Wantam: Sifuna atua Meru kwa kishindo!

SIKU chache baada ya kukumbwa na ghasia zilizosababisha vifo katika Kaunti ya Homa Bay, viongozi wa vuguvugu la Linda Mwananchi jana walijipigia debe katika Kaunti ya Meru wakisema hakuna kiwango cha ghasia kitakachozima kiu chao cha mabadiliko. Vuguvugu hilo linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, lilifika Meru kwa mapokezi makubwa mwenyeji wao akiwa aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza, ambaye pia ni kiongozi wa Umoja na Maendeleo Party (UMP). Viongozi hao walihutubia wananchi katika maeneo ya Kiirua, Githongo, Nkubu, Meru mjini na Kianjai. “Tunawashukuru watu wa Meru kwa kudumisha amani na kuonyesha jinsi demokrasia inavyopaswa kufanya kazi,” akasema Bw Sifuna. Katika mikutano hiyo, Bw Sifuna aliishambulia serikali ya Rais William Ruto, akiilaumu kwa kupuuza Katiba, sheria na ahadi ilizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi. Alisema lengo la Linda Mwananchi ni kurejesha utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na kuimarisha demokrasia. “Rais Ruto alikuwa ameahidi kuheshimu Katiba, siku moja tu baada ya maadhimisho ya miaka 16 ya Katiba, wafanyabiashara walitandikwa na kurushiwa vitoza machozi Nairobi walipokuwa wakipinga ushuru wa juu,” akasema Bw Sifuna. Katibu huyo wa zamani wa ODM pia alimshambulia Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen, akisema ameshindwa kukabiliana na uhuni na makundi ya vijana wanaovuruga mikutano ya upinzani. Alisema iwapo Linda Mwananchi itaunda serikali ijayo, Bw Murkomen atakuwa miongoni mwa mawaziri wa kwanza kuondolewa. Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa vyama vya upinzani kuungana ili kumenyana na Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027. Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino alisema upinzani unapaswa kuwasilisha mgombea mmoja wa urais ili kuongeza nafasi ya kuwahi ushindi. Vilevile, viongozi hao waliishutumu serikali kwa kushindwa kushughulikia ukosefu wa ajira na gharama ya juu ya maisha. Bw Owino aliikosoa serikali kuhusu zabuni ya Sh2.5 bilioni ya sare za polisi, akisema fedha hizo zingetumika vyema kuanzisha viwanda na kuunda nafasi za ajira kwa vijana. Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya aliitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuimarisha mifumo yake na kuhakikisha uchaguzi wa 2027 utakuwa huru na wa kuaminika. “Serikali inatoa vitambulisho kwa vijana ambao hawajafikisha umri wa miaka 18 katika baadhi ya sehem za nchi. IEBC inafaa kuwa chonjo na kuzima juhudi zozote za udanganyifu,” akasema Bw Natembeya. Viongozi hao pia walimtetea Bi Mwangaza, wakidai aliondolewa madarakani kwa njia isiyo ya haki na wanasiasa wanaounga mkono serikali.

from Taifa Leo https://ift.tt/P9Ynw7h
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post