MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imetunukiwa tuzo ya kuwa miongoni mwa Mashirika ya Umma yanayojiendesha kibiashara kwa ufanisi wa huduma na ukusanyaji wa mapato.
Tuzo ilitolewa leo jijini Arusha na Rais Samia Suluhu Hassan katika kikao cha kazi cha Wenyeviti wa Bodi pamoja na Wakuu wa Taasisi za Umma na mashirika ya serikali.
Tuzo kutoka kwa Rais Samia ilikabidhiwa kwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TPA, Dkt. Elinami Minja, ambaye aliambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Plasduce Mbossa.
Kikao cha kazi cha siku tatu kilichoanza leo kinahudhuriwa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) na kinatarajiwa kumalizika Ijumaa.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho, Rais Samia alieleza umuhimu wa mashirika ya umma kutimiza majukumu yao ili kuchangia kuvutia wawekezaji zaidi nchini na kuongeza ufanisi wa mashirika hayo.
Rais Samia aliziagiza taasisi za umma kuhakikisha zinafanya kazi kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria na taratibu, ili kuongeza uzalishaji na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Alibainisha kuwa, ili Tanzania iweze kushindana katika soko la kimataifa, ni muhimu kuhakikisha kuwa bidhaa na huduma zinazozalishwa na mashirika ya umma zinakidhi viwango vya kimataifa.
Rais Samia alitoa mfano wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), akisisitiza kwamba shirika hilo lazima lihakikishe kuwa bidhaa zote zinazozalishwa nchini zinakidhi viwango vya kimataifa, na wakati huo huo, kulinda bidhaa za ndani dhidi ya ushindani usio wa haki kutoka kwa bidhaa duni za kigeni.
Aliwaomba TBS wawe makini katika kusimamia viwango ili kuhakikisha kuwa bidhaa za Tanzania zinaweza kushindana vizuri katika masoko ya nje na ndani.
Aidha, Rais Samia aliihimiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya kazi kwa weledi ili kuondoa malalamiko ya wawekezaji yanayohusiana na kodi.
Aliwaomba wahakikishe kwamba mfumo wa kodi unakuwa rafiki kwa wawekezaji, jambo ambalo litasaidia kuvutia wawekezaji zaidi nchini.
Aliongeza kuwa TRA inapaswa kuwa na utaratibu mzuri wa kusaidia wafanyabiashara wa ndani ili waweze kukuza biashara zao na kushindana katika soko la kimataifa.
Rais Samia pia aliwaomba viongozi wa mashirika ya umma kuwa wabunifu na kufikiria njia za kuwekeza lakini alisisitiza kwamba kabla ya kufanya hivyo, lazima wawe na mpango madhubuti na wafanye utafiti wa kina.
Alikumbusha kuwa baadhi ya mashirika yamepoteza fedha nyingi kwa kufanya uwekezaji usio na tija kutokana na kutofanya utafiti wa kutosha.
Rais Samia aliwataka viongozi wa mashirika ya umma kushirikiana na sekta binafsi ili kuimarisha uchumi wa nchi.
Aliwahimiza kujadili jinsi mashirika ya umma yanavyoweza kusaidia sekta binafsi kupata masoko mapya na kuongeza uzalishaji wa ndani.
Rais Samia aliwataka viongozi kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uwazi na kuhakikisha wanatumia rasilimali za umma kwa uangalifu ili kuleta maendeleo kwa taifa zima.
Aliwahimiza wawekeze katika maeneo yenye tija ambayo yataongeza mapato kwa nchi, badala ya kufanya maamuzi ya kisiasa ambayo hayana tija kwa uchumi wa taifa.
0 Comments