Wabunge wanaounga mkono serikali kutoka maeneo ambayo upinzani umechacha wana sababu ya kuwa na tumbojoto huku wakazi wa maeneo yao wakiwasilisha maombi ya kuwaondoa ofisini kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC).
Duru zinasema makamishna wapya wa IEBC wanapokea maombi kutoka kwa wapiga kura wakitaka kuwaondoa wawakilishi wao katika Bunge la Kitaifa wanaodai wameegemea Serikali badala ya kutetea maslahi ya raia.
Jana, Mwenyekiti wa IEBC Edung Ethekon alisema kwamba tayari wamepokea rasmi maombi manne ya kutaka wabunge watimuliwe ofisini.Vyanzo kutoka ndani ya IEBC vimefichua kuwa maombi ya kuwaondoa wabunge yalipokewa kutoka kwa wananchi waliodai kuwa wabunge wao hawawakilishi vizuri.
Kulingana na afisa huyo ambaye hatuwezi kumtaja jina kwa kuwa sio msemaji wa IEBC, maombi ya kuwaondoa wabunge ofisini yalianza kuwasilishwa tangu mwanzo wa maandamano ya Gen Z mwaka jana.
Mengi ya maombi hayo yanatarajiwa kutoka kwa wapigakura wa eneo la Mlima Kenya, ambalo lilimchagua kwa wingi Rais William Ruto mwaka 2022 kabla ya kutofautiana na aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua.
Maombi mengine yanatarajiwa kutoka Ukambani, ngome ya kiongozi wa chama cha Wiper Party Kalonzo Musyoka.Kulingana na wachambuzi wa siasa, ingawa mchakato wa kuwaondoa wabunge ofisini si rahisi, idadi kubwa ya maombi inaonyesha wapiga kura wamekosa imani na wawakilishi wao.
“Mchakato wa kuondoa mbunge ofisini ni mgumu lakini pale unapoanzishwa huwa ni wazi kuwa wapigakura wamekosa imani na mbunge wao,” alisema mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.
Alisema kuwa licha ya mchakato kuwa mgumu na kwamba kuondolewa kwa mbunge kunaongezea tume zigo la kuandaa chaguzi ndogo, ni haki ya wapigakura kuwaondoa wabunge.
“Kama wapigakura wa eneo fulani wanahisi mbunge wao hawawakilishi vizuri, wana haki kisheria kuanzisha mchakato wa kumuondoa. IEBC ina jukumu la kutekeleza sheria,” alisema.
Miito ya kuwaondoa ofisini wabunge ilizidi kupata nguvu baada ya maandamano ya vijana wa Gen Z mwaka jana dhidi ya Mswada wa Fedha uliopendekeza ongezo la kodi.
Bunge lilipitisha mswada huo, lakini Rais Ruto akakataa kuutia saini kuwa sheria kutokana na shinikizo za umma.Wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba kinachoweza kuwaramba wabunge hao ni kuonekana kuwa waaminifu kwa Rais badala ya wananchi.
“Masaibu ya wabunge wanaolengwa ni ya kujiletea na kwa hivyo watabeba msalaba wao wenyewe. Hauwezi kuonekana ukiunga ajenda za serikali inayolaumiwa na raia na utarajie wapigakura waliokutuma Bungeni kuwawakilisha wakupende,” alisema.
Sheria inaruhusu wapigakura kuondoa mbunge wao kwa msingi wa ukiukaji mkubwa wa katiba au Sheria ya Uchaguzi, ufisadi, au ukiukaji wa kanuni za uadilifu.
Mchakato wa kuondoa mbunge lazima uanzishwe baada ya miezi 24 tangu uchaguzi mkuu, na sio ndani ya miezi 12 kuelekea uchaguzi unaofuatia.Mchakato huanza kwa kukusanya saini kutoka angalau asilimia 30 ya wapiga kura waliosajiliwa. Saini huambatanishwa na maombi yakieleza sababu na ushahidi wa kutaka kumuondoa mbunge ofisini.
IEBC huidhinisha ombi iwapo linatimiza vigezo vya kisheria na kutoa nafasi kwa mbunge kujitetea. Akiondolewa uchaguzi mdogo huandaliwa ndani ya siku 90.
Wiki iliyopita, Seneti ilianzisha mchakato wa kuweka mfumo wa kisheria unaoweza kuwawezesha wapigakura kuwaondoa ofisini wabunge na madiwani kabla ya muda wao kuisha. Kamati ya Seneti kuhusu Sheria ilimtaka Mwanasheria Mkuu kuandaa mfumo wa sera na sheria kabla ya Februari 26, 2026 .
Miito imetolewa mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa aondolewe kwa misimamo yake ya kutetea serikali. Kimani ni mshirika wa karibu wa Rais Ruto na wakosoaji wake wanasema mtindo wake wa uongozi umekasirisha wakazi.
Mbunge wa Machakos Mjini Caleb Mule na Mwengi Mutuse wa Kibwezi wanakabiliwa na tishio la kuondolewa ofisini kwa kuunga mkono hoja ya kumng’atua Gachagua bila kuwahusisha wapiga kura wa maeneo yao.
Wabunge wengine ambao miito ya kuwaondoa imetolewa ni Erick Wamumbi (Mathira), Esther Passaris (Mwakilishi wanawake Nairobi), Beatrice Elachi (Dagoretti Kaskazini), Seneta Mwenda Gataya (Tharaka Nithi), na Fatuma Jehow (Mwakilishi Wanawake Wajir).
from Taifa Leo https://ift.tt/zUfmP51
via IFTTT