Polisi watachukulia waandamanaji kama wahalifu, sio watoto wa watu, asema Ruto

WIKI moja baada ya kutoa wito kwa polisi kuwapiga risasi miguuni waandamanaji wanaopinga serikali, Rais William Ruto Jumapili, Julai 20, 2025 alisisitiza kuwa polisi wana haki ya kutumia nguvu kudhibiti maandamano. Katika onyo la kutisha, amesema polisi watawachukulia waandamanaji kama wahalifu. "Polisi wamefunzwa kukabiliana na wahalifu. Hawajafunzwa kulea watoto. Kwa hivyo, ukiwakabidhi polisi watoto wako unatarajia nini? Tuwe watu wa kuwajibika," alisema Rais Ruto katika Kanisa la AIC Bomani, Kaunti ya Machakos, katika hotuba ambayo ililenga kuwahusisha wazazi na kanisa katika kudhibiti maandamano ya kizazi cha Gen Z yanayokabili serikali yake. Kauli ya kuwataka polisi kuwapiga risasi waandamanaji kwenye miguu imezua upinzani mkali kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu na viongozi wa upinzani. Rais Ruto alitoa wito huo baada ya maandamano ya Saba Saba ambayo yalisababisha vifo vya watu wasiopungua 40 na wengine wengi kujeruhiwa. Jana, Rais alionekana kuashiria kuwa vijana wanaoshiriki maandamano ni watoto waliokosa malezi bora na ambao wangekuwa watu bora iwapo wangelelewa vizuri na kupata msingi wa maadili kupitia kanisa. "Malezi ni jukumu tulilopewa na Mungu. Kama wazazi, msitelekeze wajibu wenu wa malezi. Msikabidhi jukumu hilo kwa kanisa au serikali. Msiruhusu watoto wenu kulelewa mitaani na watu wengine. Zungumza na watoto wako. Kulea kizazi kijacho cha Kenya ni jukumu la jamii. Inahitaji wazazi, kanisa na serikali kulea kizazi cha wananchi wanaowajibika," alisema Rais Ruto alipohudhuria sherehe ya kumweka wakfu Mchungaji Benjamin Kalanzo kama kiongozi mpya wa Kanisa la Africa Inland Church (AIC) eneo la Machakos, pamoja na msaidizi wake Mchungaji Amos Ndunda. Waziri wa Leba Alfred Mutua, Katibu wa Uchukuzi wa Anga Terry Mbaika, Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti, na wabunge Caleb Mule (Machakos mjini), Vincent Musyoka (Mwala), Joshua Mwalyo (Masinga), na Mwengi Mutuse (Kibwezi Magharibi) pia walihudhuria hafla hiyo. Rais Ruto alitumia fursa hiyo kuwakejeli wapinzani wake wa kisiasa aliowaita 'wakosoaji wa kila jambo,' huku akijivunia mafanikio ya serikali yake katika nyanja za uchumi, kilimo, ajira kwa vijana, na afya kupitia mpango wa Afya unaosimamiwa na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA). "Baadhi ya kaunti bado zinawalipiza wagonjwa katika hospitali za ngazi ya 2, 3 na 4. Ziache mara moja. Tumesema wagonjwa watibiwe bure. Serikali ya Kenya italipia kupitia SHA," alisema.

from Taifa Leo https://ift.tt/XC3S2zP
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post