Kiini cha masaibu ya wamiliki ardhi ya KMC wakitishiwa kufurushwa

TAKRIBAN familia 5,000 katika eneo la Mavoko, Kaunti ya Machakos, zinakabiliwa na hatari ya kufurushwa kutoka kwa ardhi ya kampuni ya Kenya Meat Commission (KMC), huku maelezo zaidi yakiibuka kuhusu mafadhaiko yao zikisaka ndoto ya kumiliki ardhi. Kiini cha mgogoro huu ni iliyokuwa Manispaa ya Mavoko huku wastaafu na wawekezaji wengine wasiokuwa na hatia wakijipata katikati ya mvutano huu. Kwa mujibu wa hati zilizowasilishwa katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi ya Machakos, mzozo huu ulianza mwaka 1997 baada ya mvua kubwa ya El Niño, ambapo wakazi maskini wa mji wa Athi River walivamia ardhi ambayo haikuwa imestawishwa karibu na kiwanda cha KMC. Wakati huo, uvamizi huo haukuzingatiwa sana kwani KMC ilikuwa imeporomoka tangu 1991. Ingawa KMC ilifufuliwa mwaka 2006 chini ya utawala wa Rais Mwai Kibaki, ardhi hiyo ilibaki bila maendeleo yoyote. Mwaka 2005, wale waliokuwa wakiishi katika ardhi hiyo inayojulikana kama KMC Phase III, wakiwa na hamu ya kumiliki makao mjini, walienda kwa Manispaa ya Mji wa Mavoko kuomba watengewe rasmi ardhi hiyo. Walitaka kurekebisha hali yao na kupatiwa kipande hicho cha ardhi cha ekari 164 (LR No. 10281) huku wakitenga ekari nne kwa ajili ya barabara.Mnamo Mei 7, 2005, Kamati ya Mipango ya Miji na Nyumba ya Mavoko ilikubali ombi hilo, na Agosti 6 2007, barua zilitolewa rasmi. Hati hizo ziliwapa wamiliki ujasiri wa kuuza viwanja kwa wawekezaji wapya. Bw John Mwati, 67, mwalimu mstaafu, aliambia Taifa Dijitali kuwa waliotwaa ardhi hapo awali walijenga vibanda vya muda kabla ya kuuza ploti hali iliyobadilisha Njogu-ini kuwa eneo maarufu la makazi. “Madiwani wa wakati huo walihusika na marafiki wao wa kisiasa walinufaika.” Leo, mtaa huo unakadiriwa kuwa na wakazi wapatao 100,000. Kuna shule tatu za umma, taasisi nyingi za kibinafsi, nyumba za kudumu, nyumba za kupanga, umeme, na mitaro ya maji taka. Mnamo Mei 23, 2018, KMC iliwasilisha ushahidi mahakamani (Kesi 227/2017 mbele ya Jaji Annette Nyukuri) ikieleza kuwa ardhi hiyo ilikuwa chini ya umiliki wa mkataba wa muda kuanzia Julai 1, 1964 kwa kipindi cha miaka 85 na miezi minane. KMC ilieleza kuwa ardhi hiyo ni mali ya kibinafsi.Wakiogopa kufurushwa, mwaka 2017, Bw Kelvin Nzioki na wamiliki wengine 53 waliwasilisha kesi mbele ya Jaji Nyukuri wakitaka kutangazwa kuwa wamiliki halali kwa msingi wa umiliki kwa muda mrefu na kuomba mahakama kutoa amri ya kudumu kuzuia KMC kubomoa nyumba au kuhamisha ardhi hiyo. Ingawa kesi hiyo ya miaka minane iliwapa muda wa kujenga zaidi, pia ilifichua utoaji haramu wa barua na aliyekuwa karani wa mji, Bw Tubman Otieno, chini ya sheria zilizofutwa.Katika uamuzi uliotolewa Julai 10, 2024, Jaji Nyukuri aliamua kuwa karani huyo hakuwahi kuwa na mamlaka ya kisheria kutoa barua hizo. Alitupilia mbali kesi hiyo, akiamuru walalamishi waondoke kwenye ardhi husika ndani ya siku 90 au wafukuzwe kwa nguvu. “Walalamishi, wafanyakazi wao, maajenti wao, wapangaji na ndugu zao waondoke ndani ya siku 90. La sivyo, watafurushwa,” ulisoma uamuzi huo. Kwa uamuzi huo, hali katika eneo hilo ikawa ya wasiwasi, huku wakazi wakiishi kwa hofu kubwa.Mnamo Mei 2025, uongozi wa KMC chini ya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) tangu 2021, ulitoa notisi ya siku 14 kwa wakazi wa ardhi hiyo (LR No. 10281, ekari 164), kuondoka kabla ya Mei 21. Notisi hiyo, ambayo ilipelekwa pia kwa Naibu Kamishna wa Kaunti ya Athi River, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo, na Naibu Msajili wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi ya Machakos, ilizua hofu kubwa kwa wamiliki wa ardhi na wapangaji. Ijumaa, Mei 9, wamiliki watano wa ardhi, kupitia wakili wao Anthony Chege, waliwasilisha ombi maalum mbele ya Jaji Anne Koross. Mahakama iliagiza Serikali ya Kaunti ya Machakos na KMC kujibu ndani ya siku 14. Kesi yao imepangwa kusikizwa Julai 22, 2025. Hakuna amri ya kuzuia kufurushwa iliyotolewa hadi sasa.  

from Taifa Leo https://ift.tt/ZW48orO
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post