tetesi kuwa angeweza kuwa mgombea mwenza wake mwaka 2027. Hata hivyo, kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua mnamo Oktoba 2024 kulibadili kwa kiasi kikubwa siasa za Mlima Kenya, eneo ambalo ndilo ngome kuu ya uungwaji mkono wa Nyoro. Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kikuyu Wachira Kiago anasema eneo hilo bado linamtambua Nyoro kama kiongozi mwenye uwezo, lakini anasisitiza kuwa uamuzi wa mwisho utatolewa na wapiga kura. "Tunamuunga mkono anapoendelea kutafakari kisiasa. Akijiunga na msimamo wa eneo hili atakaribishwa, lakini akichagua njia nyingine hiyo pia ni haki yake ya kidemokrasia. Mwisho wa yote, ni wapiga kura watakaotoa alama," alisema.

from Taifa Leo https://ift.tt/HrIQ1dU
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post