Yaibuka vituo vingi vya polisi ni skwota, havina hati miliki

HUDMA ya Kitaifa ya Polisi (NPS) inakabiliwa na hatari kubwa ya kupoteza hadi vituo 44 vya polisi jijini Nairobi kutokana na ukosefu wa hati miliki za ardhi, hali inayozua wasiwasi kuhusu usalama wa mali ya umma na ufanisi wa taasisi za serikali. Kwa mujibu wa ripoti iliyowasilishwa mbele ya Kamati ya Seneti ya Usalama wa Taifa inayoongozwa na Seneta wa Garissa Abdul Haji na Inspekta Jenerali Douglas Kanja, kati ya vituo 64 vya polisi katika jiji la Nairobi, 44 havina hati miliki,  vimejengwa kwenye ardhi iliyotolewa bila usajili rasmi, au bado viko katika mchakato wa kupata umiliki  kisheria. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa tatizo hili limeenea katika kaunti ndogo kadhaa za jiji. Katika Kilimani, vituo vya polisi vya Kileleshwa, Kibra na Sarangombe vimetajwa kuwa na matatizo ya hati miliki. Lang’ata nayo imeorodhesha vituo kama Lang’ata, Hardy, Akila na Bomas ambazo hazina stakabadhi kamili, huku Gigiri ikihusisha vituo vya Loresho, Evergreen, Runda na Gigiri. Dagoretti, Starehe, Kasarani, Makadara, Kayole na Embakasi pia zinakumbwa na changamoto sawa, hali inayodhihirisha kuwa suala hili ni la kitaasisi na si la eneo moja tu. Katika kaunti ndogo ya Starehe, vituo vilivyoorodheshwa ni Ngara, Pangani, Eastleigh North, kituo cha polisi cha anga cha Eastleigh, Kariobangi, Lucky Summer, Utalii, Muthaiga, Korogocho na Drive Inn. Katika kaunti ndogo ya Kasarani, vituo vilivyoathirika ni Githurai 44, Zimmerman, Clay City na kituo cha polisi cha Mwiki. Aidha, katika Makadara, vituo vya Industrial Area, Makongeni, Kaloleni, Hamza, Land Mawe na Bahati navyo vinakosa hati miliki za umiliki wa ardhi. Ripoti hiyo pia imeorodhesha vituo kadhaa katika kaunti ndogo ya Kayole, vikiwemo Kayole, Matopeni, Twiga Patrol Base, Soweto, Masimba, Dandora na Huruma, ambavyo vyote vinakabiliwa na changamoto sawa ya ukosefu wa  hati miliki. Katika eneo la Embakasi, vituo vya Tassia na Mombasa Road vimetajwa kuwa na matatizo hayo, pamoja na Imara Daima na Expressway katika Ruaraka, na kituo cha Kamulu kilichoko Ruai. Katika uchunguzi huo, maseneta pia walitaka kufahamu hatima ya Kituo cha Polisi cha Capitol Hill. Bw Kanja alieleza kuwa ardhi hiyo ilisajiliwa mwaka 2011 kwa jina la Katibu  wa Wizara ya Fedha kama mdhamini wa NPS, lakini baadaye serikali iliidhinisha ihamishwe kwa taasisi nyingine yakiwemo mashirika ya kifedha na huduma za dharura. Hatua hiyo ilisababisha kuanzishwa kwa mchakato wa kufuta usajili kituo hicho cha polisi. Hata hivyo, aliwahakikishia maseneta kuwa huduma za usalama hazitaathirika kwani zitahamishiwa vituo vya karibu kama Kilimani, na Golf Course. Tatizo hili si jipya. Ripoti za awali za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, zimeonya mara kwa mara kuwa takriban asilimia 80 ya ardhi inayomilikiwa au kutumiwa na polisi haina hati miliki. Kati ya zaidi ya mashamba 3,000 yanayohusishwa na huduma hiyo, ni 464 pekee yaliyo na stakabadhi kamili za umiliki. Hali hii imeibua maswali makubwa kuhusu usimamizi wa mali ya umma na uratibu kati ya taasisi za serikali, hasa Wizara ya Fedha ambayo inashikilia baadhi ya hati hizo bila uwazi wa kutosha. Ukosefu wa hati miliki umechangia kuibuka kwa migogoro ya umiliki wa ardhi, hasa kwa maeneo yaliyotolewa na jamii kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya polisi bila kufuata taratibu rasmi za kisheria. Katika baadhi ya matukio, ardhi hiyo imeanza kudaiwa upya na wamiliki wa awali au warithi wao. Hatari ya hali hii tayari imeanza kuonekana. Huko Kisii, kituo cha polisi kililazimika kuhamishwa kutoka katikati ya mji baada ya kubainika kuwa kilijengwa kwenye ardhi ya kibinafsi iliyodaiwa tena na familia iliyoitoa hapo awali. Migogoro kama hiyo pia imeripotiwa katika maeneo ya Kiambu, ikiwa ni pamoja na Gatundu North na Makongeni, ambapo watu binafsi na makundi yamejitokeza kudai umiliki wa ardhi inayotumiwa na polisi. Mwanauchumi na mwanaharakati Fred Ogola anaonya kuwa hali hii inaacha ardhi ya polisi katika hatari kubwa ya kunyakuliwa. Anasema mtu yeyote mwenye ufahamu wa mfumo wa usajili wa ardhi anaweza kubaini maeneo yasiyo na hati na kuyasajili chini ya maji kwa jina lake, kisha kudai fidia kutoka serikalini. “Ni vigumu kutekeleza sheria kwenye ardhi ambayo huimiliki. Kimsingi, unakuwa kama mkazi haramu lakini unadai kusimamia sheria,” alisema, akionya kuwa hali hiyo inaweza kugeuka kuwa biashara ambapo watu wanatafuta mianya ya kujinufaisha.

from Taifa Leo https://ift.tt/Ly5hSbI
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post