
KIONGOZI wa Wiper Patriotic Front Kalonzo Musyoka ameongeza kasi ya kampeni zake katika eneo la Ukambani kwa kuwahimiza wakazi kujitokeza kwa wingi kujisajili kama wapiga kura, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha nafasi yake ya kumenyana na Rais William Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Akizungumza mjini Kitui wakati wa ziara ya siku ya pili ya viongozi wa muungano wa upinzani, Bw Musyoka alionyesha kujiamini kuwa ana uwezo wa kupeperusha bendera ya urais kwa niaba ya upinzani, akijitambulisha kama kiongozi mwenye historia ya kusaidia serikali zilizopita kuingia mamlakani.
“Mnajua namna tumekuwa tukiwasaidia wengine kwa miaka mingi, kuanzia kwa Mwai Kibaki hadi Raila Odinga. Hata nilimsaidia Rais Ruto alipokuwa akikabiliwa na kesi katika Mahakama ya Kimataifa Kuhusu Uhalifu( ICC). Sasa ni wakati wa kuleta urais nyumbani,” alisema huku akihimiza wakazi kujisajili kwa wingi.
Aliongeza kuwa ushindi wake hautakuwa rahisi, akisisitiza kuwa kura ndizo msingi wa mafanikio ya kisiasa.
“Wakenya wamechoka na siasa za mabavu. Wanataka nchi inayoongozwa kwa katiba na utawala wa sheria,” alisema.
Ziara hiyo pia iliwapa nafasi viongozi wengine wa upinzani kumshambulia Rais Ruto, wakimlaumu kwa kile walichodai ni uongozi mbovu na sera zinazowaumiza wananchi.
Bw Musyoka alisema kuwa upinzani unafikiria kumpeleka Rais katika ICC kwa madai ya ukiukaji wa haki za binadamu.
“Wewe Bw Rais, tutakurudisha ICC usipoacha siasa za mabavu,” alisema.
Hata hivyo, takwimu za usajili wa wapiga kura zinaonyesha bado kuna kazi kubwa.
Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), eneo la Ukambani limesajili wapiga kura wapya takriban 110,000 tangu kuanza kwa zoezi mwezi Machi.
Kaunti ya Machakos inaongoza kwa usajili wa wapiga kura wapya 47,000, ikifuatiwa na Kitui (37,000) na Makueni (25,000). Viongozi wa eneo hilo wanasema idadi hiyo bado iko chini ya matarajio.
Gavana wa Kitui Julius Malombe alisema Ukambani inahitaji angalau kura milioni nne ili kuhakikisha Bw Musyoka anaingia Ikulu.
“Kura ndizo zitakazomfikisha Ikulu. Lazima tuongeze juhudi za usajili,” alisema.
Kiongozi wa Democracy for the Citizens Party, Bw Rigathi Gachagua, alionya kuwa viongozi wanaomuunga mkono Rais Ruto Ukambani wanadhoofisha juhudi za Bw Musyoka.
Alisema ni jambo la kushangaza kuwa wabunge zaidi ya tisa kutoka eneo hilo wanaunga mkono serikali, hali anayosema inahitaji kubadilishwa haraka.
“Namhurumia Kalonzo. Amezungukwa na viongozi wasio waaminifu. Ikiwa mnamtaka afaulu, lazima mchague viongozi wanaomuunga mkono kikamilifu,” alisema.
Hata hivyo, Bw Musyoka alichukua msimamo wa upatanishi, akimtaka mbunge wa Kitui Kusini, Bi Rachael Nyamai kujiunga na upinzani badala ya kuendelea kushirikiana na serikali.
Ziara hiyo, iliyojumuisha mikutano katika maeneo ya Chuluni, Kisasi, Ikanga, Kyatune, Mutomo, Ikutha na Muangeni, imeonyesha wazi kuwa vita vya kisiasa kuelekea 2027 vinaanza kushika kasi, huku usajili wa wapiga kura ukiwa kiini cha mikakati ya vyama vya siasa.
from Taifa Leo https://ift.tt/PEGTqkb
via IFTTT