Uhuru ahimiza vijana kuwa wabunifu kutatua changamoto za Afrika

Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa vijana wa Kenya na bara zima la Afrika kujikita katika ubunifu na kujenga uwezo ili kusaidia Afrika kukabiliana na changamoto zake.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mama wa Taifa wa zamani, Margaret Kenyatta, kwenye Mahafali ya 6 ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amref kilichoko Northlands, Nairobi, Rais mstaafu alisisitiza umuhimu wa afya ya msingi katika kutatua matatizo ya kiafya barani Afrika.

"Leo ni mwanzo wa maisha ya kujitolea kwa kazi. Ninyi ndio matumaini ya mustakabali wa Afrika. Kwa hakika, mustakabali wa afya ya Afrika uko mikononi mwenu. Kuanzia leo, sera na ubunifu, utafiti wa hali ya juu, huduma ya msingi ya afya, huruma, teknolojia mpya na kila linalohitajika kuboresha huduma ya afya barani ni jukumu lenu. Dunia inawasubiri muonyeshe weledi na ari yenu. Rasilmali kubwa zaidi ya Afrika ni watu wake na uwezo wao," ilisema sehemu ya hotuba hiyo.

Alikumbuka jinsi janga la Covid-19 lilivyoathiri nchi na bara kwa ujumla, akisema lilidhihirisha umuhimu wa kuwa na mfumo imara wa huduma ya msingi ya afya.

"Janga hilo lilitulazimisha kubuni upya mikakati kama nchi na kama bara kuhusu umuhimu wa kuwa na ubunifu wetu wenyewe, viwanda vya kutengeneza dawa, na maabara zetu binafsi. Kama tungekuwa na uwezo wetu, tusingetegemea mataifa ya Magharibi," alisema.

Wakati wa hafla hiyo ya mahafali, Mkurugenzi Mkuu wa Amref Health Africa, Dkt Githinji Gitahi, alimpongeza Bw Kenyatta kwa kutoa eneo la kimkakati lililowezesha kuanzishwa kwa chuo hicho.

"Alikuwa anatafuta jambo litakalokuwa na athari chanya kwa jamii, nikamueleza kuhusu huduma ya afya ya msingi. Tunashukuru kwa kupokea ekari 50 za ardhi Northlands ambapo sasa tumejenga taasisi ya kisasa inayolenga kuendeleza uwezo wa vijana kuleta suluhisho la afya ya msingi barani Afrika," alisema Dkt Gitahi.

Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amref kimeibuka kuwa kitovu muhimu cha mafunzo kwa wataalamu wa afya barani, wanaopatiwa si tu maarifa, bali pia uelewa wa kisiasa, kisera na utafiti kuleta mageuzi katika afya ndani ya bara.

Chuo hicho kilianzishwa na Amref Health Africa mnamo 2017, kikapokea Barua ya Mamlaka ya Muda kutoka kwa Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu ya Kenya (CUE) kuanzia Agosti 1, 2017.



from Taifa Leo https://ift.tt/vBL4ECy
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post