Mshangao Mackenzie akiorodhesha wahadhiri, Padri na Shekhe kumtetea kortini

MHUBIRI tata Paul Mackenzie atawaita wahadhiri wa vyuo vikuu, padri wa Kanisa Katoliki, shehe wa dini ya Kiislamu na mwanasaikolojia ili kusaidia utetezi wake dhidi ya mashtaka ya kuua watoto 191 katika msitu wa Shakahola.

Jumatatu, mhubiri huyo tata aliambia mahakama kwamba ananuia kuwaita Dkt Evelyn Asaala kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, Dkt Myrna Kalsi na Bw Nelson Sitonik.

Aidha, amejumuisha viongozi wa kidini akisema atawaita Padri Felix Atindah wa Kanisa Katoliki na shehe wa Kiislamu ambaye bado hajatajwa.

“Tunakusudia kuwaita mashahidi hawa wa kitaalamu pamoja na wengine sita walioko miongoni mwa washtakiwa. Tutawasilisha maoni yao ya kitaalamu kwa upande wa mashtaka ili waweze kujiandaa,” Mackenzie alisema kupitia wakili wake.

Upande wa utetezi unatarajia ushahidi wao utapinga madai ya upande wa mashtaka na kutoa fasiri mbadala kuhusu matukio ya vifo vya halaiki katika msitu wa Shakahola.

Jumatatu, washirika wa Mackenzie walipanda kizimbani kumtetea lakini wakajikuta wakisaidia upande wa mashtaka.

Licha ya kukanusha kwamba mhubiri aliwaamuru wafuasi kufunga hadi kufa, walikiri kwamba Mackenzie aliwahi kusema chakula ni dhambi.

Steven Sanga Muye, anayejulikana pia kama Steve wa Mtwapa, alithibitisha kwamba Mackenzie ndiye alikuwa kiongozi wa Kanisa la Good News International (GNI), ambalo zaidi ya wafuasi wake 450 walifariki kwa njaa msituni Shakahola kati ya mwaka wa 2020 na 2023.

“Washtakiwa wote tulikuwa wakazi wa Shakahola. Awali, tulikuwa tukiishi kwa amani msituni,” alisema.

Alieleza jinsi alivyohama Mtwapa, alikohudhuria Kanisa la Ebenezer, na kujiunga na GNI.

Kwa mujibu wake, janga la Covid-19 lilisababisha matatizo ya kifedha na ndipo wazo la Shakahola lilipoibuka. Alihama kutoka Mtwapa hadi Malindi na baadaye akakaa msituni.

Kulingana na Bw Sanga, kwenda kwake msitu wa Shakahola kulikuwa kwa hiari.

“Nilipofika Shakahola, nilikodisha shamba kwa Sh1,000. Nilifanya kazi ya ulinzi ili kuzuia wanyama kunywa maji ya mabwawa, kwa kuwa eneo hilo liko karibu na Hifadhi ya Kitaifa ya Tsavo,” alisema.

Alikiri kwamba walikuwa wakifunga mara kwa mara ili kupata hukumu nzuri mbinguni. Alisema maagizo ya kufunga na shughuli nyingine za kidini yalitokana na Roho Mtakatifu.

“Roho Mtakatifu hunena kupitia ndoto na maono. Hivyo ndivyo maagizo yalivyotolewa msituni. Hatukupokea amri kutoka kwa Mackenzie za kufunga,” alisema.

Mark Kiogora Kiara alitoa ushahidi kwamba aliingia msituni mwaka 2020 na kulipa Sh5,000 kwa ekari mbili za ardhi.

Alidai kwamba chifu wa eneo hilo aliwaelekeza wanunuzi kumpa Mackenzie pesa kwa ajili ya wazee wa Wabaya Mwaro.

“Wakati wa mkutano wa kwanza na chifu, alituambia tuandike majina na namba za vitambulisho na tumkabidhi Evans Sirya,” alisema.

Sirya ni miongoni mwa washtakiwa.

Kiara alithibitisha kwamba aliishi Shakahola na hata kuoa mke wake huko.

Alisema alihama baada ya kanisa la Mackenzie kufungwa, ambapo mhubiri aliwaambia kufungwa huko kulimaanisha kukamilika kwa huduma yake.

