Mackenzie ‘arekebisha’ orodha ya mashahidi, aondoa Padri na Shekhe

MHUBIRI Paul Mackenzie amebadilisha mkakati wake wa kujitetea dhidi ya mashtaka ya mauaji ya Shakahola, akitangaza wazi kwamba atategemea ushahidi wa wataalamu kutoka nyanja zisizo za theolojia ya Kikristo.

Alhamisi asubuhi, Mackenzie aliieleza Mahakama Kuu kwamba upande wa utetezi hautamrejelea tena kama padri wa Kanisa Katoliki, na kwamba atafunga utetezi wake kwa mashahidi watatu wa kitaalamu kutoka nyanja nyingine.

“Kwa sababu ambazo haziwezi kuepukwa, tumerekebisha orodha ya mashahidi na hatutamleta padri wa Katoliki kama vile marekebisho hayo yametufikia,” alisema Mackenzie kupitia wakili wake Lawrence Obonyo.

Wakili huyo alifafanua kwamba kulikuwa na mkanganyiko katika rekodi ya mashahidi waliokuwa wametajwa awali, na hivyo orodha ikarekebishwa kubaki na Dkt Evelyn Asaala wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Mtaalamu wa Sayansi Dkt Myrna Kalsi, na Dkt Rashid Ali Omar.

Aliongeza kuwa padri Felix Atindah hatashirikishwa wala kuwa mmoja ya wale watakaofika Mahakamani kutoa maoni ya kitaalamu kuhusu masuala ya dini.

Mackenzie na washirika wake 30 wanajitetea dhidi ya mashtaka yanayotokana na vifo vilivyotokea katika msitu wa Shakahola, vinavyohusishwa na shughuli za Kanisa lake la Good News International.

Zaidi ya wafuasi 450 wa kanisa hilo walikufa katika mfungo wa kwenda kumuona Yesu kati ya 2020 na 2023 katika msitu huo.

Washirika sita tayari wametoa ushahidi wa utetezi, wakidai Mackenzie hakutoa amri ya moja kwa moja kwa mtu yeyote kufunga hadi kufa.

Alhamisi, wanandoa walitumia kikao cha mahakama kuomba msamaha kwa jukumu lao katika vifo vya watoto wao sita waliokufa kwa kufunga.

Ann Anyoso alikiri kuhusika, akimsamehe na kumwomba msamaha mumewe, Enos Amanya Ngala, ambaye sasa ni shahidi wa upande wa mashtaka.

Hata hivyo, alihusisha mkasa huo na imani ambayo watoto wao walikumbatia kufuatia mahubiri ya Mackenzie.

Kauli yake ilikuwa msamaha na pia hakikisho kwamba watoto wao wako na Yesu.

“Mume wangu aliniomba msamaha,hata mimi leo namuomba msamaha. Hakufanya kosa lolote. Namuakikishia kuwa watoto wetu wako salama na Yesu," Anyoso alisema bila kufafanua alivyopata habari hiyo.

Amanya amefanya makubaliano na serikali kwa kukiri mashtaka yote 191 ya mauaji na anasubiri hukumu.

Awali, alimwomba mkewe msamaha baada ya kumlaumu na Mackenzie kwa vifo hivyo.

Wakati Amanya alikiri kosa, Anyoso alisisitiza kuwa hana hatia.

Amanya ndiye alikuwa wa kwanza kuomba msamaha, akikiri yaliyotokea msituni.

Baadaye Anyoso alitoa msamaha wake hadharani kama ishara ya maridhiano kwa familia hiyo.

Wawili hao pia wamemuomba msamahama mtoto wao, Veronica Israel ambaye ndiye pekee alinusurika katika kifungo hicho baada ya kutoroka.

Anyoso alitoa ushahidi kama mmoja wa mashahidi wa Mackenzie.

Awali, alimkosoa mumewe kabla ya kukiri kwamba yeye ndiye aliyesababisha vifo vya watoto wao sita.

“Kwa kusema ukweli, Amanya hakuhusika na vifo vya watoto wetu. Ni mimi nilikuwa na hao watoto na nikawaona wakifa moja baada ya mwengine," alisema Anyoso.

Alieleza kuwa Amanya mara nyingi alikuwa mbali, akirudi tu kula, kuchukua chakula au kuwazika watoto.

Alisema kuwa Baada ya kukosana na mumewe, aliishi kando na ndugu yake David Amanya katika mojawapo wa vijiji vya Mackenzie kule Shakahola.

Anyoso alisema alimripoti mumewe kwa Mackenzie kwa kosa la kutelekezwa na akahamia karibu na mhubiri huyo.

Alidai Amanya alimjengea nyumba dhaifu iliyokaribia kuanguka.

Alikiri kushuhudia watoto wake wakifunga hadi kufa, akidai walifanya hivyo kwa hiari baada ya ndoto, wakishawishiwa na imani.

“Walipokea ndoto na kisha wakafunga hadi kufa. Nilishuhudia wakikonda mmoja baada ya mwingine,” alisema.

Alikubali kwamba watoto wako chini ya malezi ya wazazi, lakini alisisitiza hakuweza kuingilia imani yao.

Pia, Anyoso alifichua kwamba watoto wake walichimba makaburi yao wenyewe wakijiandaa kwa kifo.

"Walichimba makaburi huku wakijipima ndani kama ishara ya kujiandaa kufa Kwa kufunga," alisema.

Alieleza kuwa Mackenzie hakutoa amri ya moja kwa moja ya kufunga, bali aliwahimiza wafuasi kuachana na uchawi.

Kabla ya kujiunga na kanisa hilo mwaka 2019, wanandoa hao waliishi vizuri Nairobi, wakifanya biashara ya taka na kusomesha watoto wao.

Kuhusu kuwatoa watoto shule, alisema kuwa mtoto wake alikataa ushoga lakini hatimaye alikiri kwamba hawakufurahia masomo.

“Nilifika kidato cha nne lakini nilisukumwa tu kusoma. Watoto wangu wanaonekana walifuata mkondo huo huo,” alisema, Mackenzie na kundi lake wanakamilisha utetezi wao wiki hii.



from Taifa Leo https://ift.tt/tyJakub
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post