KUUNDWA upya kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumefungua njia kwa uchaguzi mdogo kujaza viti 22 ambao unaweza kubadilisha kabisa taswira ya siasa za Kenya, na kuwa mtihani muhimu kwa mapambano ya ubabe kati ya Rais William Ruto na aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua na hata kiongozi wa ODM Raila Odinga. Mwenyekiti mpya wa IEBC, Bw Erastus Ethekon, aliambia Taifa Leo Jumatano kwamba tume hiyo inaelewa kikamilifu masuala yote yaliyosalia, ikiwa ni pamoja na uchaguzi huo mdogo. “Tutatoa taarifa ya kina kuhusu masuala yote yanayosubiriwa kwa wakati ufaao,” alisema Bw Ethekon alipoulizwa kuhusu tarehe ya uchaguzi huo, ambao umeacha maeneo mbali mbali bila wawakilishi. Uchaguzi huo mdogo unatazamiwa kuwa uwanja wa mapambano ya kisiasa ambapo Rais Ruto na Bw Odinga kwa upande mmoja, na upinzani unaongozwa na Bw Gachagua, pamoja na kizazi kipya cha Gen Z, wote watapimana nguvu. Mbali na majina ya vigogo wa kawaida katika siasa, Gen Z wanaonekana kuwa nguvu mpya na wanaweza kuathiri pakubwa mwelekeo wa kisiasa. Sasa IEBC imewezeshwa kisheria kuendesha uchaguzi mdogo uliotokana na vifo vya viongozi waliokuwa madarakani, maamuzi ya mahakama na uteuzi wa wabunge wawili kuwa mawaziri. Tangu Januari 2023, IEBC haikuwa na makamishna, lakini sasa imekamilika kikamilifu baada ya kuapishwa kwa Mwenyekiti Ethekon na makamishna sita wapya: Ann Njeri Nderitu, Moses Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor, Francis Odhiambo na Fahima Abdallah. IEBC tayari imepokea arifa rasmi kutoka kwa Maspika wa Bunge na Mabunge ya Kaunti kuhusu viti 22 vilivyo wazi — sita vya ubunge, moja cha useneta, na 15 vya MCA. Miongoni mwa viti vinavyovutia zaidi ni cha Useneta kaunti ya Baringo, kilichobaki wazi baada ya kifo cha William Cheptumo (UDA) Februari, na cha ubunge cha Banissa baada ya Mbunge Hassan Kullow (UDM) kufariki katika ajali ya barabarani. Uchaguzi mdogo pia utafanyika maeneo bunge ya Malava na Magarini baada ya kifo na kubatilishwa kwa uchaguzi wa awali na Mahakama ya Juu. Kiti cha Ugunja kilibaki wazi baada ya Opiyo Wandayi (ODM) kuteuliwa kuwa Waziri wa Kawi na Petroli, huku Geoffrey Ruku (DP) wa Mbeere Kaskazini akiteuliwa Waziri wa Huduma za Umma. Hata hivyo, changamoto ya kifedha imekumba IEBC, ambayo ilipewa bajeti ya Sh788 milioni kufanikisha uchaguzi katika maeneo 16. Kwa sasa, inahitaji Sh 215 milioni zaidi kugharamia uchaguzi katika maeneo mengine, akiwemo Kasipul ambako Mbunge Charles Ong’ondo Were aliuawa Aprili 30. Kwa wachambuzi wa siasa, uchaguzi mndogo unaotarajiwa si wa kikatiba pekee, bali ni mtihani wa mapema wa uchaguzi mkuu wa 2027. Katika Mbeere Kaskazini, wachambuzi wanasema UDA italazimika kutumia nguvu nyingi kutwaa kiti hicho ambacho awali kilikuwa cha DP. Hata hivyo, DCP ya Gachagua inapania kushinda kwa mara ya kwanza huko Mlima Kenya. Seneta wa Kitui Enoch Wambua wa chama cha Wiper anasema:“Chaguzi hizi ni mtihani mkubwa kwa Rais Ruto. Itamlazimu afanye kazi ya ziada ili kushinda hata kiti kimoja.” Naibu Gavana wa Machakos, Francis Mwangangi, alisema: “Iwapo mgombeaji wa Rais atashindwa, itakuwa ishara ya kushuka kwa umaarufu wake kuelekea 2027.” Kwa upande mwingine, baadhi ya viongozi kama Oburu Oginga wamependekeza ushirikiano kati ya ODM na UDA katika baadhi ya maeneo katika ngome za vyama hivyo. Hata hivyo, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna amekana uwepo wa makubaliano rasmi na kusema chama hicho kitapigania kila kiti. ODM imepanga mkutano mkuu wa wajumbe wa kitaifa (NDC) Oktoba 2025 kujiandaa kwa uchaguzi wa 2027 na kusherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwake. Katika upande wa upinzani, muungano mpya unaoongozwa na Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka (Wiper), Martha Karua (PLP), Eugene Wamalwa (DAP-K), na Fred Matiang’i, unatarajiwa kuwania viti kwa nguvu hususan Mbeere Kaskazini, Malava na Magarini. Majina kama aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga na Seneta wa Busia Okiya Omtatah pia yanatajwa kama wanasiasa wanaoweza kutumia uchaguzi huu kujipima nguvu kabla ya 2027. Katika Kasipul, Moses Omondi K’Oyoo wa chama kipya cha National Liberal Party atakabiliana na Boyd Were (ODM) mwana wa mbunge aliyeuawa pamoja na wagombeaji wengine. Katika Banissa, UDA na UDM zote zimeweka wagombeaji. Lakini wazee wa koo wamekubaliana kumteua Ahmed Maalim Hassan ‘Barre’ ndugu wa marehemu mbunge kwa tikiti ya UDM. Mbunge wa Embakasi Kati Benjamin Gathiru ‘Mejjadonk’, mshirika wa karibu wa Gachagua, alisema:“Huu ni mtihani wa umaarufu kwa UDA. Kuna maeneo watu wanahisi UDA imekufa. Huu ni wakati wa wananchi kueleza hisia zao.” Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa aliongeza:“Chaguzi hizi ndogo zitatuonyesha maeneo ambayo tumepoteza au tumeshinda. Tutahitaji wagombeaji thabiti.” Naibu Gavana wa Kakamega Ayub Savula alitabiri kuwa Malava itakuwa changamoto kwa UDA na ODM kwa sababu marehemu Injendi alikuwa wa chama cha ANC kilichovunjwa kujiunga na UDA. Huku kengele ya IEBC ikikaribia kupigwa, pande zote za kisiasa zinajiandaa, na chaguzi hizi zinaweza kutoa ishara za mapema kuhusu hali itakavyokuwa 2027 . Profesa Macharia Munene wa chuo kikuu cha Kimataifa cha Amerika (USIU) anasema “kwa kuwa Gen Z bado hawajaandikishwa kwa wingi, ni mapema kusema kuwa wataathiri sana uchaguzi huu. Huu pia ni mtihani kwa tume mpya ya IEBC kuonyesha uwezo wao.” Mchambuzi Martin Oloo anakubaliana naye akisema:“Kila upande wa kisiasa utatupa karata yake. Muungano wa Kenya Kwanza/ODM utalinda nafasi zake, huku upinzani ukijaribu kuonyesha mshikamano na mikakati mipya. Vitakuwa vita vikali vya kisiasa.”
from Taifa Leo https://ift.tt/QuKeSHW
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS