MAKUBALIANO ya pamoja ya mwaka 2021–2025 (CBA) kati ya vyama vya walimu na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ya kima cha Sh33.8 bilioni yameleta masikitiko kwa maelfu ya walimu waliokuwa na matumaini makubwa, baada ya kupokea maelezo ya mishahara ya Julai.
Ingawa nyongeza ya mishahara ilitangazwa kwa mbwembwe, walimu wengi wanasema mabadiliko katika mishahara yao ni madogo mno na hayalingani na matarajio yao, hasa ikizingatiwa ongezeko la gharama ya maisha.
Wengine wanashuku hakuna uwazi na haki katika utekelezaji wa makubaliano hayo, wakilaumu vyama vyao kwa kutia saini makubaliano duni.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo mapya, walimu wa daraja la juu zaidi (D5) wanatarajiwa kupata hadi Sh167,415, ikiwa ni ongezeko la asilimia 5. Walimu wa daraja la chini (B5) walipangiwa kuongezwa mshahara kutoka Sh23,000 hadi Sh29,000 kwa mwezi.
“Tulikuwa tunapigania walimu wanaolipwa mishahara ya chini wapate nyongeza ya asilimia 100, huku wa mishahara ya juu wakipata asilimia 50. Hii ingewiana na malengo ya kupunguza pengo la kipato kati ya walimu wa chini na wa juu,” alisema Moses Nthurima, Naibu Katibu Mkuu wa KUPPET.
Hata hivyo, walimu kutoka maeneo mbalimbali wamelalamikia nyongeza ya chini mno kwenye mishahara yao ya Julai, wakisema walitegemea marupurupu makubwa kutokana na makubaliano hayo mapya.
“Ni huzuni watu wanapofikiria kuwa walimu wamepewa mabilioni, ilhali ukweli ni kwamba ni kama hatujapata chochote. Mimi nimeongezwa Sh1,000 pekee, na baada ya makato ninabaki na Sh600. Katika uchumi wa sasa, Sh600 itakusaidiaje? Kwa kweli inatamausha,” alisema mwalimu mmoja kutoka Kakamega.
Walimu wengi wanalalamikia utekelezaji wa upendeleo, wakisema walimu wa kawaida darasani wameachwa nyuma, huku wale walio katika nyadhifa za usimamizi wakipata nyongeza kubwa.
“Nipo kwenye kundi la kazi C3, nyongeza yangu ilikuwa Sh1,787, ila PAYE, NHIF, makato ya nyumba, na pensheni yalichukua sehemu kubwa. Lakini kilichonikera zaidi ni chama chetu cha KUPPET kunikata mara mbili – Sh1,063 na Sh456. Nahisi Sh456 ni ya mazungumzo ya CBA, lakini kwa nini tuwalipe tena ilhali tunawalipa kila mwezi? Huu ni unyonyaji,” alieleza mwalimu mwingine.
Walimu wanaendelea kusambaza maelezo yao mtandaoni, wakionyesha kuwa baadhi waliongezwa hadi Sh360 tu.
“Kwa kweli, iko wapi hii nyongeza ya mshahara wa walimu iliyotangazwa sana? Mwalimu anaongezwa Sh256 tu, na tuliambiwa tutatabasamu hadi benki? Huu ni mzaha. Kwa miaka minne, hiyo ni chini ya Sh1,000. Waliofaidika ni vyama vya walimu pekee. Hata siwezi kumshauri mwanangu awe mwalimu. Kwa nini tunakatwa ada ya chama ilhali hatupati chochote?” alihoji mwalimu mmoja kutoka Nairobi.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, tawi la KUPPET Kaunti ya Vihiga limelalamikia kile walichokitaja kama “makato haramu” kwenye mishahara ya Julai 2025.
Katika barua kwa Katibu Mkuu Akelo Misori, tawi hilo limeitaka ofisi ya kitaifa kueleza kuhusu makato ya ajabu yaliyotajwa kama ya KUPPET ambayo wanadai hayakuidhinishwa na wanachama.
from Taifa Leo https://ift.tt/65jLwSl
via IFTTT