MRENGO wa Upinzani umeanza kuchunguza uwezekano wa kuunda muungano unaofanana na wa Narc ulioshinda uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2002, ukijiandaa kwa uchaguzi wa 2027.
Hii ni licha ya migogoro kujitokeza kuhusu uteuzi wa wagombeaji wa pamoja katika chaguzi ndogo 23 zijazo, hali inayofananishwa na mvutano wa uteuzi uliokumba muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya kabla ya uchaguzi wa 2022.
Kuelekea katika uchaguzi huo uliopita, muungano wa Azimio uliokuwa ukimuunga mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga kugombea urais, ulikosa kusimamisha wagombeaji wa pamoja katika maeneo kadhaa, hali iliyosababisha ushindani kati ya vyama tanzu na mwishowe ukapoteza viti vingi.
Ushirikiano huu mpya, unaojulikana kama “Upinzani Ulioungana” unaongozwa na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.
Wameahidi kusimamisha wagombeaji wa pamoja katika chaguzi ndogo zijazo lakini mvutano mkubwa na kampeni sambamba kwa kila chama zinazoendelea mashinani zinaashiria hali tofauti.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilitangaza wazi viti 23 vinavyojumuisha sita katika Bunge la Kitaifa, kimoja katika Seneti, na 16 katika mabunge ya kaunti.
Viti vya ubunge vilivyo wazi ni pamoja naMagarini (Kilifi), Banissa (Mandera), Ugunja (Siaya), Malava (Kakamega), Mbeere Kaskazini (Embu), Kasipul (Homa Bay) na kiti cha Seneti cha Baringo.
Jana, viongozi wa upinzani Kalonzo Musyoka (Wiper), Martha Karua (People’s Liberation -PLP) na Eugene Wamalwa (DAP-K) waliongoza wengine kuonyesha umoja wao licha ya changamoto zinazowakumba.
“Tutakuwa na wagombeaji wa pamoja na tutashinda serikali hii kuanzia Banisa hadi Malava,” alisema Bw Wamalwa kwenye kikao na wanahabari katika makao makuu ya PLP, Nairobi.
Hata hivyo, licha ya msimamo huo, katika eneo la Malava, DAP-K na chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na Bw Gachagua tayari vimeanza kupambana vikali kisiasa, vikidhihirisha mivutano mikubwa ya ndani.
DCP inatamani kiti cha Malava ambacho kiko katika Kaunti ya Kakamega, ngome ya Naibu Kiongozi wa DCP, Cleophas Malala.
DCP inamsimamisha Edgar Busiega, huku DAP-K ikimpa tiketi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wauguzi (KNUN), Seth Panyako.
“Kiongozi wetu wa chama pamoja na Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) wamejitolea kuhakikisha kuwa DCP inashinda zaidi ya asilimia 50 ya viti katika chaguzi ndogo,” alisema Malala wakati wa kuzindua wagombeaji wao jijini Nairobi.
Eneo lingine linalozua mvutano ni Mbeere Kaskazini, ambako kiti kilibaki wazi baada ya Geoffrey Ruku kuteuliwa kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma kuchukua nafasi ya Justin Muturi.
Bw Ruku alichaguliwa kwa tiketi ya Democratic Party (DP) mwaka wa 2022, chama kinachoongozwa na Bw Muturi ambacho sasa kimejitokeza kudai nafasi hiyo na kimesisitiza kina haki ya kusimamisha mgombeaji mmoja wa upinzani.
Hata hivyo, vyanzo vya habari kutoka ndani ya upinzani vinaeleza kuwa DCP ya Gachagua, Jubilee ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, na PLP, vyama hivyo vyote vyenye asili katika eneo la Mlima Kenya, vinalenga kusimamisha wagombeaji wao katika eneo hilo.
Huku Bw Gachagua akitaka kuthibitisha ushawishi wake katika eneo lililompigia kura Rais Ruto kwa wingi, Jubilee na PLP pia zinataka kuonyesha nguvu zao kwa kusimamisha wagombeaji.
