JIJI la Nairobi limeanza kuchukua hatua kali dhidi ya hatari inayotokana na taka za hospitali zinazotupwa visivyo.
Utupaji wa taka hizo umetajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa magonjwa sugu kama vile saratani.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Usimamizi wa Taka za Matibabu katika Kaunti ya Nairobi James Muita suala la uchafuzi wa hewa halijapewa uzito unaostahili kwa muda mrefu.
“Watu wengi huenda hospitalini kutafuta huduma za afya lakini hawajiulizi taka hutupwa vipi. Serikali inatumia rasilimali kutoa huduma na pia, inapaswa kuweka bajeti ya kutosha kushughulikia taka zinazotokana na huduma hizo,” alisema Bw Muita.
Bw Muita alieleza kuwa ingawa njia ya kawaida ya kuteketeza taka za hospitali ni kwa kutumia majokofu ya kuchoma taka (incinerators), vifaa vingi vinavyotumika havifiki viwango vinavyotakiwa.
“Majokofu ya kuchoma yanapaswa kuwa na vyumba viwili. Chumba cha kwanza kifike nyuzi joto 800 na cha pili kinachochoma moshi kifike nyuzi 1200. Vinginevyo, moshi huo huwa sumu,” alifafanua.
Ili kupunguza hatari hiyo, Kaunti ya Nairobi sasa inapendekeza mabadiliko kutoka kwa kuchoma taka hadi matumizi ya teknolojia zisizotumia moto mkali, maarufu kama non-thermal technologies. Teknolojia hizi hutumia umeme na joto la kawaida kuangamiza vimelea bila kutoa hewa chafu.
“Teknolojia ya microwave inayotumika nyumbani sasa inatumika pia kuteketeza taka za hospitali kwa usalama,” alisema Bw Muita.
Hata hivyo, mabadiliko haya yanahitaji fedha, suala ambalo limekuwa changamoto kubwa. Alisema kuwa sekta ya usimamizi wa taka haipati bajeti ya kutosha.
“Tunaponunua dawa na vifaa vya matibabu, hatutengi pesa za kuteketeza taka hizo kwa usalama. Ndiyo maana tunahimiza ushirikiano wa sekta binafsi kusaidia katika ukusanyaji, utenganishaji, usafirishaji, na uteketezaji salama wa taka,” alieleza Bw Muita.
Kenya ina sheria za kutosha, zikiwemo Sheria ya Afya ya Umma (Cap 242) na Katiba inayohakikisha kila raia ana haki ya kuishi katika mazingira safi na salama.
Lakini utekelezaji wa sheria bado ni changamoto.
“Hatutaki sheria ziwe za kuadhibu tu, bali ziwe za kusaidia. Tunataka kusaidia hospitali zifike viwango vya kimazingira,” alisema Bw Muita.
from Taifa Leo https://ift.tt/RHjieJY
via IFTTT