TANGU kuibuka kwa maandamano yanayoongozwa na kizazi cha Gen Z dhidi ya serikali mnamo Juni 2024, serikali ya Rais William Ruto imegeukia kile ambacho wanaharakati wa haki za binadamu wanasema ni mbinu za kimabavu za kuhusisha upinzani na ugaidi.
Makundi ya haki za binadamu na wataalamu wa sheria wanaonya kwamba hatua za serikali dhidi ya maandamano ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa ya amani, ni sehemu ya mtindo unaoenea Afrika Mashariki, ambapo serikali hutumia sheria za kupambana na ugaidi kukandamiza upinzani na mashirika ya kutetea haki.
Kuanzia Uganda, Ethiopia, Sudan Kusini hadi Tanzania, ugaidi unatumiwa kuzima maandamano na wachanganuzi wanasema Kenya imeanza kuiga mfano huo.
Katika wiki za hivi karibuni, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imewashutumu waandalizi wa maandamano, wanaharakati wa mitandaoni, na wafadhili kwa “shughuli zinazohusiana na ugaidi,” ikitumia baadhi ya vipengele vya Sheria ya Kuzuia Ugaidi.
Serikali inadai vuguvugu la Gen Z linafadhiliwa na kuongozwa na mataifa ya kigeni kwa lengo la kuisambaratisha nchi, kauli inayofanana na zile zinazotumiwa na tawala za mataifa jirani.
Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, ametetea msimamo mkali wa serikali, akifichua kuwa watu zaidi ya 1,500 wamekamatwa kote nchini.Waliokamatwa wanakabiliwa na mashtaka ya ugaidi, mauaji, wizi wa kutumia nguvu, ubakaji, uchomaji mali na uharibifu wa mali. Lakini watetezi wa haki za binadamu wanasema mashtaka haya ni makali, yanachochewa kisiasa na yana nia ya kuwatia hofu vijana.
Wakili Paul Muite ameonya Idara ya Mahakama dhidi ya kutumiwa katika mateso ya kisiasa.“Kuweka masharti ya dhamana yasiyo ya haki kwa vijana wa Gen Z wanaokabiliwa na mashtaka ya ugaidi wa kisiasa kunakiuka haki ya kikatiba ya kupata dhamana kwa masharti yanayofaa chini ya Kifungu cha 49(1)(h). Mahakimu hawapaswi kuonekana kuwa sehemu ya Serikali Kuu,” aliandika Bw Muite.Jaji Mkuu mstaafu David Maraga amesema hatua za serikali ni ishara ya uoga.
“Wengi wa vijana walioshtakiwa hawajafikisha umri wa miaka 25 — fikiria kijana wa miaka 18 akishtakiwa kwa ugaidi katika hali ambazo, ukitazama kwa makini, hakuna kitendo chochote cha kigaidi,” alishangaa Bw Maraga, ambaye ametangaza nia ya kugombea urais mwaka wa 2027.Maraga alisema mashtaka hayo yanalenga kuwatisha vijana na familia zao.
Rais wa zamani wa Chama cha Mawakili Kenya (LSK), Nelson Havi, pia amekosoa serikali akisema vijana waliokamatwa ni 'watoto'. “Ningependa Murkomen afanye uchunguzi kuhusu Mapinduzi ya Ufaransa na kuelewa kilichosababisha kuuawa kwa Mfalme Louis XVI na mkewe Marie Antoinette.
Ilikuwa ni kwa sababu walikandamiza sauti ya wananchi; vijana ndio waliongoza mapinduzi hayo,” alionya Bw Havi.Muungano wa mashirika ya kijamii chini ya Kundi la Mageuzi ya Polisi pia ulilaani mashtaka na kukamatwa kwa vijana, ukisema yamechochewa kisiasa. Walitaka haki na uwazi kamili kuhusu vifo vya Wakenya 38 waliouawa Julai 7, majeruhi zaidi ya 500, na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.
“Katiba inapiga marufuku kuwekwa kizuizini kiholela kwa mtu kabla ya kesi. Kila mshukiwa ana haki ya kupata wakili, huduma ya afya, na nafasi ya kupinga kuzuiliwa kwake,” alisema Irungu Houghton, Mkurugenzi Mkuu wa Amnesty International Kenya.
