
MGOMBEA urais wa chama cha Jubilee, Fred Matiang'i, ametoa onyo kali kwa serikali akitaka kukomeshwa kwa siasa za vurugu na matumizi ya makundi ya wahuni, akisema hali hiyo inaweza kutumbukiza nchi katika machafuko yasiyodhibitika. Akizungumza katika Kaunti ya Nyamira, Dkt Matiang’i alionya kuwa baadhi ya viongozi wanaohusishwa na serikali wanashangilia utamaduni wa kutojali sheria, hali aliyotaja kuwa hatari kwa mustakabali wa taifa. Alisisitiza kuwa siasa hazipaswi kuwa sababu ya watu kuuawa au kujeruhiwa. Akimlenga Rais William Ruto na Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen, Dkt Matiang’i alisema serikali inapaswa kudhibiti hali kabla mambo hayajaharibika zaidi. “Simamieni kazi yenu na mhakikishe kuna amani. Msifikishe nchi mahali ambapo hamtaweza kuidhibiti. Mkisukuma watu hadi ukingoni, huwezi kujua watakayofanya,” alisema, akitumia tajriba yake kama aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani. Alibainisha kuwa tangu mwaka 2024, wananchi wamechoma vituo 13 vya polisi kutokana na hasira, akionya kuwa hiyo ni ishara ya hali inayoweza kuzorota zaidi ikiwa haitadhibitiwa mapema. Pia, alidai kuwa baadhi ya wanasiasa wanaruhusiwa kuajiri wahuni na hata kulindwa kwa sababu ya ukaribu wao na serikali. Dkt Matiang’i alisisitiza kuwa sheria inafaa kuwahusu wote bila ubaguzi—walioko serikalini na walioko upinzani. Hata hivyo, alionya kuwa uvumilivu una mipaka. “Tutaendelea kufuata sheria hadi kiwango fulani. Lakini ikiwa siasa zitageuzwa kuwa za vurugu, mtatuachia chaguo gani?” alihoji. Alihoji pia matumizi ya waendeshaji boda boda katika siasa za vurugu, akisema biashara hiyo ni halali na haipaswi kuchafuliwa kwa matumizi ya kisiasa. “Haiwezekani kutumia vijana wa boda boda kueneza vurugu. Hilo halikubaliki,” alionya. Alisisitiza umuhimu wa kulinda umoja wa taifa akisema tofauti za kisiasa hazipaswi kuhatarisha mshikamano wa nchi. “Tutakubaliana na kutokubaliana kisiasa, lakini Kenya lazima ibaki salama,” aliongeza. Alitoa kauli hizo wakati wa mkutano na wagombea wa Jubilee kutoka maeneo ya Kisii, Nyamira na Kuria, ambapo aliwahimiza kuendesha kampeni za amani na kuepuka uchochezi. Matamshi hayo yanajiri huku visa vya vurugu za kisiasa vikiongezeka nchini. Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja alisema serikali tayari imewatambua wanaofadhili na kuandaa makundi ya wahuni wanaovuruga mikutano ya kisiasa. “Uhuni huu utakoma, nawahakikishia,” alisema mbele ya Kamati ya Seneti ya Usalama wa Taifa. Ripoti pia zinaonyesha kuwa ushindani mkali wa kisiasa katika baadhi ya maeneo umechangia mashambulizi, ikiwemo kurushia mawe misafara ya viongozi na matumizi ya makundi ya vijana kwa vitisho. Kwa upande wake, Bw Kipchumba Murkomen alikiri kuwa baadhi ya wanasiasa wanachunguzwa kwa tuhuma za kufadhili makundi ya wahuni. Alisema uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya viongozi wanatumia makundi hayo kama sehemu ya vikosi vyao vya usalama ili kuwatisha wapinzani wao.
from Taifa Leo https://ift.tt/gcoeH2S
via
IFTTT