Ajabu mapanga sasa yakigeuzwa silaha kali ya wahuni

MAPANGA yanabadilishwa kutoka zana ya kawaida ya shambani kuwa silaha ya kutisha na kuwashambulia watu, huku ripoti ya kijasusi ikifichua kuwa angalau mapanga 500 yalisambazwa kwa vijana waliozua vurugu wakati wa ziara ya Linda Mwananchi, Homa Bay.
Huku joto la kisiasa likipanda kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, vijana wanaobeba mapanga katika mikutano ya hadhara na makabiliano ya kisiasa wamekuwa chanzo cha wasiwasi.
Zana iliyokuwa ikitumika hasa mashambani sasa inatumika kama silaha ya vitisho na vurugu. Baadhi ya vijana hata wameunda utamaduni wa mapanga, wakitumia nyimbo na densi kama mapangale, inayoiga kitendo cha kutumia panga kukata au kucharaza.
Hali hii inazua swali: Ni rahisi kiasi gani kununua mapanga kwa wingi, na je, Kenya ina sheria za kutosha kudhibiti uuzaji wake?
Kwa sasa hakuna mfumo maalum wa leseni unaohitaji kibali ili mtu anunue au kumiliki panga kwa kuwa inatambuliwa kama kifaa cha kilimo na matumizi ya nyumbani. Hata hivyo, inaweza kugeuka haraka kuwa silaha hatari ikitumiwa na mtu mwenye nia mbaya.
Mara kadhaa, maafisa wa usalama wamewakamata watu wakisafirisha idadi kubwa ya mapanga yanayoshukiwa kunuiwa kutumiwa katika makabiliano.
Jumapili iliyopita, wapelelezi waliwakamata watu wawili waliokuwa na mapanga matano mapya kando ya Barabara ya Ndhiwa, Yamase, Kaunti ya Migori, katika njia iliyotumiwa na msafara wa Linda Mwananchi.
Mapanga pia yamehusishwa na makabiliano ya kisiasa Kisumu na Nairobi. Video inayosambazwa mtandaoni inaonyesha watu wakikabidhiwa panga na Sh1,000 kwa kazi ambayo haijaelezwa.
Matukio hayo yanaibua maswali kuhusu idadi ya mapanga ambayo mtu anaweza kununua kwa wakati mmoja, iwapo maduka yanapaswa kurekodi ununuzi wa mapanga mengi na hatua zinazochukuliwa kuzuia zana hizo kuingia mikononi mwa wahalifu.
Pengo hilo limewaacha baadhi ya wafanyabiashara wakitumia uamuzi wao wenyewe.
Fred Ogolla, mmiliki wa duka la vifaa vya ujenzi Kondele, Kisumu, huruhusu mteja kununua mapanga mawili pekee kwa wakati mmoja na hayabandiki hadharani katika duka lake.
“Mtu akija kwangu kununua mapanga zaidi ya mawili, simruhusu,” alisema Bw Ogolla.Alisema uamuzi huo unatokana na dhamiri yake. “Kama Mkristo, nahisi nitakuwa mshirika wa uhalifu. Ikiwa panga itatumiwa kufanya uhalifu au kusababisha kifo, sitaweza kuishi na jambo hilo,” alisema.
Audi Ogada, mwenyekiti wa Kisumu Residents Voice Association na mwanachama wa zamani wa genge, alisema ujasiri wa vijana kubeba na kutumia mapanga kuwashambulia watu ni jambo la kutia wasiwasi.
Alisema ingawa kuna sheria zinazodhibiti kubeba silaha hadharani, hakuna udhibiti wa kutosha kuhusu ununuzi wa mapanga kwa wingi.
Hata hivyo, maafisa wa usalama wanasema tayari wanachukua hatua kukabiliana na tatizo hilo.
Kamishna wa Kaunti ya Kisumu Mohamed Mwabudzo alisema maafisa huwa macho zaidi kabla ya mikutano ya kisiasa na wakati wa kampeni za uchaguzi.
“Tunategemea mitandao yetu ya kijasusi. Tunaposhuku kuwa kuna shughuli haramu au ununuzi unaofanywa, tunatoa tahadhari na kuchukua hatua kabla ya jambo kutokea,” alisema.
Alisema maafisa wa usalama wanaweza pia kushirikiana na maduka ya vifaa vya ujenzi ili yaripoti ununuzi unaotia shaka.
Bw Mwabudzo pia aliwataka wananchi kuripoti wanapoona ununuzi wa mapanga kwa wingi.
Alisema mtu anayebeba au kutumia panga hadharani anaweza kukamatwa iwapo polisi wataamua kuwa linatumika kama silaha hatari.


from Taifa Leo https://ift.tt/lwASf8r
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post