Kaunti zageuka migodi ya utajiri haramu

Wanapoajiriwa katika serikali za kaunti, wengi wao huingia na vyeti vya kitaaluma, wasifu wa kazi na ahadi za kuhudumia wananchi. Hata hivyo, miaka michache baadaye, baadhi yao huondoka wakiwa na majumba ya kifahari, magari ya bei kubwa, ardhi za thamani na mamilioni ya pesa taslimu ambazo wachunguzi wanadai hazilingani na mishahara yao.

Kukamatwa kwa Afisa Mkuu wa Mipango na Maendeleo ya Miji wa Kaunti ya Nairobi, Patrick Analo, wiki hii kumeibua tena mjadala kuhusu ongezeko la utajiri usioelezeka miongoni mwa maafisa wa kaunti tangu kuanzishwa kwa ugatuzi mwaka 2013.

Maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) walipovamia nyumba yake Syokimau, walipata jumla ya Sh65.3 milioni. Pia, walipata hati za mashamba, vyeti vya kumiliki magari, mikataba ya mauzo na idhini za ujenzi.

Lakini kesi ya Bw Analo si ya kipekee.

Mwaka 2024, EACC ilimchunguza afisa wa upangaji wa jiji la Nairobi Wilson Kanani ambaye alipokea mshahara wa takriban Sh55,000 kwa mwezi. Hata hivyo, alihusishwa na mali za thamani ya zaidi ya Sh643 milioni, yakiwemo majengo, magari ya kifahari, akaunti za benki na biashara maarufu ya burudani. Mahakama iliamuru mali hizo zizimwe huku uchunguzi ukiendelea.

Mkurugenzi Mkuu wa EACC, Abdi Mohamud, amesema msako katika nyumba ya Bw Analo umefichua mtandao mpana wa ushahidi ambao awali haukujulikana kwa wachunguzi.

“Wakenya wengi wanaamini baadhi ya maafisa wa kaunti wamegeuza nyadhifa walizopewa kuwa njia ya kujinufaisha wao wenyewe, familia zao na marafiki zao. Hili linatupa wasiwasi mkubwa,” alisema.

Katika Kaunti ya Kiambu, aliyekuwa gavana Ferdinand Waititu alipatikana na hatia ya ufisadi katika zabuni ya ujenzi wa barabara yenye thamani ya Sh588 milioni. Mahakama ilimhukumu kifungo cha miaka 12 gerezani au kulipa faini ya Sh53.5 milioni. Baadaye, mali za thamani ya Sh131.2 milioni zilitaifishwa baada ya kubainika kuwa hakuweza kueleza chanzo chake.

Aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado naye alikubali kukabidhi mali za thamani ya Sh235.6 milioni kwa serikali kupitia makubaliano maalum yaliyofanikisha kufutwa kwa baadhi ya mashtaka ya ufisadi yaliyokuwa yakimkabili.

Katika Kaunti ya Trans Nzoia, wachunguzi walipata Sh61.9 milioni na dola 55,000 katika uchunguzi uliomhusisha Gavana George Natembeya. Hata hivyo, mahakama baadaye ilifutilia mbali kesi hiyo kwa misingi ya ukiukaji wa haki za kikatiba wakati wa uchunguzi.

Kaunti ya Turkana nayo imehusishwa na uchunguzi wa madai ya ulaghai wa Sh600 milioni ambapo Sh6.5 milioni zilipatikana ndani ya gari la afisa mkuu wa fedha wa kaunti hiyo. Busia na Homa Bay pia zimekumbwa na visa vya uchunguzi kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma na utoaji wa zabuni.

Kinachowatia wasiwasi wachunguzi ni mwenendo unaojirudia wa maafisa kuhifadhi mamilioni ya pesa taslimu nyumbani, ofisini au kwenye magari badala ya benki.

“Mara nyingi fedha hizo huwekwa nje ya mfumo wa benki ili kuficha mwelekeo wake na kuzuia wachunguzi kufuatilia miamala,” alisema mpelelezi mmoja wa masuala ya kifedha ambaye hakutaka kutajwa.

Ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, zimeendelea kufichua matumizi mabaya ya fedha katika kaunti nyingi. Ukaguzi maalum wa mwaka 2025 katika kaunti 26 uligundua wafanyakazi hewa 596 waliolipwa mishahara ya karibu Sh978 milioni. Wakuu wa kaunti mbalimbali pia wamehojiwa kuhusu miradi iliyokwama, zabuni zenye utata na malipo yasiyo na uthibitisho.

Zaidi ya Sh400 bilioni hutumwa kwa serikali za kaunti kila mwaka, mbali na mapato zinazokusanya zenyewe. Kiasi hiki kikubwa cha fedha kimeunda mazingira yanayowapa baadhi ya maafisa nafasi ya kujitajirisha kwa njia zisizo halali.

Changamoto kubwa kwa wachunguzi ni kuthibitisha kuwa mali na fedha zinazopatikana zimetokana na ufisadi. Kumiliki pesa nyingi si kosa kisheria. Hivyo, EACC hulazimika kufanya uchambuzi wa kifedha, ukaguzi wa kitaalamu na vita mahakamani ili kuonyesha kuwa utajiri huo hauendani na mapato halali ya mhusika.



from Taifa Leo https://ift.tt/I4fcQ1e
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post