
MTU mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi huku wengine wawili wakijeruhiwa Jumanne wakati maandamano ya kupinga kutoweka kwa vijana wawili yalipogeuka mapigano kati ya waandamanaji na polisi katika maeneo ya Mathare na Kiamaiko, Nairobi.
Marehemu alitambuliwa kuwa mfanyakazi wa kichinjio huko Kiamaiko.
Maandamano hayo yalilemaza shughuli za biashara na usafiri huku waandamanaji wakichoma tairi, kuweka mawe barabarani na kuimba nyimbo za kuikosoa serikali wakitaka wenzao waliopotea warejeshwe.
Waandamanaji walitaka kuachiliwa kwa Abdulaziz Duba Molu maarufu kama Zizou, ambaye familia yake inasema alikamatwa na polisi Juni 23 karibu na Juja Farm, pamoja na kiongozi wa vijana Macmillan Kiarie, ambaye alionekana mara ya mwisho kupitia kamera za CCTV Juni 20 eneo la Mwihoko, Githurai.
Pia walitaka serikali kueleza aliko Michael Oloo, ambaye pia ameripotiwa kutoweka.
Mwanzilishi mwenza wa Mathare Social Justice Centre, Wanjiru Wanjira, alisema maandamano hayo yalilenga kupinga visa vya utekaji nyara.
"Tunataka Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen na Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja kuheshimu Katiba. Hakutakuwa na amani hadi wenzetu warejeshwe," alisema.
Ndugu wa Abdulaziz Duba alisema familia imezunguka vituo mbalimbali vya polisi na hospitali kwa siku saba bila mafanikio.
"Tunatumaini tu atapatikana akiwa hai. Hatujapewa taarifa yoyote na vyombo vya usalama wala hajafikishwa mahakamani," alisema.
Wakazi walisisitiza wataendelea na maandamano hadi watu wote waliopotea wapatikane.
Wakati huo huo, Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (KNCHR) ilitoa ripoti kali ikishutumu serikali kwa ukiukaji wa haki za binadamu wakati na baada ya maandamano ya Juni 25 yaliyoadhimisha mwaka wa pili tangu maandamano ya Gen Z ya mwaka 2024.
Ripoti hiyo ilisema watu saba walitoweshwa kwa nguvu, 361 wakakamatwa, watetezi wa haki za binadamu 18 wakazuiliwa na wanahabari wawili wa kujitegemea kukamatwa.
KNCHR ilisema visa hivyo vinaonyesha ukiukaji mkubwa wa haki za kikatiba, zikiwemo haki ya uhai, uhuru wa kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kuandamana kwa amani.
Tume hiyo ilisema inaendelea kupokea taarifa za watu kutoweshwa, mateso, kukamatwa holela, matumizi ya nguvu kupita kiasi na kuzuiwa kwa uhuru wa kutembea.
Miongoni mwa waliotajwa kutoweka ni Boniface Mulinge Muteti, Elisha Ochieng Alam, Collins Otieno, Fredrick Ojiro, Christine Alubengo na Michael Ngige waliokamatwa nje ya Bunge Juni 25 na kuonekana tena siku mbili baadaye baada ya kutupwa kandokando ya barabara za Lang'ata na Ngong.
Kwa mujibu wa KNCHR, walieleza kuwa walichukuliwa na watu waliokuwa wamevalia kiraia, wakafunikwa macho, wakapelekwa mahali pasipojulikana, wakateswa na baadaye kutupwa barabarani.
Tume hiyo pia ilisema Davis Lichuma, aliyekamatwa wakati wa maandamano, alipatikana hospitalini Juni 28 baada ya kutoweka kwa siku nne.
KNCHR iliwataja Macmillan Kiarie, Michael Oloo na Abdulaziz Duba, ambao kutoweka kwao kulichochea maandamano ya Jumanne, kuwa bado hawajulikani waliko na kuitaka serikali iwafikishe mahakamani mara moja au kuwaachilia ikiwa wanazuiliwa kinyume cha sheria.
Aidha, tume hiyo ilikosoa kukamatwa kwa watu 361 katika kaunti mbalimbali ikisema lazima ichunguzwe iwapo haki zao za kikatiba ziliheshimiwa.
Pia ililaani kukamatwa kwa watetezi wa haki za binadamu 18 na wanahabari wawili waliokuwa wakiripoti maandamano, ikisema hatua hiyo ilikiuka uhuru wa habari.
KNCHR ilitaka uchunguzi huru ufanywe kuhusu matumizi ya risasi dhidi ya waandamanaji, ikiwemo madai ya kupigwa risasi kwa Ben Kamiti mjini Naivasha na kushambuliwa kwa James Mungai, mtu mwenye ulemavu, mjini Nakuru.
Tume hiyo pia ilikosoa vizuizi vingi vya polisi vilivyowekwa Nairobi na maeneo mengine, ikisema vilikwamisha shughuli za kiuchumi na kuzuia wananchi kufika kazini.
Mwenyekiti wa KNCHR, Claris Ogangah, alisema ni jambo la kusikitisha kwamba serikali inaendelea kulipa fidia kwa waathiriwa wa ukiukaji wa haki za binadamu huku madai ya ukiukaji huo yakiendelea kujitokeza.
Tume hiyo ilimtaka Inspekta Jenerali wa Polisi kuchunguza visa vya ufyatuaji risasi, kuhakikisha maafisa wanaolinda maandamano wanatambulika wazi na kutii maagizo ya mahakama kuhusu usimamizi wa mikusanyiko ya umma.
Pia iliitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kupitia upya kesi zote zinazohusiana na maandamano ili kuhakikisha hakuna anayeshtakiwa au kuzuiliwa kinyume cha Katiba.
Ripoti ya Fridah Okachi, Kevin Cheruiyot, Steve Otieno
from Taifa Leo https://ift.tt/5EIhvOs
via
IFTTT