
NAIBU Rais Rigathi Gachagua ameapa kutembelea Emurua Dikirr, Narok, leo Ijumaa licha ya vitisho kutoka kwa viongozi wa eneo hilo.
Chama chake cha Democracy for Citizens Party (DCP) kimesema Bw Gachagua atatumia ziara hiyo kuwashukuru wakazi waliounga mkono chama hicho katika uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika hivi majuzi.
Pia, anatarajiwa kuzungumzia masuala ya ardhi na kile anachodai ni kushindwa kwa serikali kulinda haki za wakazi kuhusu ardhi.
Mvutano kuhusu ziara hiyo umeongezeka huku viongozi wanaounga mkono serikali na wale wa upinzani wakibadilishana kauli kali.
Katika uchaguzi mdogo wa Emurua Dikirr, mgombea wa DCP Vincent Rotich alipata kura 10,760, huku mgombea wa UDA David Keter akishinda kwa kura 18,266.
Bw Gachagua amesema kura hizo ni ishara kwamba chama chake kinaanza kupata uungwaji mkono katika eneo linalochukuliwa kuwa ngome ya Rais William Ruto.
Nitakuwa Emurua Dikirr Agosti 21 kuzungumza na watu walioniamini na kuunga mkono chama cha DCP licha ya changamoto zote,” alisema.
Bw Gachagua pia atatembelea familia ya aliyekuwa Mbunge wa Emurua Dikirr Johana Ng’eno katika kijiji cha Mogindo kutoa rambirambi, miezi mitano baada ya kiongozi huyo kufariki katika ajali ya helikopta.
Jumatano, Bw Gachagua alizungumza kwa simu na mama wa marehemu, Mama Mary Temas, na kumthibitishia kwamba angemtembelea leo.
Pia amesema atatumia ziara hiyo kuzungumzia kifo cha Bw Ng’eno na kucheleweshwa kwa ripoti ya uchunguzi wa ajali hiyo.
Ajali hiyo ilitokea Februari 28, 2026 katika kijiji cha Chepkiep, kaunti ya Nandi. Watu sita walifariki.
Waliofariki ni Bw Ng’eno, rubani George Were, mpiga picha Nick Kosgei, afisa wa Huduma ya Misitu Kenya Amos Kipngetich Rotich, mwalimu Carlos Robert Kibet Keter na afisa wa itifaki wa Serikali ya Kaunti ya Narok Wycliff Kiprotich Rono.
Serikali iliahidi kutoa matokeo ya uchunguzi, lakini ripoti hiyo bado haijatolewa hadharani na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Kenya (KCAA).
Bw Gachagua na marehemu Ng’eno walikuwa washirika wa karibu kisiasa kabla ya mchakato wa kumuondoa Bw Gachagua kama Naibu Rais kuanza.
Wakati huo, Bw Ng’eno alikuwa miongoni mwa wabunge waliosemekana kuwa hawakuunga mkono kwa dhati juhudi za kumtimua Bw Gachagua.
Mbunge Keter amemuonya Bw Gachagua kutotembelea Emurua Dikirr, akisema ziara yake inaweza kuvuruga amani.
“Nataka kumuonya Bw Gachagua asikanyage Emurua Dikirr kwa sababu hajaribishwi hapa. Aelekeze nguvu zake kwingine kwa kuwa hapa ni eneo la UDA,” alisema.
Mbunge huyo pia alimlaumu Bw Gachagua kwa kuwakosoa mara kwa mara wanachama wa jamii ya Kalenjin katika mikutano ya kisiasa huku akitafuta uungwaji mkono wao kuelekea uchaguzi wa 2027.
Naibu Gavana Koech pia alisema ziara hiyo haitakuwa rahisi.
“Imekuwa wazi kwamba Bw Gachagua amejaribu uvumilivu wetu. Hatuwezi tena kukaa kimya. Hawezi kututukana halafu aje katika eneo letu kutafuta uungwaji mkono,” alisema.
Lakini Bw Gachagua amepuuzilia mbali vitisho hivyo.
Amesema amekuwa mwathiriwa wa mashambulizi zaidi ya 25 ambayo amedai yalifanywa na makundi yanayoungwa mkono na serikali pamoja na maafisa wa polisi.
“Mpaka sasa nimeshambuliwa zaidi ya mara 25. Hii haijapunguza kasi yangu. Niko tayari kukabiliana na mengi zaidi,” alisema akiwa Murang’a.
Amesema hakuna vitisho vitakavyomzuia kutembelea Emurua Dikirr.
“Wacha watuletee vurugu. Nimepata taarifa kwamba wanapanga kufanya hivyo, lakini hilo halitatuzuia. Tutaendelea na ziara yetu bila woga,” alisema.
Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot na Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago wamesema Bw Gachagua ana haki ya kutembelea Rift Valley.
Bw Cheruiyot alisema jamii ya Kipsigis haiwafukuzi wageni na kwamba Bw Gachagua atakaribishwa kama mwanasiasa mwingine.
“Katika utamaduni wetu kama jamii ya Kipsigis, hatuwafukuzi wageni. Tunawakaribisha wafanye shughuli zao na waondoke kwa amani. Tutajitokeza kukusalimia, lakini usifikirie kwamba hiyo itakuletea kura mwaka ujao,” alisema.
Bw Mandago alisema jamii ya Rift Valley haitakubali kuchochewa kufanya vurugu kwa misingi ya siasa.
from Taifa Leo https://ift.tt/LzhygRU
via IFTTT