
TANGAZO la Katibu Mkuu wa UDA, Hassan Omar kuwania ugavana Mombasa mwaka 2027 limezua mgawanyiko katika ushirikiano unaoibuka kati ya UDA na ODM, huku juhudi za kugawana maeneo ya kisiasa Pwani zikikabiliwa na changamoto.
Bw Omar ametangaza kuwa ataendelea na azma yake ya kuwania kiti hicho, hatua inayotishia mpango wa vyama hivyo kuepuka kushindana moja kwa moja katika baadhi ya kaunti.
Kwa zaidi ya mwezi mmoja, viongozi wa UDA na ODM wamekuwa wakijadili uwezekano wa kugawana maeneo, ambapo kila chama kingepewa nafasi ya kuongoza katika kaunti fulani huku kingine kikimuunga mkono mgombea wake.
Hata hivyo, Bw Omar amekataa mpango huo akisema wapiga kura wanapaswa kuwa huru kuchagua viongozi wanaowataka.
“Tuungane na tuchague viongozi wetu kwa uhuru. Kwale tumeona ODM haitaki ugawaji wa maeneo, nasi UDA hatutaki. Hatuwezi kuamriwa na mtu, tutafanya maamuzi yetu,” alisema Bw Omar.
Kauli hiyo imeweka mashakani juhudi za kubadilisha ushirikiano wa kitaifa kati ya UDA na ODM kuwa muungano wa kisiasa wa kuelekea uchaguzi wa 2027.
Mombasa ni ngome ya muda mrefu ya ODM, huku UDA ikijaribu kupanua ushawishi wake katika eneo hilo.
Kuingia kwa Bw Omar katika kinyang’anyiro hicho kunaweza kuwa mtihani wa uwezo wa UDA kuvunja ngome hiyo na pia wa ODM kuhifadhi umaarufu wake baada ya kuingia katika serikali ya muungano mpana.
Changamoto hiyo pia imejitokeza Kwale, ambako baadhi ya wanachama wa ODM wanataka chama hicho kutoa mgombea wake wa ugavana badala ya kumuunga mkono Gavana Fatuma Achani anayehusishwa na UDA.
Wiki iliyopita, Waziri wa Madini, Hassan Ali Joho alikumbana na upinzani kutoka kwa baadhi ya wanachama wa ODM katika mkutano Vingujini, Kwale.
Mkazi Donate Mwavale alimtaka Bw Joho kuwasikiliza wananchi, hasa wanawake, kabla ya viongozi kufanya maamuzi kuhusu ushirikiano wa kisiasa.
“Huo uongozi wako tutauvua usipotusikiza,” aliambia Bw Joho.
Mivutano hiyo inaonyesha ugumu wa kutekeleza makubaliano ya kisiasa yanayofanywa na viongozi wa kitaifa bila kuzingatia matarajio ya wanasiasa na wapiga kura wa mashinani.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kisiasa, Mombasa, Kilifi na Tana River zimekuwa zikitajwa kuwa maeneo ambayo ODM inaweza kupewa nafasi zaidi, huku UDA ikitarajiwa kuzingatia Kwale, Taita-Taveta na Lamu.
Hata hivyo, azma ya Bw Omar inaweza kuvuruga mpango huo na kuongeza ushindani kati ya vyama hivyo.
Kwa UDA, kushinda Mombasa kungeipa nafasi ya kupanua mizizi yake Pwani na kubadilisha ramani ya kisiasa ya eneo hilo.
Kwa ODM, kupoteza kaunti hiyo kungekuwa pigo kubwa kwa chama kinachojaribu kujenga upya nguvu zake baada ya kifo cha kiongozi wake wa muda mrefu Raila Odinga.
Huku uchaguzi wa 2027 ukikaribia, Mombasa na Kwale huenda zikawa maeneo muhimu ya kupima iwapo UDA na ODM zinaweza kuwa washirika wa uchaguzi au zitaendelea kuwa washirika wa serikali pekee.
from Taifa Leo https://ift.tt/Mr86hUV
via
IFTTT