Katika safari yake ya kisiasa, kiongozi wa ODM, Raila Odinga, amekuwa akigeuka kila mara, kuunda na kubadilisha miungano, misemo ya kuvutia ya kisiasa, kauli maarufu, na falsafa mpya zinazoendana na wakati.
Kuanzia ushirikiano wa KANU-NDP mwaka wa 2001, hadi Muungano wa Rainbow mwaka uliofuata, kundi la Pentagon la 2007, serikali ya muungano ya 2008 hadi 2013, Handisheki yake na Rais Uhuru Kenyatta mwaka wa 2018, Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (NADCO) ya 2023 na Rais William Ruto, hadi “kutoa wataalamu kuhudumu katika Baraza la Mawaziri”, na sasa kongamano la vizazi.
Bw Odinga amekuwa na sura nyingi – kila moja ikitokana na mahitaji ya wakati na mazingira ya kisiasa yanayobadilika nchini Kenya.Kutoka kwa usaliti hadi mapatano, juhudi za kura ya maamuzi hadi migawanyiko ya kisiasa, taaluma ya kisiasa ya Bw Odinga ni kama tamthilia ya hadhi ya juu inayofunguka hatua kwa hatua.
Huku miungano ikibadilika na ngome mpya za mamlaka zikiibuka, Bw Odinga ameendelea kubadilika.Awe kama mwanamageuzi na mzalendo, sura nyingi za kisiasa za Bw Odinga zimelenga kudumu katika siasa na tamaa ya mamlaka katika uwanja wa siasa usiotabirika nchini Kenya.
Kuanzia kuzindua vyama, kujenga miungano, kuanzisha vuguvugu hadi kuvunjilia mbali miungano na kuanza mipya, taaluma ya aliyekuwa Waziri Mkuu imekuwa ikiendeshwa na tabia moja kuu: kuzoea kubadilika.
Safari yake imejaa awamu tofauti na misamiati, kwa muktadha wa mageuzi ya kidemokrasia ya Kenya, mara nyingi ikikumbana na matukio muhimu ya taifa.
Katika mahojiano ya hivi karibuni yaliyofanyika nyumbani kwake Karen, Nairobi, na Taifa Leo, kiongozi huyo wa upinzani alitafakari kuhusu nafasi zake za kisiasa zinazobadilika. Hii ni baada ya kutoa wito wa mazungumzo ya kitaifa yanayoshirikisha vizazi tofauti. “Kila awamu ilikuwa muhimu,” alisema.
“Sio kuacha misingi, ni kuutathmini na kuurekebisha kulingana na hali ya wakati huo.”Baada ya kushiriki uchaguzi wa 1997, mabadiliko ya kisiasa ya Bw Odinga yalianza kwa kasi kupitia ushirikiano wa mwaka 2001 kati ya chama tawala cha wakati huo kilichoongozwa na hayati Rais Daniel arap Moi na chama chake cha National Development Party (NDP) ambacho baadaye kilimezwa na KANU.
Ingawa ushirikiano huo ulizua mjadala, ulimfanya Bw Odinga kuingia katika Baraza la Mawaziri kwa mara ya kwanza na kuonja mamlaka ya serikali.
Lakini kufikia mwaka wa 2002, Bw Odinga alijiondoa KANU na kushirikiana na waliokuwa vigogo wa upinzani kama vile Michael Kijana Wamalwa, Charity Ngilu na George Saitoti kuunda Muungano wa Narc, uliomwezesha Mwai Kibaki kushinda urais na kumaliza utawala wa KANU wa miaka 40.
Ndani ya Narc, Bw Odinga alikuwa mwanachama muhimu wa kamati kuu ya uongozi ya muungano huo – Narc Summit.“Jogoo alimeza trekta, lakini injini iliendelea kuwaka. Trekta likafufuka na kuanza kusonga kwa kasi yake,” alisema kwa kejeli katika mojawapo ya mikutano yake ya kisiasa baada ya kutofautiana na Moi.
Lakini hali haikudumu vizuri katika kambi hiyo mpya. Makubaliano ya MoU ya mwaka 2002 ambayo yalitarajiwa kuunda wadhifa wa Waziri Mkuu na kugawana mamlaka yalitupiliwa mbali na upande wa Kibaki – hali iliyozidisha kutoaminiana.
Hali iliendelea kuwa mbaya kiasi kwamba Bw Odinga – aliyesaidia kuwavuta vigogo wa KANU kuingia upinzani – alifungiwa nje ya Ikulu na wandani wa Kibaki.
Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2007, Bw Odinga alizindua kundi maarufu la ODM jopo la uongozi wa kitaifa lililojumuisha yeye mwenyewe, William Ruto (ambaye sasa ni Rais), Musalia Mudavadi, Najib Balala na marehemu Joseph Nyagah – kisha wakajiunga na Charity Ngilu.
Pentagon ilikuwa jaribio la kuonyesha umoja wa kitaifa na kupambana na siasa za kikabila, mkakati ambao karibu ulimfikisha Ikulu kabla ya vurugu kulipuka kufuatia matokeo tata ya uchaguzi.Mnamo 2013, Raila alibadilika tena kwa kuunda muungano wa Cord pamoja na Kalonzo Musyoka (Wiper) na Moses Wetang’ula.
Baada ya Cord kushindwa uchaguzini, Bw Odinga alianzisha kampeni ya kura ya maamuzi kupitia OKOA Kenya, ambayo ilizimwa na uamuzi wa mahakama kuhusu sahihi zilizokusanywa.Mwaka 2017, alizindua NASA muungano mwingine wa kisiasa uliohusisha sura zile zile.
Mnamo Januari 2018, baada ya kuapishwa kihisia kama 'Rais wa Watu' katika Uhuru Park, alichukua hatua isiyotabirika – Handsheki na Rais Uhuru Kenyatta. Maridhiano hayo yalimaliza miezi ya misukosuko na kuzalisha Mpango wa Maridhiano (BBI).
Ingawa mpango huo haukupitia mahakamani, uliibuka kama ishara ya maridhiano, mshikamano wa kitaifa, na makubaliano ya kisiasa ya juu.
“Katika kila mabadiliko, nimekuwa nikilenga kuimarisha taasisi na kukuza demokrasia,” alisema Bw. Odinga kwenye mahojiano ya Karen.Mnamo 2022, Raila alijiunga na Rais Kenyatta kupitia Azimio la Umoja One Kenya, muungano uliolenga kufanikisha safari yake ya kuingia Ikulu – lakini haukufua dafu.
Hata hivyo, anasema hajasalimu amri.Mnamo 2023, alitetea mazungumzo ya pande mbili yaliyosababisha ripoti ya Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (NADCO) – mapatano ya kisiasa kati ya Kenya Kwanza na Azimio yaliyoweka msingi wa mageuzi muhimu.
from Taifa Leo https://ift.tt/sHp6hqw
via IFTTT