Alieleza tukio la Septemba 2022, miezi michache kabla ya kugunduliwa kwa makaburi ya halaiki, ambapo kulikuwa na jaribio la kuwafukuza wakazi wa Shakahola.

Walipinga, wakidai fidia kwa uwekezaji wao, lakini hawakulipwa.

Kiara alisema yeye na mke wake hawakufunga. Alithibitisha kwamba mikutano ilifanyika chini ya miti ya Mitola msituni, lakini ilikuwa ya kujadili changamoto za wakazi.

“Ndoto na maono yalishirikiwa kama jambo la pembeni; hayakuwa ajenda kuu,” alisema.

Alikiri kwamba vifo vilitokea msituni na mazishi yalifanywa bila majeneza, lakini alikanusha kuhudhuria mazishi yoyote wala kushuhudia kifo cha mtu yeyote.

“Sikufunga. Mke wangu na mtoto wangu wako hai; hawakufa,” aliongeza Kiara, ambaye alisema alikuwa Mwadventista kabla ya kujiunga na kanisa la Mackenzie mwaka 2019.

Alithibitisha kwamba baadhi ya wafuasi walidai kupokea maono ya kufunga ili kumuona Yesu, na wakatekeleza.

Hata hivyo, ushahidi wa Lucas Owino Ogola uliunga mkono upande wa mashtaka.

Ogola, fundi wa cherehani kutoka Gem, Kaunti ya Siaya, alieleza jinsi alivyohama kutoka Legio Maria na kujiunga na mafundisho ya Mackenzie.

Alisema alihamia Shakahola mwaka 2019, ambapo watu walilazimishwa kufunga hadi kufa na Musa Makelele, kwa maagizo ya mwanamke asiyejulikana.

Alidai mwanamke huyo alitoa amri ya kufunga katika mkutano uliohudhuriwa na Mackenzie na wafuasi wake.

“Nilikataa kufunga hadi kufa, na kwa hilo nilipigwa na wanaume ambao hawapo mahakamani,” alisema.

Ogola alithibitisha kwamba Mackenzie alipinga elimu, akiiita uovu na kudai kwamba inaleta roho ya mpinga Kristo.

Ushuhuda wake uliimarisha hoja ya upande wa mashtaka kuhusu udanganyifu wa kimfumo na mateso ndani ya makazi ya msituni.

Ogola alitoa ushahidi kwamba Mackenzie alisisitiza kukosa kufunga ni dhambi, na kudai kwamba maono kutoka kwa mwanamke aliyefariki yalionyesha kula ni dhambi.

Aliongeza kwamba kulikuwa na kundi lililolazimisha watu kufunga hadi kufa, wakidai maono kutoka kwa mwanamke huyo.

“Nililazimishwa kufunga kinyume na matakwa yangu. Kwa kupinga amri hiyo, nilihesabiwa msaliti, lakini sikukubali,” alisema.

Ogola alishuhudia kwamba alijua watoto walikuwa wakifunga na kufa msituni, lakini hakuripoti kwa polisi.

“Watoto hawakuwa na haki ya kuamua kufunga, lakini niliacha kila mtu abebe msalaba wake,” alisema.

Ushuhuda wake wa kupigwa kwa kukataa kufunga ulionyesha kulazimishwa na ukosefu wa uvumilivu ndani ya kundi hilo, jambo ambalo upande wa mashtaka umekuwa ukisisitiza.

Ogola aliongeza kwamba Mackenzie hakupinga amri ya mwanamke kwamba chakula ni dhambi, bali aliwaambia wafuasi kufuata sauti ya kwanza.

“Mackenzie hakupinga wito wa kufunga hadi kufa; badala yake aliwahimiza wafuasi kutii,” alisema.

Alikumbuka tukio ambapo wanaume waliokuwa kwenye pikipiki walimtafuta rafiki yake Daniel Makori, wakimtuhumu kwa usaliti kwa kupinga kufunga.

Mashahidi hao watatu ni miongoni mwa 12 ambao Mackenzie ameamua kuwaita katika utetezi wake.



from Taifa Leo https://ift.tt/0NRB2zc
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post