Mkurugenzi Mkuu wa Transparency International Kenya, Sheila Masinde, alitoa wito kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Polisi Huru (IPOA) kuchapisha matokeo ya uchunguzi unaoendelea kuhusu vifo na majeraha hayo.
“Tunashtushwa na matumizi holela ya risasi katika maeneo ya makazi, hasa katika kaunti za Kajiado na Kiambu. Kwa sasa, angalau watoto saba wanatibiwa kwa majeraha ya risasi,” alisema Houghton.
Mwelekeo wa sasa wa Kenya unafanana na ule wa mataifa mengine Afrika Mashariki, ambako tawala zimeegemea sheria za kupambana na ugaidi kuzima upinzani.
Nchini Uganda, utawala wa Rais Yoweri Museveni umejulikana kwa kutumia sheria za usalama kuwashambulia wapinzani. Angalau wafuasi 36 wa upinzani walishtakiwa kwa ugaidi mwaka 2024 baada ya maandamano yaliyochochewa na chama cha National Unity Platform (NUP) cha Robert Kyagulanyi.
Nchini Tanzania, kiongozi wa upinzani Freeman Mbowe na wenzake — Halfan Bwire, Adam Hassan, na Mohammed Abdillahi — walizuiliwa kwa miezi minane kati ya katikati ya 2021 hadi Machi 2022 kwa mashtaka ya ugaidi.
Kukamatwa kwao kulitokana na madai ya kutaka mageuzi ya kikatiba.Nchini Ethiopia, Jawar Mohammed, kiongozi maarufu wa upinzani, alikamatwa mwaka 2020 na kushtakiwa kwa ugaidi, akidaiwa kuchochea ghasia za kikabila baada ya kuuawa kwa msanii maarufu Hachalu Hundessa.
Nchini Sudan Kusini, mwanaharakati Peter Biar Ajak alikamatwa mwaka 2020 na kushtakiwa kwa ugaidi baada ya kuzuiliwa miezi minane. Kukamatwa kwake kulifuata wito wake kuhimiza kuzingatiwa kwa demokrasia na uwezeshaji wa vijana.
Wanasheria wa kikatiba wanatahadharisha kuwa Kenya iko katika hatari ya kufuata mkondo huo wa kisiasa ikiwa sheria za usalama zitatumika kisiasa.
“Sheria za ugaidi ziliwekwa kwa ajili ya kushughulikia vitisho halisi, si kuwatisha vijana wanaoandamana. Matumizi mabaya ya sheria hizi yanaharibu demokrasia na kugeuza harakati za kiraia kuwa uhalifu,” alisema wakili wa kikatiba Waikwa Wanyoike.
Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2012, iliyotungwa wakati wa vitisho vya kundi la Al-Shabaab, sasa inatumika dhidi ya waandamanaji wanaobeba mabango na kutumia mitandao ya kijamii.
Wakosoaji wanasema mwelekeo huu unapotosha lengo la sheria hiyo. Wanaharakati na wanasheria wanaonya kuwa kuhusisha maandamano na ugaidi kunadhoofisha imani kwa mfumo wa haki na kunakiuka uhuru wa kujieleza, kuandamana na kuungana unaolindwa na Katiba.“Ikiwa serikali itamwita kila kijana anayepinga sera zake kuwa gaidi, basi tunakaribia utawala wa kidikteta.
Mashtaka haya si ya haki — ni njia ya kuwanyamazisha Gen Z,” alisema wakili wa haki za binadamu Njeri Mwangi.Mashirika ya msaada wa kisheria yanasema mamia ya waandamanaji waliokamatwa bado wanazuiliwa rumande, baadhi yao wakishindwa kutimiza masharti magumu ya dhamana.
Wengine hawajulikani waliko. Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR) inataka maelezo kutoka kwa Wizara ya Usalama wa Ndani kuhusu hatima ya waliopotea. Pia imetaka ukaguzi huru kuhusu mienendo ya polisi wakati wa maandamano hayo.
from Taifa Leo https://ift.tt/qCSc4kF
via IFTTT