
RAIS William Ruto jana aliwaomba wapiga kura wa Mlima Kenya wasimwondoe madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa 2027, badala yake wamuunge mkono kwa muhula wa pili akisema ametekeleza ahadi alizotoa kabla ya uchaguzi wa 2022. Akizungumza akiwa katika ziara yake ya Kaunti ya Murang’a, Rais Ruto aliwataka wananchi wa eneo hilo kukumbuka mchango wake wa muda mrefu, akisema amekuwa akijihusisha na shughuli za kijamii ikiwemo ujenzi wa makanisa na ziara za mara kwa mara kwa zaidi ya miaka 20, jambo linalomfanya kuwa rafiki wa eneo hilo. “Niliwajia mwaka 2022, nikawaahidi huduma na ninaendelea kutekeleza. Msisikilize wanaonitukana na kuwachochea dhidi yangu. Mimi ni chaguo lenu bora,” alisema akiwa katika ziara ya siku mbili katika maeneo bunge ya Mathioya, Kiharu na Gatanga. Alisema anatambua changamoto ndogo zilizojitokeza lakini ataendelea kurejea eneo hilo mara kwa mara ili kuhakikisha umoja unapatikana. Katika ziara hiyo, Rais Ruto alizindua na kukagua miradi mbalimbali ikiwemo barabara ya Kiriko-Kagumo-ini-Gitugi-Karugia, mabweni katika vyuo vya kiufundi Kiharu, maabara ya Jitume ICT, mradi wa makazi nafuu Murang’a, pamoja na ukaguzi wa uwanja wa Mumbi na soko la Kayole. Katika Gatanga alikagua mradi wa nyumba za nafuu wa Del Monte na upanuzi wa Hospitali ya Kenneth Matiba, kabla ya kuelekea Kandara kuweka jiwe la msingi mradi wa nyumba za nafuu. Ruto alisema sekta za kilimo, afya na ujenzi zimeimarika chini ya serikali yake, akidai bei ya kahawa imepanda kutoka chini ya Sh60 hadi zaidi ya Sh110 kwa kilo. Aliongeza kuwa serikali yake imeboresha elimu, umeme, maji na mazingira ya biashara. Hata hivyo, alitumia fursa hiyo kuwashambulia wapinzani wake akisema wanatumia matusi na uchochezi badala ya kuonyesha mchango wao kwa wananchi. Akisindikizwa na Naibu Rais Prof Kithure Kindiki na viongozi wa UDA, baadhi ya washirika wake walitoa kauli kali kuhusu siasa za 2027, wakisisitiza kuwa Mlima Kenya utaendelea kumuunga mkono Rais Ruto. Waziri wa Ardhi Alice Wahome alisema eneo hilo halitakuwa na mgombea mwingine wa urais isipokuwa Ruto, huku Prof Kindiki akiwataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais kwa sababu ya maendeleo. Hata hivyo, viongozi wa upinzani wakiongozwa na DCP ya Rigathi Gachagua wamesema watahakikisha Ruto anaondoka madarakani kupitia kura katika uchaguzi mkuu wa 2027. Wabunge wa eneo hilo nao wamegawanyika, huku baadhi wakiwa bado hawajatangaza msimamo wao. Seneta wa Murang’a Joe Nyutu alisema hatahudhuria ziara hiyo akidai hakuna miradi halisi inayoshughulikiwa, akisema ziara hizo ni za kampeni zaidi kuliko maendeleo.
from Taifa Leo https://ift.tt/CwMYQA1
via
IFTTT