Kauli ya Wetang’ula kwamba ajira za TSC hugawiwa wabunge Ikulu yachemsha vyama

VYAMA vya walimu vimekasirishwa na matamshi ya Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula kwamba baadhi ya wabunge hupewa barua za ajira za Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) katika Ikulu.

Chama cha Walimu Nchini (KNUT), Muungano wa Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Anuwai (KUPPET) na Muungano wa Walimu wanaofundisha maeneo kame (KETHAWA), wote wamesema kauli hiyo imeibua upya madai ya mapendeleo ya kisiasa katika kuwaajiri walimu.

Bw Wetang’ula alisema mwishoni mwa wiki kwamba baadhi ya wabunge huandamana naye hadi Ikulu na kupewa hadi barua 10 za ajira za walimu, lakini baadaye huziuza kwa Sh400,000 kwa kila mzazi.

“Baadhi ya wabunge ninaowapeleka kwa Rais hupewa hadi barua 10 za ajira za walimu. Lakini baadaye unasikia wamekuwa wakiziuza,” akasema Bw Wetangúla.

Alisema kitendo hicho si cha kimaadili, hasa kwa wazazi maskini wanaolazimika kutafuta fedha nyingi ili watoto wao wapate ajira.

Kauli hiyo imezua wasiwasi wakati TSC imechapisha nafasi 20,000 za ajira za walimu wa shule za sekondari za chini.

Naibu Katibu Mkuu wa Kuppet Moses Nthurima alisema madai hayo ni ya kusikitisha na yanalemaza uhuru wa TSC, ambayo ni tume huru ya kikatiba.

Alisema walimu waliohitimu miaka mingi iliyopita na kupata alama za juu katika mahojiano wanafaa kupewa kipaumbele badala ya nafasi kupewa watu wenye uhusiano na wanasiasa.

“TSC ina sera ya kuajiri. Waliohitimu mapema na kupata alama za juu katika mahojiano wanapaswa kuwa na nafasi kubwa ya kuajiriwa,” akasema.

Katibu wa Kitaifa wa Kethawa Ndung’u Wangenye alisema kauli ya Spika imethibitisha madai ya muda mrefu kwamba wanasiasa huingilia mchakato wa kuwaajiri walimu.

Mwenyekiti wa Kitaifa wa Kuppet Omboko Milemba alisema walimu lazima waajiriwe kupitia TSC pekee, kwa kuwa hiyo ndiyo taasisi iliyopewa jukumu hilo kikatiba.

Naibu Katibu Mkuu wa Knut Hesbon Otieno alisema baadhi ya walimu wameomba ajira mara nyingi bila mafanikio huku wengine wakipata nafasi kupitia uhusiano wa kisiasa.

Hata hivyo, TSC imepuuza madai hayo na kusisitiza kuwa mchakato wake wa kuwaajiri walimu hufanywa kwa haki na ushindani kwa mujibu wa Katiba na sheria.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TSC Evaleen Mitei alisema ajira hufanywa katika ngazi ya kaunti ndogo baada ya nafasi kutangazwa rasmi na miongozo ya uteuzi kuchapishwa.

Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba alisema serikali itashirikiana na TSC kukabiliana na uuzaji wa nafasi za ajira, akisema ni uhalifu unaopaswa kukomeshwa.



from Taifa Leo https://ift.tt/OPig2R4
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post