Mshikemshike wazuka ODM shutuma zikitanda kwamba inapendelea Boyd Were

CHAMA cha ODM kinakabiliwa na mtihani mkubwa kuhusu uteuzi huku uchaguzi mdogo wa Kasipul ukitarajiwa utafanyika mnamo Novemba 27.

Mshikemshike umekumba wawaniaji kuhusu mbinu ya uteuzi itakayotumika huku kukiwa na hofu kuwa chama kitampendelea Boyd Were.

Uchaguzi huo mdogo utaandaliwa kufuatia mauti ya aliyekuwa mbunge Ong'ondo Were mnamo Aprili.

Kampeni tayari zimechacha huku wawaniaji mbalimbali wakipanga kuchukua kiti hicho.

Kuna hofu kuwa ODM inachelewesha mchakato wa kufanya uteuzi ili kumpa Bw Were tikiti ya moja kwa moja siku za mwisho kabla ya makataa ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) kufika.

Tofauti zimezuka kati ya wasomi, wanasiasa na wapigakura jinsi ambavyo ODM inastahili kushughulikia uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge Kasipul Evance Ndege amepinga vikali shutuma na shinikizo ambazo zinaelekezewa ODM kufanya mchujo wa wawaniaji.

Bw Ndege alisisitiza kuwa ODM ina haki ya kutoa tikiti ya moja kwa moja, kuandaa mchujo au kuafikiana kuhusu nani wa kupokezwa tikiti ya kupeperusha bendera yake kwenye uchaguzi huo mdogo.

“Hakuna mwenye mamlaka ya kuamrisha ODM na bado hatujapokea mawasiliano yoyote kutoka makao makuu ya chama. Kwa hivyo, watu watulie,” akasema Bw Ndege akihutubu katika kijiji cha Karabok.

Naibu Kiongozi wa Wanawake Walemavu Akilias Abongó na Kiongozi wa Vijana Edward Otina, nao walionya dhidi ya uteuzi wa ODM kuingiliwa.

Nalo vuguvugu jingine linaloongozwa na Tom Okoko limeonya kuwa hawatakubali ODM iwalazimishie mwaniaji na raia wanastahili kupewa nafasi ya kuamua nani atapeperusha bendera ya chama hicho.

Bw Okoko alisema wafuasi chama watakata tamaa Kasipul na Homa Bay nzima iwapo chama kitawaamulia mgombeaji.

“Tayari kuna wanasiasa ambao wanashinikiza Were apokezwe bendera na hii si tabia ambayo watu wanataka. ODM lazima ihakikishe kuwa uteuzi ni huru na haki,” akasema Bw Okoko.

Alitaja tukio ambalo maafisa wa kaunti walinaswa kwenye video wakimpigia kampeni kali Were mwanawe marehemu Bw Ong’ondo.

Profesa Silvance Abeka pia alisema kuwa kimya cha ODM kuhusu uteuzi, muda na tarehe kinaongeza tu taharuki na madai kuwa wanampendelea mwanawe marehemu Bw Were.

“ODM imewahi kupoteza viti hapo awali baada ya uteuzi kusimamiwa vibaya. Wapigakura waliadhibu chama debeni, hatufai kuelekea njia hiyo,” akasema Bw Abeka.

Kando na Boyd, wengine ambao wanawania kiti hicho ni Mfanyabiashara Philip Aroko, Robert Riaga anayefahamika kama Moneybior, Dkt Adel Ottaman, aliyekuwa mwanahabari wa Redio George Otieno maarufu kama Ajo Mbuta, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Newton Ogada na Rateng’ Otiende miongoni mwa wawaniaji wengine.



from Taifa Leo https://ift.tt/xyVFIqw
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post