Katibu Mkuu wa DP, Jacob Haji, alisema chama hicho kinalenga kutetea kiti hicho kilichokuwa chake.
“Tutamsimamisha mgombeaji wetu katika Mbeere Kaskazini kwa sababu hicho kilikuwa kiti chetu. Hatutakubali kusukumwa kando na DCP au chama chochote kingine ndani ya upinzani. Tumeshazungumza na Kalonzo na Eugene na wamekubaliana nasi,” Haji alisema.
Tayari migogoro hii imeibua hofu ya uasi wa ndani sawa na vurugu za uteuzi ndani ya Azimio kabla ya uchaguzi wa 2022.
Vyanzo vya ndani vinaeleza kuwa kuna wasiwasi miongoni mwa wagombeaji na viongozi wa vyama kuhusu mchakato wa uteuzi wa wagombeaji wa pamoja.
Wengi wanaogopa kuwa wagombeaji maarufu mashinani huenda wakatolewa kafara kwa sababu ya makubaliano ya kisiasa.
Hali hii inafanana na ile ya Azimio ambapo uteuzi wa pamoja ulizua mapambano, kuhama kwa wagombeaji, na mgawanyiko uliodhuru muungano huo.
Viongozi wa upinzani jana walisisitiza uwezekano wa kushirikiana kumkabili Rais Ruto, lakini vyanzo vya ndani vinaonya kuwa udhibiti wa matamanio ya wenyeji wa kila eneo ndio utaamua hatma ya umoja huo.
Walisema watafanya kazi kwa pamoja katika chaguzi ndogo ili kuhakikisha kuwa serikali ya Kenya Kwanza inashindwa.
Viongozi hao walisisitiza kuwa wanatarajia IEBC kutoa ratiba ya wazi kuhusu chaguzi hizo ndogo bila kuchelewa zaidi.
“Tunahitaji IEBC itoe ratiba ya chaguzi hizi ndogo mara moja. Ukitaka kujua kuwa hii ni serikali ya muhula mmoja tu, itakuwa kupitia matokeo ya chaguzi hizi ndogo,” Bw Wamalwa alisema.
Aidha, Wamalwa alisema kuwa muungano huo unajipanga ipasavyo kuelekea uchaguzi wa 2027 na utazindua mgombea wao wa urais mwaka ujao.
“Suala la umoja wetu na ni lini tutamtangaza mgombeaji wetu wa urais ni haki yetu ya msingi. Tutafanya hivyo wakati ufaao, labda mwaka ujao,” alisema.
Walisema pia kuwa wako imara na juhudi zozote za kuwagawanya hazitafanikiwa.
Mwanachama mmoja wa muungano huo wa upinzani alifichua kuwa kamati ya kiufundi ya muungano imepiga hatua muhimu:
“Majina ya muungano yanayopendekezwa tayari yamewasilishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) kuzingatiwa,” alidokeza.
“Timu yetu pia inatengeneza mkakati wa uchaguzi, mpango wa kitaifa utakaowezesha kusimamisha wagombeaji kuanzia kwa urais hadi MCA kote nchini pamoja na manifesto ya mageuzi na inayojali wananchi.”
Aliongeza kuwa wanatengeneza mfumo madhubuti wa kusuluhisha migogoro ili kuepuka makosa ya 2007, 2013, na 2022, pamoja na mpango wa ukusanyaji rasilmali za kuendesha kampeni kwa uendelevu.
Bw Kalonzo Musyoka alisema kuwa wanaunda vuguvugu kubwa la ukombozi kama Narc ya mwaka 2002 ili kumng'oa Rais Ruto mamlakani.
Alisema kuwa muungano huo mpya utafanana na Narc iliyoiangusha KANU katika uchaguzi wa 2002 chini ya hayati Mwai Kibaki, na utarejesha utawala bora, uthabiti wa kiuchumi, na heshima kwa utawala wa sheria ambazo zimedorora chini ya utawala wa Rais Ruto.
from Taifa Leo https://ift.tt/noZJ1B0
via IFTTT