Familia yafurahi Nduta hatanyongwa Vietnam; juhudi sasa ni kuomba msamaha wa Rais

FAMILIA ya Margaret Nduta, ambaye alihukumiwa kifo nchini Vietnam, imesema kuwa hukumu hiyo imesababisha msongo mkubwa wa mawazo kwao, japo wanafurahi kwamba adhabu hiyo ya kifo haikutekelezwa dhidi yake. Nduta alihukumiwa kuuawa baada ya kupatikana na kilo 2 za mihadarati, kosa ambalo awali lilihusishwa moja kwa moja na adhabu ya kifo chini ya sheria ya jinai ya Vietnam. Alhamisi, Mahakama ya Juu ya Vietnam ilipunguza adhabu hiyo na badala yake ikampa kifungo cha maisha gerezani. Atakuwa na fursa ya kuwasilisha ombi la msamaha kwa Rais wa nchi hiyo, jambo ambalo Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Kenya imesema itafuatilia kwa karibu. Nduta anatoka kijiji cha Weithaga, eneobunge la Kiharu, kaunti ya Murang’a. Jana, Rosemary Macharia ambaye ni dada yake Nduta, alisema kuwa familia ilipokea kwa mikono miwili uamuzi wa mahakama lakini wakakiri kuwa kufungwa jela maisha bado kunawatia hofu kubwa. Alisema mama yao ndiye aliyeathirika zaidi na amelazimika kutumia dawa kutokana na hali yake kiafya. “Mama yangu alianza kuugua alipopata habari za masaibu ya dada yangu. Tangu wakati huo amekuwa akitumia dawa. Hata hajafahamu kuhusu uamuzi mpya wa mahakama na hatutaki azidi kusononeka kwa sasa,” alisema. “Kwa sasa nimetoka hospitali na kumweleza kuhusu suala hilo kutamletea msongo zaidi. Tunangoja tuone hatua itakayofuata ili tuweze kumsaidia dada yetu,” aliongeza. Nduta ni mzaliwa wa mwisho katika familia ya wasichana wanne. Alizaliwa mwezi Oktoba mwaka wa 1988. Uamuzi huo uliotolewa Alhamisi unafuatia mageuzi ya kisheria nchini Vietnam ambayo yaliondoa adhabu ya kifo ya moja kwa moja kwa baadhi ya makosa, ikiwemo ulanguzi wa dawa za kulevya. Uamuzi wa mahakama sasa unampa Nduta nafasi ya kuwasilisha ombi la msamaha au kupunguziwa adhabu kutoka kwa Rais wa Vietnam, ambaye ana mamlaka ya kikatiba kusamehe wafungwa. Kabla ya mageuzi hayo, mtu aliyekamatwa na gramu 100 za mihadarati alikuwa akihukumiwa kifo moja kwa moja. Nduta alikamatwa na kilo 2 za mihadarati alipowasili Vietnam Julai 2023.


from Taifa Leo https://ift.tt/hBkZNEw
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post