UKOSEFU wa ufadhili wa kutosha, kukosa mamlaka ya utekelezaji, na kukosa ushirikiano kutoka mashirika ya udhibiti vimetajwa kuwa vizingiti vikuu vinavyolemaza tume za kikatiba kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Kulingana na ripoti iliyowasilishwa katika Bunge la Kitaifa, tume za kikatiba na ofisi huru zimelemazwa kabisa, na hivyo ripoti zao—pamoja na mapendekezo mazuri—hukosa kutekelezwa na serikali.
Ripoti hiyo ya Kamati ya Uangalizi wa Utekelezaji wa Katiba (CIOC), inayohusisha Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA), Ofisi ya Mdhibiti wa Bajeti, na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, inalenga kuelewa utendakazi na wajibu wa kikatiba wa taasisi hizo.
Ilibainika kuwa mapendekezo mengi ya taasisi hizo hayatiliwi maanani.'Utamaduni wa kudumu wa kukosa ushirikiano unadhoofisha moja kwa moja majukumu ya uangalizi wa tume za kikatiba na ofisi huru,' inasema ripoti hiyo.
Kwa upande wa Ofisi ya Mdhibiti wa Bajeti, ripoti hiyo imebainisha mapungufu ya kisheria, ukosefu wa mbinu za kisheria za kulazimisha utekelezaji wa mapendekezo, na ukosefu wa adhabu kwa wanaokiuka ushauri wake kama changamoto kuu.
Kutokana na mianya ya kisheria, Mdhibiti wa Bajeti hana mamlaka ya kusimamia Hazina ya Ushuru wa Nyumba, ambapo serikali hukusanya takriban Sh63 bilioni kila mwaka.Ripoti hiyo inasema kuwa ushuru huo haupo ndani ya mamlaka ya Mdhibiti wa Bajeti kwa sababu umetajwa kama ushuru; si hazina.
Kuhusu akaunti nyingi za benki zinazotumiwa na serikali za kaunti 31 kinyume na Kanuni za Usimamizi wa Fedha za Umma, ripoti hiyo inasema Mdhibiti wa Bajeti hana mbinu za kisheria za kulazimisha utekelezaji wa sheria au kutoa adhabu kwa wakiukaji.
Hivyo basi, ukiukaji huo unaendelea katika serikali za kaunti.Kuhusu madeni ambayo, hayajalipwa yanayokadiriwa kufikia Sh558 bilioni, kamati hiyo ilibainisha kuwa Mdhibiti wa Bajeti ana mamlaka finyu katika mchakato wa malipo.
"Huku Mdhibiti wa Bajeti akithibitisha na kuhakikisha madeni hayo kuwa halali, mchakato halisi wa malipo hauhusishi ofisi hiyo mara baada ya fedha kutolewa kwa mashirika husika," inasema ripoti hiyo.
Ripoti hiyo pia ilibainisha kuwa Sheria ya Mdhibiti wa Bajeti, inazuia ofisi hiyo kutoa ripoti kuhusu maendeleo ya kiuchumi na utabiri wa mapato—jambo muhimu ambalo ofisi hiyo inapaswa kushughulikia kikamilifu.
Kamati sasa inataka Bunge la Kitaifa kurekebisha Sheria ya Mdhibiti wa Bajeti ili kumpa mamlaka ya utekelezaji, kuondoa vikwazo vya utoaji wa ripoti za kiuchumi, na kuweka adhabu kwa wale wanaokiuka masharti.
Kwa upande wa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, Bunge la Kitaifa limelaumiwa kwa kuchelewesha kupitisha mapendekezo ya sheria ambayo yangeboresha utendakazi wa ofisi hiyo.Ripoti hiyo inataja ukosefu wa uhuru wa kifedha na wa utendaji kuwa matatizo makuu yanayokumba ofisi hiyo katika kutekeleza majukumu yake ya kikatiba.
Kuhusu uhuru wa kifedha, ripoti inasema kuwa kwa sasa, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu hupokea asilimia 0.2 pekee ya bajeti ya kitaifa—kiasi ambacho hakitoshi ikizingatiwa uzito wa kazi ya ofisi hiyo.
[caption id="attachment_166722" align="aligncenter" width="300"]
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kumekuwa na ongezeko kubwa la taasisi zinazokaguliwa kutoka 1,192 katika mwaka wa fedha wa 2016/17 hadi zaidi ya 12,700 katika mwaka wa fedha wa 2023/24, lakini bajeti haijaongezwa.
"Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu inapokea asilimia 0.20 ya bajeti ya kitaifa, jambo linaloathiri uwezo wake wa kutekeleza majukumu yake," inasema ripoti hiyo.Kamati hiyo sasa inataka bajeti ya ofisi hiyo iwe asilimia 0.5 ya mapato ya taifa, kwa kuzingatia hesabu zilizokaguliwa za hivi punde.
Kuhusu kufanikisha uhuru wa utendaji, Bunge la Kitaifa pia limelaumiwa kwa kuchelewesha kupitisha Mswada wa Marekebisho ya Ukaguzi wa Umma wa mwaka 2024, ambao ukipitishwa kuwa sheria, utaruhusu ofisi hiyo kujisimamia kifedha bila kikwazo cha urasimu.
Kwa upande wa Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA), kamati hiyo ilibaini kuwa changamoto kuu ni ukosefu wa bajeti ya kutosha na kukosa mamlaka ya utekelezaji ili kuhakikisha kuwa mapendekezo yake yanatekelezwa.
Kamati hiyo pia inataka Hazina ya Kitaifa iongeze mgao wa bajeti kwa tume hiyo katika mwaka huu mpya wa fedha ili kupanua programu za kujenga uwezo na kuboresha mifumo ya ukusanyaji data.
Tume hiyo, iliyoanzishwa chini ya Kifungu cha 215 cha Katiba, ina jukumu la kuhakikisha kuwa mapato yanagawa kwa haki. Wajibu wake mkuu, kulingana na Katiba, ni kupendekeza msingi wa mgao wa mapato kati ya serikali kuu na serikali za kaunti 47.
from Taifa Leo https://ift.tt/GdQW4It
via IFTTT